Mfungwa aliyepata shahada alonga
Halima Mlacha
HabariLeo; Thursday,November 01, 2007 @00:08
MFUNGWA wa kwanza katika historia ya Tanzania kutunukiwa shahada ya kwanza ya sheria akiwa gerezani, Haruna Gombela ameeleza mazingira aliyokutana nayo na kumwezesha kupata mafanikio hayo.
Mfungwa huyo ambaye anatarajiwa kutoka kifungoni mwaka 2025, hata hivyo hakuweka wazi kosa lililosababisha afungwe.
Gombela ambaye alihukumiwa mwaka 1998 kifungo cha miaka 50, alitunukiwa cheti chake jana katika mahafali ya 20 ya Chuo Kikuu Huria (OUT) yaliyofanyika katika Bwalo la Magereza ya Ukonga.
Kamishna Mkuu wa Magereza Tanzania, Augustino Nanyaro, alisema tukio la kutunukiwa shahada kwa mfungwa akiwa gerezani ni la kwanza katika historia ya Tanzania na gereza.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kutunukiwa shahada yake hiyo, Gombela alisema jambo kubwa lililomfanya kusomea sheria, ni baada ya kuona wafungwa wenzake wakisumbuliwa na matatizo madogo ya sheria.
“Nikiwa ndani ya gereza niliona wafungwa wenzangu wakikabiliwa na matatizo ya sheria ndogo ndogo na pia niliona muda wangu wa kutoka ambao ni mwaka 2025 ni mrefu hivyo sikuwa na kazi ya kufanya zaidi ya kuamua kujiendeleza katika elimu,” alisema.
Kwa mujibu wake, alipata usajili wa kujiunga na OUT mwaka 1999 lakini hakuanza masomo mara moja kutokana na sababu za kisheria na badala yake, alianza mwaka 2004.
Alisema alikuwa akipata msaada kutoka kwa walimu, Magereza na wanafunzi wenzake. Alisema awali alifadhiliwa na familia yake na baadaye wakajitokeza watu wengine, kikiwamo Chuo ambacho kilimfadhili.
Gombela alisema ataitumia elimu yake hiyo katika kuwasaidia wafungwa wenzake kisheria. Alisema hadi sasa ameshawasaidia wafungwa zaidi 90 kuwaandalia rufaa zao
Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa OUT, Paul Kihwele alimwelezea Gombela kuwa ni miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakijituma na amekuwa akifanya vizuri pamoja na kuwa katika mazingira ya gerezani.
Kwa mujibu wa Kihwele, katika ripoti yake ya utafiti uliohusu matatizo ya wafungwa katika kupata rufaa, alipata alama daraja la pili.
Naye Mkuu wa Gereza la Ukonga, Kamishna Msaidizi wa Polisi Samweli Nyakitina, alisema kufanikiwa kwa mfungwa huyo kumetokana na ukaribu uliokuwapo kati ya walimu wake na Magereza.
Alisema gereza hilo lilimpangia ratiba ya kazi ambayo ilimwezesha kujisomea na kuwasaidia wenzake kwa kuwaandikia rufaa hali iliyompa nafasi ya kufanya vizuri. Alimwelezea mfungwa huyo kuwa anajituma na ni msaada mkubwa kwa wenzake.
Nanyaro alisema mhitimu huyo, atatumiwa na Jeshi la Magereza kama mfano na hamasa kwa wafungwa wengine ili na wao wawe na moyo wa kujiendeleza katika elimu kwani umefika wakati wa kuliona gereza kama siyo mahala pa kutumikia adhabu pekee bali kujifunza na kujiendeleza kwa manufaa ya mhusika na taifa kwa ujumla.
Alisema Gombela atapewa fursa na gereza hilo ya kuwaelimisha wenzake pamoja na kuwapa msaada wa kisheria ikiwa ni pamoja na kufanya kazi katika Ofisi ya Sheria ya gereza hilo.
Kwa upande wa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, John Malecela alimpongeza mfungwa huyo kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM kwa kujiendeleza na kuwasaidia wenzake hivyo alihimiza wafungwa wengine kuiga mfano wake.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Tolly Mbwete alisema chuo hicho kimeamua kumpa nafasi ya kujiendeleza zaidi kwa kumfadhili katika shahada ya uzamili ya sheria kama Gombela atakuwa tayari na chuo hicho kitakuwa kikimpatia mahitaji yote ya masomo bila ulazima wa kutoka nje ya gereza hilo.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na familia yake, Rais wa wanafunzi wa OUT, Vincent Magendela, alisema tukio hilo limewatia moyo hasa baada ya kumuona mwenzao anajitihada za kusoma bila kujali mazingira magumu aliyonayo jambo lililowahamasisha wanafunzi hao kumchangia fedha za kujikimu na masomo.
Gombela ana watoto wanne ambao ni Halima, Jaffari, Bahati na Leila Haruna. Mama yao alifariki mwaka 2000 na hivyo kulelewa na mjomba wao, Said Mohammed.
No comments:
Post a Comment