Thursday, November 22, 2007

Zitto: Watu wanacheza.

Aristariko Konga.

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini kupitia kofia ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amesema kuteuliwa kwake na Rais kuwa mjumbe wa Kamati ya Kuchunguza Mikataba ya Madini kamwe hakutamfunga mdomo kama ambavyo wengi wamekuwa wakicheza na uteuzi wake.

Katika mahojiano maalum na RAIA MWEMA mwishoni mwa wiki iliyopita, Zitto alifafanua masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuuhakikishia umma kuwa hawezi kufunga kinywa chake kutokana na uteuzi huo wa mkuu wa nchi, kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.

“Ninaweza kudiriki kusema kwamba nipo comfortable na uteuzi wa Rais. Sidhani kama imekuwa ni njia ya kuninyamazisha. Siamini hivyo. Nadhani watu wanacheza tu na suala hili muhimu kwa taifa. “Inawezekana kuna wana CCM ambao wanadhani uteuzi wangu ni njia ya kuninyamazisha. Kamwe siwezi kunyamaza. Hao wajue kuwa na wazo hilo ni kuchezea tu maslahi ya nchi.

“Kama kuna watu wanadhani kuwa kamati hiyo ni mtego wa kisiasa, bado wako wrong (wamekosea)…Kama wanadhani kuwa uamuzi wa Rais kuniteua mimi ni njia ya kuninyamazisha, basi wamekosea. Sitanyamaza kamwe. Hao wanacheza tu.

“Inabidi watu wafahamu kuwa suala la uchunguzi wa mikataba ya madini ni la maslahi ya taifa. Sijui kama ni la kisiasa. Ni suala la ulinzi wa maslahi ya taifa letu,” anasema Zitto.

Zitto anasema kwamba suala hilo si la ushindani wa CCM na CHADEMA, ingawa amesikia baadhi ya watu wengine wakisema kwamba baadhi ya wajumbe wa kamati hii ni marafiki wa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ambaye alishiriki kutia saini Mkataba wa Buzwagi, ambao ndio ulioibua mjadala katika Bunge, na kupelekea Zitto kusimamishwa ubunge hadi Januari, mwakani.

“Kuna masuala kwamba baadhi ya wajumbge wa kamati ni marafiki wa Karamagi, ni wanasiasa…Lakini mimi ninaamini kuwa CHADEMA ipo juu ya siasa, inaangalia zaidi maslahi ya taifa hili.

“Nikiwa mjumbe wa kamati hii nina uhakika nitakuwa huru kutoa maoni yangu. Nimekuwa uhuru kutoa maoni yangu ndani ya Bunge na ndivyo nitakavyokuwa huru kutoa maoni yangu kwenye kamati hii ya madini,” anasema.

Zitto anasema kwamba amekuwa akiungwa mkono na viongozi wa chama chake, akiwamo muasisi wa CHADEMA na mwanasiasa wa siku nyingi, Mzee Edwin Mtei, wananchi na viongozi wa Kigoma, ingawa hana uhakika na msimamo wa mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Bob Makani.

Hata hivyo, anasema kwamba chama chake bado hakijatoa kauli rasmi, kupitia vikao vyake, kuhusu uteuzi wake huo, licha ya kuwapo kwa kauli za kuungwa mkono kutoka kwa baadhi ya viongozi wake.

Zitto anasema kwamba kabla ya uteuzi huo wa Rais Kikwete, hakuwa na mawasiliano yoyote naye na wala hakuarifiwa mapema, kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakisema.

Anasema: “Mimi sijazungumza lolote na Rais Kikwete na sitaki kujiingiza kuwa nilishaurika kuwa mjumbe wa kamati hiyo. Sitaki kulifanya suala hilo kuwa ni la kisiasa.” Mpaka sasa ni Zitto Zuberi Kabwe ni mbunge kivuli wa uchumi kupitia chama chake.

Toka Raia Mwema.

No comments: