*Asema wengi humaliza vifungo kabla ya rufaa kusikilizwa
Na Andrew Msechu
UTAFITI uliofanywa na mfungwa aliyehitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria wiki iliyopita, Haruna Pembe Gombela umeibua vikwazo vinavyowakwamisha wafungwa kukata rufaa kwa wakati na hivyo kuendelea kusota magerezani bila sababu.
Katika utafiti uliofanywa katika gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, mfungwa huyo ambaye ni wa kwanza nchini kufanya hivyo akiwa gerezani, amesema ni vigumu kwa wafungwa wengi kukata rufaa wakiwa gerezani kutokana na kutokufahamu taratibu na kukosa msaada wa vifaa na ushauri na ukiritimba wa watu wa mahakama.
Kwa mujibu wa Gombela tatizo kubwa linalowakwamisha wafungwa hao ni kutokuwa na ufahamu juu ya haki zao ikiwemo haki ya kukata rufaa.
Katika utafiti wenye kurasa 41, Gombela anabainisha kuwa ukiritimba wa maafisa wa mahakama katika utoaji wa hati za hukumu nalo limekuwa ni tatizo kwa wafungwa wengi na kusababisha washindwe kukata rufaa.
Kwa upande wa Magereza Gombela anaeleza katika utafiti huo kuwa hakuna vitendea kazi vya kutosha, kama vile mashine za kupiga chapa na vingine vya kuwasaidia wafungwa kutafuta haki zao kwa njia ya rufaa.
Vile vile anazungumzia matatizo yatokanayo na watumishi wa magereza, "Matokeo (ya utafiti) yanaonyesha kuwa wataalamu wengi wa sheria wanaotakiwa kuwasaidia wafungwa katika kukata rufaa, wamekuwa hawatoi msaada wa kutosha, hasa kwa mtazamo kuwa taratibu zao haziwaruhusu kuwa karibu na wafungwa, lakini hii inachochewa kwa kiasi kikubwa na utawala wa magereza," inasomeka sehemu ya utafiti huo.
Aliongeza kuwa hatua hiyo imekuwa ikisababisha wataalamu hao kujiweka mbali na wafungwa na matatizo yao, hatua ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kukwama kwa uandaaji wa rufaa na matatizo mengine ya wafungwa.
Matatizo mengine anayoainisha mtafiti ni utaratibu wa kutuma hati za hukumu wa njia ya Posta hivyo baadhi yake kuchelewa na kuwanyima wafungwa waliotumiwa haki ya kukata rufaa. Vile vile anadokeza kuwa hakuna utaratibu ulio na wazi wa kuhakikisha kuwa hati hizo zinamfikia mfungwa mapema bila kujali kuwa ana nia ya kukata rufaa au la.
Gombela anasema msongamano wa kesi katika mahakama unachelewesha mashauri na kuwa kikwazo kwa wafungwa kukata rufaa kwa kuwa wengi wao hujikuta wakimaliza muda wao wa adhabu na kuruhusiwa kabla rufaa zao hazijasikilizwa.
"Mabadiliko ya mara kwa mara ya mawakili wa serikali na majaji wanaosikiliza rufaa hizi yanawafanya wapya wanaokabidhiwa majukumu kuomba muda zaidi kwa ajili kufanya mapitio ya muendelezo wa rufaa hizo ili kujua namna atakavyoweza kuziendeleza, lakini pia kikwazo kingine ni mlolongo mrefu usiokuwa na sababu yoyote ya msingi," alisisitiza. Kwa mujibu wa mfungwa huyo, jambo jingine linalokwamisha hata jitihada za uongozi wa Magereza katika kusimamia suala la rufaa kwa wafungwa ni ongezeko la kasi la wafungwa wapya siku hadi siku na kuwafanya wshindwe kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa uwiano wa ongezeko hilo.
Katika utafiti wake, Gombela anapendekeza kuwa hati za rufaa ziandaliwe mahakamani badala ya gerezani na kusajili mara moja baada ya mtuhumiwa kupatikana na hatia na kuhukumiwa.
Anapendekeza pia wizara inayohusika iyapatie magereza vifaa vitakavyowasaidia wafungwa kukata rufaa kwa wakati na kuajiri watumishi wenye ujuzi wa kuvitumia. Vile vile anawataka wanasheria waliopo magerezani kuwa huru ili kuwasaidia wafungwa kupata msaada wa kisehria unahotajika.
Akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa msaada wa kisheria, mfungwa huyo anaweka bayana kuwa yeye binafsi kati ya mwaka jana na mwaka huu amewasadia wenzake kwa kuandaa rufaa 90 ambazo tayari kesi zake zimeshapangwa kuanza kusikilizwa na ameandaa hati 30 za nia ya kukata rufani kwa wakati Utafiti huo ulifanywa kwa kuwahoji wafungwa waliokuwa wakishughulikia rufaa zao katika gereza la Ukonga na wale wote waliokuwa wakipelekwa gerezani humo kwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wakitokea kwenye magereza yaliyopo mikoa mingine.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu huria nchini (OUT) aliyemsimamia Gombela katika utafiti huo, Benhajj Masoud, alimwelezea mwanafunzi wake huyo kuwa miongoni mwa wanafunzi waliomfurahisha hasa kwa kuweza kufanya marekebisho yote yaliyotakiwa kwa wakati.
Katika mazungumzo maalum na Mwananchi Jumapili, Masoud alisema Gombela alikuwa akimshangaza kutokana na namna alivyokuwa akitekeleza wajibu wake kwa wakati licha ya mazingira magumu aliyokuwa nayo.
Alinifurahisha sana, huyu ni miongoni mwa wanafunzi wepesi kuelewa na kutekeleza katika wachache niliowahi kukutana nao kwani tangu alipoelekezwa utafiti wake ulifanyiwa marekebisho machache mara tatu na ulipokuja mara ya nne haukurudi tena, ulikuwa umekamilika, alisema.
Aliongeza kuwa Gombella alikuwa akipatiwa mafunzo juu ya namna ya kufanya utafiti kwa ushirikiano wake na baadhi ya wakufunzi wa OUT waliokuwa wakipangiana zamu na maeneo ya kumwelekeza. Hata hivyo, Masoud anasema kazi yote ya utafiti huo aliifanya Gombela mwenyewe na ndiye mwenye hatimiliki.
Alisema suala la kujivunia ni kuwa eneo ambalo mfungwa huyu alilifanyia utafiti halikuwahi kufanyiwa utafiti na mtu mwingine yeyote hivyo matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kuwa changamoto kwa mamlaka husika na wasomi wanaohitaji kuutumia kwa ajili ya kukamilisha masomo yao.
Utafiti huo unaelezea matatizo yanayowapata wafungwa mara wanapoingia gerezani na kuhitaji kukata rufaa kupinga adhabu walizopewa, lakini pia njia zinazoweza kuchukuliwa ili kupunguza matatizo hayo.
Kutoka gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment