
Na Muhibu Said.
HARAKATI za kutaja orodha ya vigogo 11 wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi wa mabilioni ya fedha za umma nchini, zimeingia katika sura mpya, baada ya Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Willibrod Slaa, kupeleka orodha hiyo katika Baraza la Congress, nchini Marekani.
Dk Slaa ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema, aliondoka nchini Oktoba Mosi, mwaka huu, kuelekea Marekani ambako anatarajia kukutana na wajumbe wa baraza hilo katika ziara iliyoandaliwa na Shirika moja la Kidini ambalo limekuwa likichangia maendeleo katika Jimbo la Karatu.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho taifa, Kabwe Zitto amethibitisha suala hilo na kusema kuwa Dk Slaa huyo, anatarajiwa kuwapo nchini humo kwa kipindi cha wiki mbili, kuanzia Oktoba Mosi hadi 19, mwaka huu.
Zitto alisema katika mkutano huo, Dk Slaa ataelezea hali halisi ya kisiasa Tanzania pamoja na tuhuma za ufisadi alizozielekeza kwa baadhi ya wanasiasa hivi karibuni.
Tayari viongozi sita wa serikali, walishatoa taarifa kwa waandishi dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwao kwa nyakati tofauti, huku baadhi wakikanusha kuhusika, wengine wakitangaza kumshtaki mahakamani Dk Slaa na wengine wakizipuuza tuhuma hizo kwa sababu hazihitaji kutolewa maelezo kwa sababu walizosema kuwa tuhuma hizo si mpya kutolewa maelezo.
Viongozi hao, ni pamoja na Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Patrick Rutabanzibwa na Waziri Mkuu Edward Lowassa.
No comments:
Post a Comment