Thursday, November 22, 2007

RAI YA JENERALI ULIMWENGU


Ngoma inapotawaliwa na harufu mbaya.

NAPENDA kukiri kwamba tunapotumia muda mwingi na nishati kubwa ya akili kujadili matatizo yanayotokana na uongozi unaopatikana kwa njia ya kununua kura na njia nyingine haramu, tunabadhiri muda na nishati ambavyo vingetumika kujadili maana halisi ya uongozi bora.

Ni sawa sawa na kutumia muda na nishati kuzungumzia matatizo ya gari ambalo injini yake ‘imenoki’ wakati ambapo tungekuwa tunazungumzia modeli mpya za magari, sifa zake barabarani, kasi yake, utumiaji wa mafuta, n.k.

Lakini, kwa sababu gari letu ndilo hilo hilo, na injini yake ‘imenoki’na inavyoelekea hatujapata mtaji wa kununua gari jipya, inatubidi tujadili ni jinsi gani tunavyoweza kuikarabati injini yetu mbovu hadi hapo tutakapopata mtaji wa kununulia gari jipya.

Aidha, ni sawa na kutumia muda na nishati kuzungumzia shamba lililoharibika mno kutokana na mmomonyoko wa udongo, tukiwa na shauku ya kulitia mboji ili kulirejeshea siha yake ya awali, kwa sababu hilo ndilo shamba letu kwa sasa, na wala hatuna uwezo wa kuhama na kwenda kulima kwingine.

Endapo tutapata uwezo wa kununua shamba lililo bora tutafanya hivyo, lakini kwa sasa hatuna budi kulitibu hili tulilo nalo kwa kutia mbolea, kujenga matuta ya kuzuia mmomonyoko na kuepuka kuingiza ndani ya ardhi yetu kemikali mbaya zitakazoongeza uharibifu.

Ninayosema hapa yanahusu siyo tu chama-tawala bali pia Taifa letu. Kuhusu chamatawala, kama nilivyokwisha kusema, hiki ndicho chama kinachotawala nchi hii kwa sasa, kutokana na ridhaa ya raia waliopiga kura na kukiweka madarakani.

Haitoshi, ndicho chama kilichoiongoza au kuitawala (wakati mwingine kuna utata kati ya maneno haya mawili) nchi hii tangu kabla ya Uhuru, kwa maana ya TANU na Afro Shirazi.

Aidha, inawezekana kwamba injini hii inayoonekana kama ‘imenoki’ ikakarabatiwa na ikaweza kulikokota gari kwa kipindi kingine kirefu au kifupi.

Kwa hiyo hiki ndicho chama kinachoangaliwa na watu wote kwa mema na mabaya; ndicho chama kitakachosifiwa iwapo mambo yatakwenda vizuri, na ndicho chama kitakacholaumiwa iwapo mambo yatakwenda kombo.

Kama vile ambavyo kinayo haki ya kutamba pale nchi inapokwenda sawa, hakiwezi kujivua lawama nchi inapokwenda mrama. Kuhusu Taifa, ni dhahiri kwangu kwamba uoza tunaoukemea ndani ya chamatawala ni wa Watanzania, tena kwa maana kadhaa.

Kwanza, hiki ndicho chama chenye wanachama mamilioni, kiasi kwamba wanachama wa vyama vingine vyote wangejumlishwa, bado idadi yao isingefikia idadi ya wanachama wa chama-tawala.

Pili, kwa kukaa madarakani kwa muda wote huu chama hicho kimetia muhuri wake katika hisia za Watanzania na utamaduni wao wa kisiasa, kiuchumi, kiutawala, n.k.

Tatu, kutokana na hayo mawili hapo juu, hata vyama vilivoasisiwa chini ya mfumo mpya wa ‘vyama vingi’ navyo haviwezi kuepuka kufuata mambo fulani fulani yanayotokana na mwenendo wa chama-tawala. Kimsingi, pia, viongozi wengi wa vyama hivi vipya wanatokana na chama-tawala.

Kumbe wangetokea wapi? Kwa maana hiyo, sote, wanachama na wasiokuwa wanachama tunayo haki ya kukichambua chama-tawala na kukikosoa pale inapobidi, kwa sababu Watanzania wote, kwa njia tofauti, ni wadau wa chamatawala, na, ama katika heri ama katika shari, mwenendo wake utatuathiri, tupende tusipende.

Ni bora pia tutambue kwamba tunapozungumzia uoza na ufisadi haiwezekani ukawa ni ubovu uliomo ndani ya chamatawala peke yake.

Ni tatizo la jamii iliyo pana. Kama ni ulaghai, utapeli, ukosefu wa uaminifu, rushwa, unafiki, ukatili na kadhalika, hizi ni sifa mbovu zilizoenea katika jamii. Ingeturahisishia fikra kama tungeweza kusema kwamba yote haya yameletwa na CCM, lakini tungekuwa tunajidanganya. Mmomonyoko wa maadili na kupotea kwa sifa njema za Taifa letu vimesababishwa na mambo mengi, na sote tunahusika, chama-tawala kikiwa na sehemu yake lakini na sisi sote tukichangia.

Kwa hiyo, sote tuna wajibu wa kujirekebisha, hata kama chama-tawala kinao wajibu mkubwa zaidi wa kujibadilisha na kuwa chama-kiongozi ili kituongoze katika juhudi zetu za kujirekebisha. Naamini, bado naamini, hili linawezekana, na kwamba si kila kitu kimepotea.

Nimeisikiliza kwa makini hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete katika mkutano mkuu uliopita, nami nakiri kwamba ilikuwa hotuba muhimu iliyogusa masuala makubwa ya chama na nchi.

Amekemea maovu ambayo tumekuwa tukiyalalamikia kwa muda mrefu bila kusikia mwangwi wa malalamiko yetu kutoka kwa ‘ viongozi’.

Kama tulikuwa na ‘bahati’ ya kusikia cho chote kutoka kwa wakubwa ilikuwa ni sauti za kutubeza na kutukejeli na kutudharau.

Sasa mkuu wa wakuu mwenyewe katusemea. Kasema kwamba atayashughulikia malalamiko yetu. Sasa tunapata faraja kwamba wa kutubeza watakuwa wachache kwa sababu wakitubeza tena watakuwa wanambeza mwenyekiti wao. Lakini nasi tusichoke kumsaidia kwa kukemea vitendo viovu kila tunapovishuhudia.

Kazi hiyo hatuna budi kuifanya kwa sababu inahusu mustakabali wa Taifa hili na hatari zinazouchungulia. Tukizembea, tukisita, tukichelea, tukiogopa, tujue tumetega bomu ambalo lazima siku moja litalipuka, na isitoshe linaweza likatunusuru sisi mafisadi waasisi, lakini likawalipukia wanetu ambao katika unafiki wetu, au ufinyu wa fikra, tunajifanya tunawapenda mno.

Huwezi kumpenda mwanao na kisha ukamwacha nyumbani ukiwa umemtegea bomu, nawe ukayoyoma.

Napenda sana kurejea mafundisho ya Uislamu kuhusu ‘munkari’, au tendo ovu tunalolishuhudia . Tunafundishwa kwamba tunapoona tendo kama hilo hatuna budi, kama tunaweza, kulikomesha mara moja kwa mikono yetu.

La hatuwezi, basi tulikemee kwa sauti ya kusikika. Na kama hata hilo hatuwezi, basi tunune, ili anayelitenda ajue kwamba hatujalifurahia.

Matendo ninayoyajadili katika maandiko haya ni ‘munkari’ wa aina mbaya kabisa, na tusipoyakomesha au kuyakemea au kuyanunia yatatufikisha pabaya.

Nasema tena, naamini kwamba tunaweza kuyakomesha. Majuzi nimemsikia kijana mmoja aliyepewa nafasi ya juu katika chama-tawala akitamba kwamba katika uchaguzi uliopita hakutoa hata senti moja kununua kura.

Hizo ni tambo za kutia moyo, nami nampongeza kwa dhati kwa tambo hizo. Kinachotakiwa ni kwa wote kutamba kama kijana huyo, ila tu waseme ukweli, kwani tumewahi kuwasikia mafisadi wakubwa wakilaani ufisadi.

Tambo za kijana huyo zimenikumbusha ukweli kwamba huko nyuma mchakato wa chama-tawala haukuwa na vituko tunavyovishuhudia leo. Wagombea walifanya kampeni kali za kujitambulisha na kubainisha mchango wao katika chama na, kwa msingi huo, wakaomba kura kwa njia za kiungwana kabisa.

Kweli, walikuwapo wachache walioona kwamba matumizi ya fedha yaliwapa njia ya mkato kuwashinda waagombea wasiokuwa na ‘kitu kidogo’, lakini walikuwa wachache mno kiasi kwamba hawakuhatarisha uhai wa chama, na mara nyingi walidharauliwa na kunyimwa kura.

Sasa hivi, yale mambo yaliyodharauliwa wakati ule ndiyo yamekuwa msingi wa falsafa ya ugombeaji wa nafasi za uongozi, na wanaodharauliwa ni wale wasiocheza mchezo wa kusambaza fedha, kuranda mikoani wakikusanya wajumbe na kuwaweka kikao, kuwapa fedha na kuwalisha na kuwanywesha.

Mfano wake ni kama vile katika ngoma yo yote hutokea ushuzi ukamtoroka mmoja wa wachezaji, na kero yake ikawasumbua kidogo wenzake wanaopata harufu yake.

Inapotokea kwamba uwanja mzima inapochezwa ngoma ukajaa mashuzi, halafu ngoma ikawa inasikika kwa mbali, hiyo inakuwa si ngoma tena bali ni mchezo wa kuchafua hewa.

Ikifikia hali hiyo uwanja huo hautaweza tena kuwavutia wachezaji mahiri na watazamaji makini, bali utawavuta mabingwa wa mashuzi waliokula maharagwe yaliyooza.

Hasara zitokanazo na mchezo kama huo ni nyingi, lakini mojawapo kubwa ni kuwafanya watu wanaojiheshimu kukaa mbali na shughuli ya ya aina hiyo. Pia mchezo huo unawaengua wale wote wasio na uwezo wa kifedha.

Ni aina nyingine ya ubaguzi ambao hatimaye utawaruhusu wachache tu ndio waweze kushindana.

Na tukumbuke kwamba hii haitokei ndani ya chama-tawala tu bali katika vyama vingine vyote na katika mchakato wa kupata viongozi wa kitaifa kama vile madiwani, wabunge na rais.

Kwa njia hii hatuwezi kupata uongozi wa maana hata tungedhikiri usiku kucha.

Itaendelea.


No comments: