Friday, November 09, 2007

Rai ya Jenerali Ulimwengu



Ni uongozi, basi.

MANTIKI ya msingi kabisa katika hayo niliyosema wiki iliyopita ni kwamba ili tuweze kuendelea tunahitaji vitu vinne: Mosi, uongozi bora, pili, uongozi bora, tatu, uongozi bora na nne, uongozi bora.

Basi.Vingine, kama nilivyosema, tunavyo, kuacha siasa safi, ambayo haina budi kutokana na uongozi bora. Hili ndilo suala litakalotusumbua kwa muda mrefu, na kabla ya kulidurusu ipasavyo na kulipatia ufumbuzi, hakuna matumaini ya kupiga hatua yo yote ya maendeleo. Tutaendelea kusuasua na kubabaisha; tutakimbilia kunukuu mafanikio ya kitakwimu na maliwazo ya sifa za kinafiki za “wafadhili”, lakini hatua endelevu za kimaendeleo hazipigwi katika mazingira yaliyokosa uongozi bora.

Sasa inabidi kujadili dhana yenyewe ya uongozi bora, kwa sababu kwa jinsi tulivyoivuruga dhana ya uongozi katika nchi hii haitashangaza iwapo tutashindwa kuelewana kuhusu dhana yenyewe.

Iwapo nafasi nyingi zinazoitwa za uongozi zimekamatwa na walaghai, matapeli mabazazi na mafisadi, nadharia juu ya ‘uongozi’ itasaidia nini wakati wananchi wamekuwa wakiona sifa mbovu na matendo machafu ya hao wanaojiita viongozi?

Hata hivyo hatuna budi kuendelea kukumbushana kuhusu sifa zinazotakiwa kuambatana na uongozi. Ni kitu gani kinachomfanya raia au mwanajamii awe kiongozi, tofauti na raia au wanajamii wengine?

Hapana shaka kwamba haya nitakayosema hapa ni yale yale yaliyosemwa miaka yote hii. Lakini ukweli ni kwamba matendo yetu hayaendani kabisa na sifa hizi ninazozizungumzia . Namwalika msomaji azipitie tena sifa hizi, halafu aamue mwenyewe ni lini mara ya mwisho aliwahi kukutana na kiongozi.

Kwanza kabisa hana budi kuwa na sifa kadhaa ambazo zinampambanua na wengine, sifa zinazowafanya raia na wanajamii wengine wamwone kama mfano wa kuiga, kama funzo la kujifunza, kama njia ya kufuata.

Hii ina maana kwamba ana hulka, tabia, mwenendo, na lugha ya uungwana; anao uadilifu mkubwa katika kufuata maadili yanayoiongoza jamii; hana ubinafsi na yuko tayari kujitolea kuwasaidia wanajamii wenzake, hata kama kufanya hivyo kutamtwisha gharama, kumpotezea muda au kumsababishia matatizo mengine.

Pia ni mjuzi wa mambo, kwa kuwa anajibidiisha kujielimisha na kujipatia taarifa ambazo zinamwezesha kujua mwelekeo wa jamii yake, nchi yake na dunia nzima, na sifa hii inamwezesha kuwa na msaada kwa jamii yake. Kuongoza ni kuonyesha njia, na ili mwanajamii aweze kuwaonyesha wenzake njia, hana budi kuwa na ari na uwezo wa kutaka kujua na kuweza kukieleza hicho alichokipata kwa ufasaha ili wenzake wamwelewe na, kwa kumfuata, wanufaike nacho.

Pamoja na ujuzi wake na uwezo mkubwa wa kupata taarifa na maarifa kiongozi wa asili hajengi kiburi kinachotokana na kujua, na wala hawaonyeshi dharau wenzake kwa sababu anajua kwamba hata mwanajamii asiyejua mambo mengi naye anao mchango wa kutoa.

Kwa hakika busara kubwa za kijamii zimesinzia ndani ya wanajamii wenye akili za kawaida tu, ambazo zinasubiri kiongozi wa kweli azitambue, azitekenye na kuzileta nje, kisha aziunganishe pamoja ili kujenga busara ya pamoja ambayo haiwezi kulinganishwa na busara za mtu mmoja, hata zingekuwa kubwa kiasi gani.

Kiongozi asilia hapendekezi jina lake, wala hajitokezi kusema anataka kuwa kiongozi. Kiongozi wa kweli huonekana na kutambulika ndani ya jamii yake, na akiisha kutambulika, hubebeshwa majukumu ya uongozi, na mara nyingi atasita kuyakubali majukumu hayo, kimsingi kwa sababu anajua kwamba ni mzigo anabebeshwa, si nafasi ya kula anayopewa. Anajua kwamba uongozi rasmi, tofauti na ule wa kujitolea bila kuwa na ofisi, una maana kwamba atakuwa na muda kidogo zaidi wa kushughulikia mambo yake binafsi, na biashara zake zinaweza zikaathirika.

Aidha kiongozi ni mtu mwenye misimamo inayoeleweka na kutabirika. Kutokana na jamii anayoiongoza, kiongozi anakuwa na misimamo kuhusu mambo yote makuu na muhimu yanayoihusu jamii yake, na misimamo hii haina budi kutabirika, ili anaowaongoza wasilazimike kubahatisha au kupiga ramli ili kujua msimamo wake utakuwa upi kuhusu suala la msingi.

Katika umoja wa majizi, mathalan, wezi wote watajua kwamba kiongozi wao akipewa taarifa kwamba mmoja wao amevunja benki na kuchota mamilioni ya shilingi, atampongeza na kumpandisha cheo, kumfanya jambazi mfawidhi.

Lakini akijua kwamba mmoja wao anawasiliana na polisi ili kuusaliti umoja wake wa wezi, atamchinja.Huyu ni kiongozi. Anatabirika.

Katika umoja wa watu walioapa kuitumikia nchi yao na watu wake na wakasema “Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie”, iwapo kiongozi atapewa taarifa kwamba mmoja wa watu wake walioapa hivyo anafanya mambo yanayohujumu nia yao ya pamoja ya kuitumikia nchi, kisha watu wasijue atachukua hatua gani dhidi ya msaliti huyo (kwa kuwa msaliti mmoja aliwahi kufungwa lakini wasaliti wengine wakapandishwa vyeo) huyo si kiongozi, kwa sababu hatabiriki, ni kigeugeu, hana msimamo.

Kutabirika huku kunakwenda sambamba na ujasiri. Mtu asiyetabirika ni mwoga anayebadili msimamo wake kila mara kutegemea amekabiliwa na nani na ana maslahi gani kwa wakati huo. Kutokana na woga atasema maneno tofauti katika nyakati tofauti kwa watu tofauti ili kumpendeza kila mmoja. Tofauti yake na malaya ni biashara wanazofanya, lakini mwenendo ni sawa sawa.

Katika mazingira yetu nchini na barani Afrika ni dhahiri tunahitaji uongozi wa aina fulani, lakini imekuwa vigumu mno kuupata. Tunahitaji uongozi wa kujitoa mhanga, kwa sababu hali yetu ni mbaya, kama nilivyosema mapema, na inazidi kuwa mbaya; watu wetu wanateseka na umsikini ambao hauelezeki tukiangalia raslimali zilizowazunguka; ipo hatari ya kweli ya watu wetu kufikia hatua ya kusema, “Ah, liwalo na liwe, tumechoka na hali hii!”

Dalili zinajitokeza taratibu, lakini watawala wetu, kwa ustadi wao wa kubeza, uliochanganyika na “shibe mwanamalevya” hawatambui alama za nyakati.Wanabeza bila kujua kwamba wanaibeza Historia. Wakija kulitambua hilo, jua litakuwa limekuchwa.

Nchini mwetu utapeli, ubazazi na ubabaishaji vimo ndani ya vyama vyote vya siasa, kama ulivyo ndani ya shughuli nyingine nyingi za kitaifa: biashara, michezo, mapenzi, hata imani za kiroho. Kwa hiyo ninapozungumzia utapeli wa kisiasa nisije nikaeleweka kwamba nataka kukisema chama tawala pekee.

Hata vyama vya upinzani vinao matapeli wengi tu, na baadhi yao ni hao popo wanaohama kila uchao, leo wapinzani wakali wanaokitukana chama tawala kama samaki waliooza, kesho ndio hao hao “wanaorejea” chama tawala (hata kama hawakutoka huko awali) na kupokelewa kwa nderemo na kuwa “makada waandamizi” wa chama hicho wanaogeuzia matusi yao upande ule ule walikokuwa wakitambia jana. Na wala hawaoni haya.

Hapana, matapeli wako kote katika vyama vyetu. Lakini chama tawala hakina budi kukubali kubeba jukumu zito zaidi kuliko vyama vingine; hivyo iwapo katika maandishi yangu haya nitakitaja mara nyingi ieleweke kwamba CCM ndiyo chama kikongwe kuliko vyote na ndicho kilichotafuta na kufanikiwa kupewa dhamana ya kuliongoza Taifa hili.

Aidha chama hicho kimejenga tabia ya kutamba kwa jeuri ya “chama tawala”, na kinayo haki ya kutamba, sawa sawa na baba alivyo na haki ya kutamba kwa kuwa mkuu wa familia. Pamoja na haki hiyo ya kutamba, chama hicho hakina budi kuelewa kwamba kina majukumu makubwa ya kulipa Taifa hili uongozi makini, sawa na baba alivyo na majukumu mazito ya kuiongoza familia yake na kukidhi mahitaji yake.

Iwapo baba atashinda klabuni akitambia ubaba wake, akasahau kushughulikia chakula, matibabu na elimu ya mkewe na wanawe, kuna siku atajikuta si mume wala baba tena, na familia yake inahudumiwa na mababa wengine, ambao anaweza baadaye akawaita “wafadhili”.

Si tofauti kwa chama kinachoshinda katika ulevi wa mikutano ya kujisifu na karamu za kusherehekea nini sijui, huku nchi inateketea kwa umasikini usioelezeka katikati ya utajiri mithili ya El Dorado, halafu nchi nzima inawekwa chini ya “ufadhili” wa mababa tusiowajua.

Mnamo mwaka 1993 nilijikuta katika kundi dogo lililokuwa likijadili masuala mbali mbali ya kisiasa na muasisi wa Chama Cha Mapinduzi, Mwalimu Julius Kambarage.

Siku moja Mwalimu alitusimulia yaliyomkuta miaka ya 1986 na 1987 alipokuwa katika zoezi aliloliita “Mradi wa Kuimarisha Chama,” baada ya kuwa amestaafu urais mwaka 1985.

Anasema baada ya kutembelea wilaya zote nchini na kukutana na viongozi wa ngazi zote za uongozi wa chama, na kuwaangalia vizuri wale viongozi, na kuwasikiliza wakitoa taarifa, wakijenga hoja au wakijibu maswali yake, anasema alifika mahali akajiuliza swali: “Hivi hawa, pamoja na mimi, tumo ndani ya chama kimoja?”

Hali aliyoiona Mwalimu haijabadilika isipokuwa kama ni kuwa mbovu zaidi.

No comments: