Friday, November 30, 2007

Tanzania hainufaiki na madini - Mnorwejiani








Yohanes Mbelege na Flora Temba, Moshi

TANZANIA imekuwa ikipata faida kidogo kutokana na madini ikilinganishwa na nchi zingine zenye madini, imeelezwa.

Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Mwakilishi wa Shirika lisilo la kiserikali la Norwei la Norwegian Church Aid, Bw. Fredrick Glad-Gjernes, wakati akitoa salamu kwenye mkutano wa wachungaji na wajumbe wa Bodi za SACCOS zilizo chini ya Benki ya Uchumi inayomilikiwa na Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania (KKKT).

Alisema kimsingi si Tanzania pekee yenye tatizo hilo, kwani Afrika imekuwa ikifadhili mataifa tajiri, ambayo yamekuwa yakichukua raslimali nyingi kutoka Afrika.

Bw. Glad-Gjernes alisema ipo haja kwa mataifa ya Afrika kuweka juhudi za pamoja kwa ajili ya kufanya mapinduzi ya kiuchumi, ambapo alimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuwa alikuwa akihubiri mapinduzi hayo.

Akizungumzia uhusiano wa kibiashara, Bw.Glad-Gjernes, alisema kutokana na bidhaa za nchi za nje kuwekewa ruzuku na mataifa hayo, bidhaa za Tanzania zimekuwa haziwezi kushindana nazo.

Aidha, alisema wakulima wa mazao mbalimbali wamekuwa hawanufaiki na kilimo na akatolea mfano wa kahawa, kuwa wakulima huambulia asilimia mbili tu ya bei ya madukani Ulaya.

Katika hatua nyingine, mwakilishi huyo alipigwa na butwaa kuona maduka makubwa nchini, yakiuza matunda ya nje na kuwataka Watanzania kujenga tabia ya kupenda bidhaa zao.

“Nilikuwa na mke wangu natafuta juisi Dar es Salaam, nikawa kila nikipita nakuta juisi imetengenezwa kwa matunda ya Ulaya au maziwa yametoka nchi za nje, huku vitu hivyo vikioza Tanzania kwa kukosa soko!,” alisisitiza Bw. Glad-Gjernes.

Alisema tatizo kubwa ni uhusiano wenye mifumo ya kiunyonyaji katika sekta za biashara na uwekezaji, zilizopo baina ya Tanzania na mataifa makubwa.

Aliongeza kuwa hali hiyo ikiachwa ilivyo, itaifanya Tanzania iendelee daima kuwa maskini.

Alisema uhusiano wa aina hiyo umekuwapo kwa muda mrefu, huku matajiri kutoka mataifa makubwa yakijitajirisha kutokana na raslimali za Tanzania.

“Hii ni changamoto kwa Kanisa, kwani bila hivyo Watanzania wataendelea kubaki maskini, iwapo hakutakuwa na nguvu ya pamoja kukomesha uhusiano ya aina hiyo,” alisema.

No comments: