Thursday, November 29, 2007

TRA yanasa meli ikishusha magendo


Hassan Simba, Mtwara
HabariLeo; Thursday,November 29, 2007 @00:03

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) inaishikilia meli ya Mizigo ya Mv. Ariyana iliyokuwa ikisafiri kutoka Zanzibar kwenda Msumbiji baada ya kutia nanga kinyemela katika bandari ndogo ya Verani karibu na hapa kwa lengo la kuteremsha mizigo kinyume cha taratibu.

Kukamatwa kwa meli hiyo kulitokana na taarifa ya wananchi kwa TRA.

Meneja wa TRA mkoani, Laurent Paul, alisema jana kwamba meli hiyo ilikamatwa Jumatatu saa 11 jioni.

Alisema baada ya upekuzi nyaraka zilibainisha kuwa Meli hiyo yenye uwezo wa kubeba tani 80 haikupaswa kutia nanga katika bandari yoyote nchini isipokuwa Msumbiji ambako ilikuwa inakwenda na kwamba kitendo cha kuiegesha katika bandari ya Mtwara ni kinyume cha maelekezo ya nyaraka hizo.

Paul alibanisha kuwa nyaraka hizo zinatambua kuwapo kwa Betri aina ya dry cell katoni 1,200 na mchele magunia 1,500 yenye ujazo wa kilo 50.

Hata hivyo baada ya upekuzi baiskeli 80, ngano na mafuta ya kula na seti kadhaa za luninga ambazo idadi wala thamani yake havijajulika vilikutwa ndani ya meli hiyo bila hadidu za rejea.

Alisema maofisa wake kuanzia Jumanne hadi sasa wanashughulikia taratibu za kushusha mzingo huo ili waweze kufahamu idadi na thamani yake na sababu ambazo zilisababisha kupindishwa kwa safari hiyo.

“Kuna kila dalili za watu hao kula njama za kukwepa kulipa ushuru…..iwapo hilo tutalibaini wahusika watalipa ushuru na hatua zingine za kisheria zitafuatwa…hatujui kwa nini waliamua kupindisha safari….lakini kingine cha kushangaza ni kuona mzingo mwingi hauna nyaraka za kusafirishia,” alisema Paul.

No comments: