Friday, November 09, 2007




Wanafunzi 20 mbaroni kuvuja kwa mitihani.

Paul Sarwatt, Arusha
HabariLeo; Friday,November 09, 2007 @00:04

WANAFUNZI zaidi ya 20 kutoka shule tatu tofauti mkoani Arusha, wamekamatwa na polisi juzi kwa tuhuma za kukutwa na majibu ya Mtihani wa Taifa wa kidato cha pili.

Kukamatwa kwa wanafunzi hao, kunadhihirisha kukithiri uvujaji na wizi wa mitihani hiyo inayoendelea nchini kote ambako hata hivyo, tayari Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema inaendelea na uchunguzi wa hali hiyo.

Kuhusu tukio hilo la Arusha, habari zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali na kuthibitishwa na Polisi, zinaeleza kuwa watahiniwa waliokamatwa, wanatoka shule mbili zilizoko wilayani Arumeru na moja ya Arusha Mjini.

Miongoni mwa matukio hayo ni wanafunzi wanane wa Shule ya Sekondari Muungano, iliyopo Usa River wilayani Arumeru na Mwalimu wao (jina tunalo). Walikamatwa baada ya mwalimu huyo kukutwa katika moja ya madarasa ya shule hiyo akiwafundisha watahiniwa hao majibu ya mtihani wa baolojia.

Mwalimu huyo pamoja na wanafunzi walikamatwa na kufikishwa katika kituo cha Polisi cha Usa River kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Wanafunzi wengine 10 wa Shule ya Sekondari ya Oldadai, walikamatwa na msimamizi wakiwa na majibu ya mtihani huo wa baolojia katika chumba cha mitihani na wengine wanne walikamatwa chooni wakipeana majibu ya mtihani wa somo hilo.

“Baadhi ya watahiniwa wa kike walikuwa wamenakili majibu kwenye mapaja yao kwa kutumia kalamu na baada ya majibu hayo kuoanishwa yalikuwa sahihi na maswali ya mtihani wa somo hilo,” alieleza mmoja wa walimu wa shule hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Watahiniwa wengine waliokamatwa, ni wa Shule ya Sekondari ya Kimandolu katika Manispaa ya Arusha ambao walifikishwa kituo kikuu cha Polisi cha Arusha juzi na waliachiwa jana asubuhi kwa dhamana.

Maofisa wa Elimu Kanda ya Kaskazini ambao mitihani hiyo ya kidato cha pili iko chini ya ofisi yao, jana walithibitisha kuvuja kwa mitihani hiyo lakini walikataa kutoa ufafanuzi wakisema kuwa msemaji wa suala hilo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu.

“Ni kweli kuna wanafunzi wamekamatwa na mitihani lakini sisi hapa tunaandaa taarifa na Katibu Mkuu ndiye mwenye jukumu la kuitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari,” alisema moja wa maofisa hao.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Wenceslaus Magoha alithibitisha kutokea kwa tukio na kueleza kuwa polisi bado walikuwa wanakusanya taarifa zaidi za upelelezi kuhusu watuhumiwa hao.

“Hivyo niko wilayani Ngorongoro katika operesheni maalumu lakini nikirudi mjini nitatoa taarifa zaidi juu ya suala hilo,” alisema Magoha kwa njia ya simu.

Akizungumza na HabariLeo kwa simu jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza alisema wizara yake inaendelea na uchunguzi wa kina. Alisema watakaobainika kuhusika, watapelekwa kwenye vyombo vya sheria.

Mahiza alisema wizara yake iko makini katika kulishughulikia suala hilo kuhakikisha kwanza kama mitihani iliyovuja ni mitihani ya kitaifa kweli au ni wajanja wachache tu wamejifanya kutunga mitihani ya namna hiyo.

“Ikibainika ni kweli mitihani hiyo imevuja na wahusika wakatambuliwa hatua zitachukuliwa. Lakini kwa kweli tunatumia busara kubwa katika kulishughulikia suala hilo,” alisema Mahiza.

No comments: