Germany celebrating after winning the final of the FIFA Women's World Cup, China 2007, the 30th of september 2007 in Shanghai. Photo from FIFA.com
_____________________________________
na Freddy Macha.
__________
Ajabu wanawake wengi nilioongea nao wala hawajui. Hawafahamu Kombe la Dunia la Kandanda limekuwa likichachatika nchini China kwa majuma kadhaa:
”Ah Mpira sipendi…”
“Lakini ni wanawake wanacheza.”
“Ah, mpira unaniboa.”
“Lakini wanawake wamekuwa wakicheza vizuri sana.”
“Ah mpira mambo ya wanaume.”
“Ni wanawake wenzio wanacheza.”
“Aka…”
Chukua mechi ya nusu fainali kati ya Brazili na Marekani. Tazama alivyoonyesha vitu, Marta namba Kumi wa Brazili. Mtangazaji mmoja wa BBC akasema, “Anavyocheza na kuchenga Marta ni kama Maradona…”
Na kweli. Marta alichaguliwa mchezaji bora wa FIFA mwaka huu. Kafunga mabao mengi kuzidi wenzake pamoja na kwamba walitolewa na Ujerumani leo. Pamoja na kwamba aliwatwanga Marekani 4-0 na wengine wengi ikiwemo New Zealand. Lakini mpira ni nini? Si mchezo tu? Kwanini wapo mabondia wa kike na wakimbiaji wa kike? Kwanini wanawake hawastuki kuwa mashindano haya kabambe yamekuwa yakichangamsha Uchina nzima? Ukweli nimetazama karibu mechi zote toka mwanzo na mtazamo wangu kuhusu mpira wa wanawake yamebadilika kabisaaaa….Wanawake wanacheza vizuri, wana ufundi, wanafunga pia mabao mazuri, wanachenga, wana hamasa kama vile walivyo wanaume.
Nimeelezwa sababu za wanawake wa kileo kutopenda mpira mathalani hapa UIngereza zinatokana na historia. Mpira ulifutwa na shirika la Mpira la Taifa (FAT) mwaka 1965 baada ya kugundua wanawake walikuwa wakianza kuwazidi wanaume, kusahau kuwapikia, kutunza nyumba au kukaa na watoto. Na hilo limo limeenea jamii nyingi nyingine. Vyombo vya michezo haviungi mkono. Nchini Brazili ambapo mwaka huu tumewaona wanasoka hatari (ukiacha Marta), Christiane, Daniela na Formiga (maana yake Sisimizi, kwa Kireno)…hakuna shirikisho la mpira wa wanawake, lakini baada ya kuona jinsi walivyosisimua kule Beijing, serikali ya Brazili imeamua kuanzisha “FAT ya wanawake.”
Uingereza ilitolewa na Marekani katika robo fainali. Lakini pamoja na kutolewa wamekuwa na mchezaji stadi Kelly Smith. Vyombo vya habari havikuwa vikionyesha haya machuano. Magazeti kimyaaaa….wanasafu maarufu wa kike kimyaaa…. Runinga ilikuwa ikiyaonyesha usiku wa manane ambapo mabundi machache (kama mimi) ndiyo huwahi kuyatazama. Vyombo vya habari havikusaidia, mashirika ya michezo havikusaidia, historia nayo haikusaidia, wanawake nao hawaupendi mchezo….sasa iliyobaki moja. Kusema ukweli mashindano haya yalikuwa mazuri. Labda kulikuwa na udhaifu mdogo katika magolikipa (kama wa Ghana na Argentina aliyefungwa mabao Kumi na Moja na Wajerumani) lakini wapo magolikipa waliotia fora (kama wa Ujerumani ambaye hakuingizwa hata bao moja hadi mwisho)…na ushahidi mmoja umethibitishwa. Mpira wa wanawake, upendwe na baadhi ya wanawake au usipendwe umeingia kwa kishindo mwaka huu. Kwetu Bongo wasichana wanaoonyesha vipaji wapewe moyo, tusiwanyime ruhusa.
Mchezaji hatari wa Uingereza Kelly Smith alisema katika mahojiano karibuni kuwa alipokuwa mdogo alikuwa akizuiwa na wasichana wenzake, ndugu zake, wanaume kwa wanawake asicheze. Hakukatazwa. Leo ni mmoja wa wanamichezo wakuheshimika duniani. Kaitwa Zidane wa kike…
Kutoka: http://kitoto.wordpress.com
No comments:
Post a Comment