Lula wa Ndali-Mwananzela
WAHENGA walisema kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi, na ndiyo wao pia waliosema kuvunjika kwa mpini siyo mwisho wa kilimo.
Misemo hiyo na mingine inayofanana nayo, ina maana moja kubwa kwamba kitu kikienda kombo au kisipofanya kazi inavyotakiwa basi isiwe mwisho wa kile kinachotakiwa kufanywa kufanyika. Nikichukua misemo hiyo na kuipanua kidogo naweza kusema kuwa kujiuzulu kwa kiongozi si mwisho wa kuongoza.
Wiki iliyopita ilikuwa ni almanusra Watanzania tushuhudie kujiuzulu kwa mmoja wa watendaji wa makampuni nyeti nchini, lakini kwa sababu ambazo bila ya shaka zinajulikana zaidi sasa baada ya kujiuzulu huko kukomeshwa saa chache baada ya habari zake kuvuja.
Habari za kujiuzulu Dk. Idris Rashid, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Umeme nchini (Tanesco) ziliposikika mwitikio wa watu wengi ulikuwa si tu wa kushangazwa bali kwa namna fulani wa kuona kuwa hatimaye kuna mtu ameamua kuwajibika.
Hata hivyo, saa chache baadaye habari mpya zikatokea kuwa Dk. Idris ameondoa barua yake ya kujiuzulu (mwenyewe anasema alishauriwa kufikiri upya) na hivyo anaendelea na wadhifa wake. Ni tukio hilo ndilo leo limenifanya nizungumzie kidogo suala hili la viongozi na watendaji wetu kujiuzulu.
Katika historia ya nchi yetu, mara kadhaa baadhi ya viongozi walijikuta wanalazimika kujiuzulu kwa sababu moja au nyingine. Mwalimu Julius Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu ili aijenge TANU, akamuachia Rashidi Kawawa kabla ya kurudi baadaye kama rais; Ali Hassan Mwinyi alijiuzulu uwaziri nafasi yake ya uwaziri wa mambo ya ndani kwa mauaji yaliyotokea Shinyanga; Profesa Simon Mbilinyi na Idi Simba walilazimika kujiuzulu baada ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa ichunguze misamaha ya kodi ya sukari; na Aboud Jumbe alilazimika (lazimishwa) kujiuzulu kwa kile ambacho kinajulikana kwenye kumbi za wanasiasa kama “kuchafuka kwa siasa za Zanzibar”.
Hata hivyo, tukio la “almanusra” la Dk. Idris limetuonesha jambo moja dhahiri; ni vigumu sana kwa viongozi wetu kujiuzulu hasa pale ambapo kujiuzulu huko kunatishia maslahi ya kisiasa ya walio madarakani au watu wenye maslahi katika nafasi za watu wanaotaka kujiuzulu.
Lengo langu leo ni kutaka kuonyesha kuwa kwanza, kiongozi kujiuzulu si mwisho wa uwezo wake kuongoza; na pili sisi kama Taifa lazima tuanze kujenga utamaduni wa kujiuzulu pale inapopasa na tusijisikie vibaya kama alivyofanya Peter Machunde baada ya mgongano wa kimaslahi tulioonyesha wiki iliyopita kuwa dhahiri mno.
Kwa nini kuna wakati viongozi wanapaswa kujiuzulu? Tukio hili ambalo nusura litokee linatuongoza kufikiri juu ya swali hilo. Kuna wakati ambao viongozi wanapaswa kujiuzulu. Kwa kuangalia suala la Dk. Idris tunaweza kupata sababu mojawapo. Inapotokea kuwa mtumishi wa umma au hata kwenye sekta binafsi anayeamini kuwa ana uwezo wa kufanya kitu fulani au ana mamlaka fulani na anapojaribu kutumia uwezo au mamlaka hayo anakutana na vizingiti visivyo vya lazima basi mtu huyo anaweza kuchukua uamuzi wa kujiuzulu. Mara nyingi vizingiti hivyo vinatokea pale ambapo maslahi ya watu fulani yanatishiwa na maamuzi ya kiongozi hiyo na kwa vile watu hao wana uwezo au mamlaka ya juu zaidi basi wanaamua kuingilia kati uamuzi huo.
Kwa wale wanaoweza kukumbuka watakumbuka mwaka ule ambapo kiongozi mmoja alidiriki kukimbia usiku kwenda uwanja wa ndege ambako alienda kuthubutu kuwakamata watu waliodaiwa kuwa walikuwa wanatorosha dhahabu ya nchi yetu. Kiongozi huyo alipowakamata watu hao aligundua kuwa mmoja wao ni mke wa mkubwa mmoja wa nchi na alipotaka maelezo zaidi aliamuriwa awaachilie.
Suala kama hili linaweza na linapaswa kumfanya mtu ajiuzulu. Kama wewe ni kiongozi na wakati wa kutekeleza majukumu yako unakuta wakubwa wako wanakuingilia kazi ili usitekeleze majukumu yako au wakikutaka upinde au uvunje sheria basi wewe kama kiongozi unapaswa kujiuzulu nafasi hiyo. Vinginevyo, ni rahisi kujikuta unageuzwa kikaragosi cha “wakubwa” ambapo wanajua katika nafasi fulani wana “mtu wao”.
Wakati aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ukiwaona Ditopile wa Mzuzuri alipojikuta ana kesi nzito ya kujibu Rais Jakaya Kikwete angeweza kumuondoa mara moja au kumpa nafasi ajiuzulu nafasi hiyo. Rais aliamua kumpa muda wa kujiuzulu na Mzuzuri alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo ili mchakato wa kutafuta haki uanze na yeye asionekane kuwa ni kizuizi. Wakati Mawaziri Idi Simba na Juma Ngasongwa walipoamua kujiuzulu, sababu kubwa ni kuwa walijikuta kwenye mazingira ambayo wasingeweza kuendelea kushikilia nafasi zao mbele ya msukumo mkubwa uliokuwapo bungeni.
Mara nyingi tumekuwa na watu ambao wamekuwa waking’ang’ania nafasi zao huku wakijua (na watu wengine bila ya shaka) kuwa hawana uwezo wa kuendelea na nafasi hizo hasa kutokana na kuboronga kwao ambako kuko dhahiri. Kwa vile hatuna utamaduni wa watendaji kujiuzulu basi tunajikuta tunaendelea na watu walioishiwa ubunifu wa uongozi na ambao taa yao ya kuongoza imekwisha fifia. Watu hao wangeweza kuliepushia Taifa mambo mengi kama wangeamua kujiuzulu.
Wakati mwingine viongozi wanaamua kujiuzulu ili kuonyesha kuwajibika kwa yale yaliyotokea chini ya uongozi wao.Wakati mauaji wa Shinyanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo ilimbidi ajiuzulu nafasi hiyo.Waziri huyo alionyesha kuwa alikuwa tayari kuwajibika kwa vitendo vilivyotokea yeye akiwa waziri wa idara husika ya Polisi. Miaka michache baadaye waziri huyo alijikuta akidhaminiwa jukumu kubwa zaidi la kuwa Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano akimpokea baba wa Taifa.
Kitendo cha Mzee Mwinyi kuamua kuwajibika si tu kilimjengea heshima bali pia kilionyesha kuwa yeye ni mtu wa namna gani. Leo hii ukiangalia watawala wetu kuwajibika inakuwa ni mbinde. Leo hii ni vigumu wakati mwingine kufahamu kama kuna kiongozi yeyote ambaye anaweza kuwajibika kwa matendo yaliyotokea chini ya uongozi wake.
Baada ya Tanesco kuamua kupandisha bei ya umeme na wakati huo huo kujaribu kuwadai shirika la Saruji Tanga na kukutana na ugumu wa kukusanya deni hilo, Dk. Idris alijikuta hana jinsi isipokuwa kuamua kubwaga manyanga. Japo kuwa jaribio hilo halikufanikiwa, ukweli unabakia kuwa Dk. Idris nusura awajibike kutokana na yale yaliyotokea chini ya uongozi wake.
Sababu nyingine ambayo inaweza kumfanya kiongozi ajiuzulu ni ukweli kuwa kujiuzulu ndiyo njia ya kiungwana kabisa ya kiongozi kutoka madarakani kabla ya wakati wake na bila ya kusubiri kufukuzwa. Baadhi ya watu wanaona kuwa kujiuzulu ni suala la aibu au fedheha.
Aliyekuwa Rais wa Marekani mwaka 1973 Richard Nixon alijikuta hana ujanja isipokuwa kujiuzulu wadhifa huo baada ya Kashfa ya Watergate. Uzito wa kashfa hiyo ulifikia mahali ambapo Bunge la Marekani lilikuwa tayari kuchukua hatua za kibunge za kumuondoa Rais na akiwa amepoteza imani ya wananchi na zaidi watu wa chama chake, alilazimika kujiuzulu badala ya kusubiri Bunge limuondoe kwa fedheha. Kwa taifa letu tutajitendea hisani kubwa endapo viongozi watatambua kuwa hakuna haja ya kung’ang’ania mfupa uliomshinda fisi au wanapojua ya kuwa aibu inawangojea.
La msingi kutambua ni kuwa hata kama mtu ataondoka kwenye uongozi kwa kujiuzulu haina maana kuwa huo ni mwisho wa mtu huyo isipokuwa kama amekata tamaa yeye mwenyewe. Kujiuzulu na kutoka madarakani haina maana kuwa wananchi au viongozi wa juu hawawezi tena kumtumia mtu yule. Kama nilivyoonesha hapo nyuma kuwa Mzee Mwinyi alipojiuzulu uwaziri haukuwa mwisho wa uongozi wake, Simba na Dk. Ngasongwa walipojiuzulu haina maana ulikuwa ndiyo mwisho wao. Ndipo hapo nilipotumia msemo kuwa kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi.
Sisi kama Taifa ni lazima tuanze kujenga utaratibu na utamaduni wa viongozi kujiuzulu na tuanze kukubali kuwa kujiuzulu kote si lazima kuambatane na aibu. Kama Dk. Idris angetekeleza tishio lake la kujiuzulu sidhani kama angegubikwa na aibu, bali angepokewa na makofi ya kishujaa. Ni wazi kuwa kama kuna kitu ambacho Serikali ya Rais Kikwete haiwezi kuhimili sasa hivi ni kujiuzulu kwa kiongozi yeyote wa juu kwa sababu ya kutokubaliana na maamuzi ya wakubwa wake.
Ni rahisi zaidi kwa kiongozi kujiuzulu kwa sababu ya uzembe au kushindwa lakini ni vigumu zaidi kujiuzulu kupinga maamuzi ya viongozi wa juu. Katika mfano wa Nixon, alipoona kuwa uchunguzi wa kipepelezi unamkaribia kumbamba, alimuamuru Mwanasheria wake Mkuu, Elliott Richardson na Msaidizi wake William Ruckelshaus kumfukuza Mwendesha Mashtaka Maalum Archibald Cox (ambaye alikuwa anachunguza utawala wa Nixon). Richardson na William wote walikataa kutii agizo hilo na wakaamua kujiuzulu nafasi zao kupinga kuingiliwa madarakani namna hiyo.
Tunapoamua kuiga mambo mengi (na mengine machafu) toka nchi za Magharibi kuna haja ya kuangalia yale mazuri yanayoimarisha demokrasia na yanayolinda utendaji kazi pia. Mojawapo ni hili la viongozi wetu (serikalini na katika sekta binafsi) kuweza kuachia ngazi pale maji yanapowazidi kimo au inapolazimika kufanya hivyo. Isionekane kuwa katika taifa hili kuna kikundi cha watu ambao wameng’ang’ania madaraka kama luba. Ndiyo maana inakuwa ni fedheha kubwa pale ambapo inamlazimu Rais kubadili baraza lake au hata kulivunja kabisa.
Viongozi wasisubiri kitendo hicho kikali cha Rais; kila kiongozi anajua utendaji wake na anajua kwa jinsi gani ameweza kumsaidia Rais Kikwete kutimiza Ilani na kukidhi matarajio ya Watanzania.Wapo wanaojua kabisa kuwa nafasi walizo nazo zimewashinda na ya kuwa licha ya jitihada zao kwa kweli wamekwama na wakati umefika kuwapisha Watanzania wengine.
Kwa maoni yangu ni kuwa badala ya kusubiri watimuliwe watajijengea heshima kama watajindoa kwa hiari yao kwani kwa kufanya hivyo haina maana wamefikia mwisho wa utumishi wao. Leo kina Ngasongwa na Simba si wapo na bado wana nafasi?
Viongozi wasiogope kujiuzulu na sisi wananchi wa kawaida tuondokane na dhana kuwa kujiuzulu ni kitendo cha aibu au fedheha. Lakini pia tunatambua kuwa wengine inabidi wajiuzulu ili kuepusha fedheha zaidi na aibu siku zijazo.
Kwa wote hawa swali kubwa wanalokabiliwa nalo ni kujiuzulu au kutojiuzulu? Dk. Idris alipata kigugumizi; wengine wanaogopa hata kufikiria uwezekano huo; hata hivyo, kama hawatajiuzulu wenyewe huku wakiendelea kusongwa na kashfa na matatizo na uzito wa kazi ukiwaelemea watajikuta wanarahisishiwa uamuzi huo pale viongozi wa juu yao wanapoamua kuwaondoa madarakani.
Ninafahamu mazoea yana tabu na wakati mwingine wamezoea kukaa katika madaraka yao kiasi cha kuamini kuwa bila wao mambo hayataenda au hakuna mtu mwingine wa kushika madaraka hayo. Ukweli ni kuwa wapo wananchi wengi na wenye uwezo wa kujaza nafasi yoyote katika Tanzania (ukiondoa zile za utaalam mahsusi) na hakuna mtu ambaye bila yeye Tanzania, idara, au chombo cha serikali hakitaenda.
Ni lazima tufikie mahali tukubali kuwa kama mtu kashindwa au mambo yanakuwa magumu, basi tumsaidie afikie uamuzi wa kujiuzulu badala ya kujaribu kumfanya ang’ang’anie ilimradi tu asiondoke kwa kujiuzulu. Wakati mwingine ndugu zangu, viongozi huwa wanajiuzulu na kujiuzulu kwao si mwisho wa wao kupata nafasi za kuongoza, kwani kuvunjika kwa ndoana, siyo mwisho wa uvuvi.
Niandikie: lulawanzela@yahoo.co.ukKutoka Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment