Wednesday, November 07, 2007

Kikwete amrejesha Makamba kundi la vigogo CCM.



* Kusaidiwa na makapteni wawili

* Kingunge, Sumaye nje Kamati Kuu

* Waliotemwa sekretarieti kupangiwa kazi

* Salim, Msuya waula, nane kuteuliwa

Na Midraji Ibrahim, Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekamilisha kupanga safu ya uongozi wake, huku Katibu Mkuu, Yusuf Makamba akifanikiwa kubaki kwenye nafasi yake na mwanasiasa wa siku nyingi, Kingunge Ngombale-Mwiru akitupwa nje ya Kamati Kuu (CC) ambamo amedumu kwa kipindi kirefu.

Kingunge ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano Jamii), alipendekezwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kwa

halmashauri kuu, lakini akadondoshwa kwenye kura.

Kigogo mwingine aliyeangushwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye katika kura za NEC aliibuka na ushindi mnono.

Akizungumza baada ya kikao hicho jana mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, alisema Mwenyekiti wa chama aliwaeleza wajumbe kwamba waliokuwemo sekretarieti iliyopita watapangiwa kazi nyingine na kwamba isichukuliwe kuwa walishindwa kazi.

Watendaji wote waliokuwemo kwenye Sekretarieti iliyopita wameondolewa isipokuwa Makamba anayeendelea kuwa Katibu Mkuu. Waliondolewa ni Naibu Katibu Mkuu, Jaka Mwambi, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Aggrey Mwanri na Mweka Hazina, Rostam Aziz.

Awali, taarifa zilisambaa kwamba Rostam alikuwa amejiuzulu nafasi hiyo kutokana na shughuli zake za biashara, lakini alipoulizwa alisema kuondolewa kwake ni uamuzi wa Mwenyekiti wa chama.

Katika sekretarieti mpya, Naibu Katibu Mkuu anakuwa Mbunge wa Newala, Kapteni George Mkuchika, Uchumi na Fedha imechukuliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana, Amos Makalla, Itikadi na Uenezi anakuwa Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Kapteni John Chiligati na Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje ni Benard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa.

Upande wa Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu, Ramadhan Saleh Feruzi, anaendelea na wadhifa huo.

Wajumbe Kamati Kuu ni Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, Mbunge wa Viti Maalum, Pindi Chana, Naibu Spika wa Bunge, Anna Makinda, Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda, Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Majina mengine yaliyodondoshwa upande wa Bara ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Guninita John Guninita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, William Kusila, Dk Rehema Nchimbi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Mizengo Pinda na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.

Upande wa Zanzibar waliopitishwa ni Waziri Kiongozi mstaafu, Dk Gharib Bilal, Naibu Waziri Miundombinu, Dk Maua Daftari, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib, Fatma Saidi Ali, Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Omar Yusuf Mzee na Waziri wa Biashara, Viwanda na Utalii, Samia Suluhu Hassan.

Waliokuwa wamependekezwa na kudondoshwa ni Mwajuma Majid Abdallah, Ali Mzee Ali, Machano Othman Saidi, Salim Hamad Saleh, Usi Yahya Haji, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yusuf Himid, Haroun Ali Suleiman na Hamad Masauni Yusuf.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Mwenyekiti anatakiwa kupendekeza majina yasiyozidi 30, majina 15 kutoka kila upande wa muungano; ili yachaguliwe majina saba kutoka kila upande na miongoni mwa watakaochaguliwa wanawake wasipungue wawili.

Kulingana na Katiba ya CCM, Mwenyekiti wake anaruhusiwa kuchagua wajumbe 10 kuingia kwenye NEC. Walioteuliwa ni Mawaziri Wakuu mstaafu, Cleopa David Msuya na Salim Ahmed Salim.

Msekwa alisema, Rais Kikwete alisema hakuteua kujaza nafasi zote kwa sababu anaendelea kuangaza wengine wanaoweza kumsaidia.

Pia, Rais Kikwete alisema kikao cha halmashauri kuu kijacho kitafanyika Butiama, Mara kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere na kwamba maandalizi ya kikao hicho yatafuatiliwa kwa karibu na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono.

No comments: