Friday, November 30, 2007

Dk. Rashidi, Kazaura hawaivi

Mmoja alipokonywa gari na ofisi.

KUJIUZULU Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Dk. Idris Rashidi, pamoja na mambo mengine, kunaelezwa kutokana na msuguano wa muda mrefu kati yake na Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Fulgence Kazaura.


MKURUGENZI Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idris Rashidi

Habari zinasema katika moja ya misuguano hiyo, mara baada ya kuingia Tanesco, Dk. Rashidi alifanya mabadiliko kadhaa yaliyolenga kupunguza matumizi na uboresha huduma kwa wateja, uamuzi ambao ulimgharimu Balozi Kazaura, aliyepunguziwa baadhi ya huduma.

Kazaura alikua na ofisi katika majengo ya Tanesco barabara ya Samora yalipokua makao makuu ya shirika hilo, ofisi ambazo sasa zinatumiwa na Meneja shirika hilo Mkoa wa Ilala.

“Mkurugenzi aliamua ofisi aliyokua akiitumia Mwenyekiti wa Bodi itumiwe na Meneja Mkoa wa Ilala, na gari alilokua akitumia nalo lifanye kazi nyingine za kiutendaji na Mwenyekiti apatiwe huduma hizo wakati wa vikao husika pekee,” kinasema chanzo chetu cha habari ndani ya Tanesco.

Kwa mujibu wa habari hizo, Balozi Kazaura alikuwa pia na Katibu Muhtasi, aliyetajwa kwa jina la Rukia Wandwi, ambaye alikua katika ofisi hiyo iliyokabidhiwa Tanesco Mkoa wa Ilala.

Kwa mujibu wa habari hizo, hatua hiyo haikumfurahisha Balozi Kazaura na baadhi ya watumishi ambao baadhi walisema pamoja na kuwa utaratibu hauruhusu Mwenyekiti kuwa na ofisi inayohudumiwa wakati wote na shirika, ilipaswa “busara na diplomasia itumike kumnyang’anya ofisi Mwenyekiti.”

“Unajua kwanza bodi yenyewe ndiyo inamaliza muda wake kwa hiyo ingekuwa busara kumwacha amalize muda wake ndipo uwekwe utaratibu mwenyekiti mpya anapokuja asiwe na ofisi badala ya kumuondoa na kumdhalilisha mzee wa watu,” anaeleza mfanyakazi mwingine wa Tanesco anayelifahamu sakata hilo vizuri.


Balozi Fulgence Kazaura

Habari zaidi zinaeleza kwamba tofauti kati ya Dk. Rashidi na Mwenyekiti wake zilianza wakati Balozi Kazaura akiwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, yeye (Dk. Rashidi) akiwa Gavana wa Benki Kuu (BoT).

“Hawa watu hawakuwa na mawasiliano mazuri tokea wakiwa serikalini, Kazaura akiwa Wizara ya Fedha na Dk. Rashidi akiwa BoT, lakini sina hakika walitofautiana kwa jambo gani. Kila mmoja ni mtu mwenye kujiamini,” anasema mtumishi mmoja mstaafu wa Serikali.

Balozi Kazaura alipoulizwa na Raia Mwema kuhusu kuondolewa baadhi ya huduma, alijibu, “huo ni uongo,” na kukata simu yake ya mkononi ambayo baadaye ilipokewa na mtu mwingine aliyedai kwamba “mzee ametoka, sijui amekwenda wapi.”

Kwa upande wake, Dk. Rashidi alisema yuko katika kikao na hivyo hawezi kuzungumza jambo lolote na hadi tunakwenda mitamboni hakuweza kupatikana kuzungumzia mahusiano yake na Mwenyekiti wa Bodi.

Awali ilielezwa kwamba bodi nzima ya Tanesco imegawanyika katika makundi mawili - moja likimuunga mkono Mwenyekiti na jingine Mkurugenzi huku wengine wote wakionyesha kutofurahia msuguano kati ya viongozi hao wawili.

Balozi Kazaura amenukuliwa na mtoa habari wetu akisema kwamba Dk. Rashidi anawajibika kwa Bodi kwa mujibu wa sheria ya kuundwa kwa Tanesco na si Rais kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakimtaka (Mwenyekiti) amheshimu kwa kuwa ni mteule wa Rais.

Tukio la hivi karibuni la Tanesco kukata umeme wa kiwanda cha Saruji cha Tanga, lilielezwa kutonesha kidonda cha msuguano wa muda mrefu kati ya Dk. Rashidi na Mwenyekiti wake, ambaye anaelezwa kupewa maelekezo ya kuhakikisha umeme unarudi.

Haijafahamika mara moja ni nani aliyemuagiza Mwenyekiti ahakikishe umeme unarudi, japo kuna taarifa kuwa amri hiyo inaweza kuwa imetoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ambaye hata hivyo amekwisha kukanusha kuhusika katika suala hilo.

Kiwanda hicho cha Saruji cha Tanga ambacho hutumia umeme wa zaidi ya milioni 400/- kwa mwezi, kilikatiwa umeme kikidaiwa milioni 49/- ambazo zilitokana na madai ya ‘kuchezea’ mita ya Tanesco.

Kujiuzulu kwa Dk. Rashidi kulikotokana kwa kiasi na msuguano huo wa umeme wa kiwanda hicho, na hatimaye, kubadili kwake uamuzi na kuifuta barua yake ya kujiuzulu, kumezua maswali mengi katika kipindi hiki ambacho shirika analoliongoza limo katika hali mbaya ya kifedha kutokana na matumizi kuwa makubwa kuliko mapato.

Wako wanaodai kwamba Rais Jakaya Kikwete, ndiye aliyemuomba Dk. Rashidi kubadili uamuzi wake wa kujiuzulu, huku baadhi wakidai kwamba aliombwa na Waziri Karamagi.

Lakini jambo lililo dhahiri ni kwamba aliombwa kubadili uamuzi wake huo. Habari za ndani zaidi zinaeleza kwamba mbali ya kuombwa kubadili uamuzi wake huo, Dk. Rashidi sasa amepewa uwezo zaidi wa kufanya maamuzi mazito zaidi ndani ya shirika hilo ili aweze kulikwamua kiuchumi.

Tayari shirika hilo limekwisha kuomba idhini ya kupandisha bei ya umeme ili kufidia sehemu ya gharama za umeme wakati shirika hilo limetakiwa kujiendesha kibiashara.

Dk. Rashidi anaelezwa kupelekwa Tanesco ili kulikwamua shirika hilo katika matatizo ya kifedha kutokana na uzoefu wake katika masuala ya fedha na uchumi, lakini wachunguzi wa mambo wanasema hawezi kufanikiwa hadi Serikali ilisaidie kwa kulipa fedha za kulipa madeni na kuepuka mikataba mibovu.

Tanesco inaelezwa kuwa katika hali ngumu kutokana na kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato lakini zaidi kutokana na kuelemewa na mikataba kadhaa mibovu inayowalazimu kulipa sehemu kubwa ya mapato yake.

Shirika hilo hivi sasa linalazimika kulipa mamilioni ya shilingi kwa mradi wa umeme wa gesi wa Independent Power Limited (IPTL) huku ikiwa na mikataba mingine inayoashiria hatari zaidi kama ule wa Kiwira Coal Power na ule wa Richmond Development ambao Bunge limeunda Kamati ya kuuchunguza.

Shirika hilo linaelezwa kupoteza shilingi bilioni 6.4/- kwa mwezi kutokana na kushindwa kupandisha bei ya umeme kama lilivyoomba.

Taarifa za Tanesco zinaeleza kwamba shirika hilo ni lazima lipandishe bei ya umeme kwa asilimia arobaini (40%) maombi ambayo yamewasilishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Shirika hilo kwa sasa linatoza wateja wake Shilingi 84/- kwa uniti moja wakati gharama za uzalishaji ni shilingi 183/- kwa uniti moja na hivyo kulifanya shirika hilo kupoteza shilingi 99 kwa kila uniti inayotumika.

Dk. Rashidi aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco mwishoni mwa mwaka jana kuchukua nafasi ya menejimenti ya Net Group Solutions kutoka Afrika Kusini iliyohitimisha mkataba wake wa miaka minne Desemba 31 mwaka jana.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Rashidi alikuwa Ofisa Mwendeshaji Mkuu na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Rabobank Holland inayosimamia shughuli za benki ya National Microfinance (NMB) tangu Oktoba mwaka juzi.

Mbali ya kuwa Gavana wa BoT, Dk. Rashidi aliwahi pia kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC kati ya mwaka 1992 hadi Juni mwaka 1993 na Mkurugenzi wa Benki ya Akiba Commercial (ACB) tangu mwaka 1999 hadi Machi 2000.

Kutoka Raia Mwema wiki hii.

No comments: