Sunday, November 25, 2007

WASIFU WA JUMAPILI

MAJUKUMU MA-3 MUHIMU ULIYONAYO KWA MPENZI WAKO!

Tunakutana tena mpenzi msomaji wangu kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima kabisa na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku. Mimi namshukuru Mungu kwani afya yangu ni bomba, kama kawaida naendelea kukuletea 'majamboz' yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Swali ambalo nalazimika kulifafanua zaidi ni lile la wale wenye hisia kwamba, wapenzi wao wanawasiliti.....


Hakika walio wengi kila wanapokuwa mbali na wapenzi wao hujihisi kusalitiwa, lakini sasa unachotakiwa kujiuliza ni kwamba, unaweza kumchunga mpenzi wako asiwe na uhusiano usiofaa na mtu mwingine zaidi yako kama akiamua? Hakika ni kitu kisichowezekana! Nasema haiwezekani kwa sababu kama mpenzi wako hajatulia, hajatulia tu na anaweza kila mara akawa anakueleza kwamba hawezi kukuumiza lakini huyo huyo siku moja akaja kukufanyia mambo ya ajabu.

Sasa ufanyeje basi ili uweze kuishi maisha ya amani? Kinachotakiwa kwa sisi tulio katika mapenzi ni kuwaamini wapenzi wetu kwa asilimia zote wala tusiwe na shaka pale wanapokuwa mbali na sisi.

Tuamini yale wanayotuambia na tusipende kuwafuatilia sana wapenzi wetu katika maisha yao labda itokee umepata tetesi kuwa laazizi wako anakuzunguka, hapo sasa fanya uchunguzi na muwekee mitego ili kumnasa.

Baada ya kugusia kidogo mada hiyo ya wiki iliyopita sasa nirudi katika mada yangu ya wiki hii. Nazungumzia kitu ambacho nimegundua watu wengi walio katika mapenzi hawakitambui.

Hiki si kingine bali ni majukumu uliyo nayo wewe ambaye umeamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu uliyempenda kwa dhati kabisa. Ukishindwa kuyatimiza majukumu hayo hesabu tu kwamba huwezi kudumu katika uhusiano kwani ni lazima mpenzi wako atakutosa.

Tufahamu tu kwamba, majukumu katika uhusiano wa kimapenzi yapo mengi lakini leo nitazungumzia matatu makubwa ambayo kila aliye katika mapenzi anatakiwa kuyatekeleza ipasavyo.

Kumridhisha kimapenzi:
Lengo la kila mtu kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mtu fulani ni kupata mapenzi ya kweli na mapenzi ya kweli hayo hayawezi kupatikana kama hutamridhisha mpenzi wako ipasavyo.

Ninaposema hivyo baadhi yenu hukimbilia moja kwa moja kwenye mambo ya sita kwa sita. Sawa hapo ndipo kwenye mzizi wa kipengele hiki. Kimsingi utakuwa ukijiweka katika mazingira magumu kama utashindwa kumpatiliza mpenzi wako katika mambo flani.

Unachotakiwa kufanya ni kuwa mtundu na mbinifu wa vitu ambavyo ukimuonjesha mpenzio hatafikiria kukuacha. Tatizo walio nalo wengi ni kutokuwa tayari kubadilika kwa kujifunza. Nimekuwa nikiandika mara kwa mara mambo ambayo unaweza kufanya ya kamdatisha mpenzi wako, lakini wengine bado wanakubali kuuacha uhusiano wao unadorora bila kuchukua hatua zozote.

Kumhudumia kwa hali na mali:
Kwa wapenzi walioshibana kisawasawa kusaidiana katika mambo flani flani ni jambo la kawaida. Tukisema huduma tunajumuisha vitu vingi na si kwa pande moja tu kama ilivyozoeleka kwamba mwanaume ndiye mwenye jukumu la kumhudumia mpenzi wake. Wanaofahamu hivyo watakuwa wanakosea kwani huduma hutolewa pande zote mbili japo zinakuwa katika viwango tofauti.

Niwakumbushe kuwa, tunaposema kumhudumia mpenzi wako kwa hali na mali ni kuhakikisha unamfanyia kila jambo ambalo ni muhimu katika maisha yake. Mfano hakikisha anakula vuzuri, anavaa smati, kumpeleka hospitali pale anapokuwa anaumwa, akiwa na shida msaidie. Kwa kufanya jambo hili hakika wapenzi mtakuwa mmehudumiana na mwisho wa siku kuliweka penzi lenu katika hali nzuri.

Usiishie hapo akiwa na shida ya pesa na akaomba msaidie, fanya kila uwezalo kuhakikisha unampatia. Kwa kufanya hivyo itadhihirisha kwamba unamdhamini na kumjali na hayo ndio mapenzi sasa.

Kumliwaza asipokuwa na raha:
Tulio wengi wapenzi wetu wanafanya kazi na wakati mwingine unaweza kumuona mpenzi wako amerudi kutoka kazini akiwa hana raha, hakika ni jukumu lako kuhakikisha unamfurahisha na kumuuliza ni kitu gani kilichomuweka katika hali ile.

Kama mpenzi wako ana upendo na wewe atakueleza sababu ya yeye kuwa katika hali hiyo na wewe kujua jinsi gani unaweza kumrudisha katika hali yake ya kawaida.

Lakini ikumbuke kwamba, hawezi kukwambia iwapo wewe utachukulia poa pale atakaporudi akiwa katika hali tofauti na siku zote. Mwanamke au mwanaume anayeweza kumpa raha mwenzake ni yule aliyechangamka na mcheshi hasa anapomuona mpenzi wake akiwa hayupo katika 'mudi'.

Sasa basi nawashauri wapendanao kuona umuhimu wa kuliwazana. Mnapokuwa katika wakati mgumu kimaisha mpe maneno ya faraja kama vile "pole na kazi mpenzi wangu mbona huna raha? Muulize ni nani kamkosea, wakati huo si kwa kumkaripia, tumia lugha laini ili hata kama alitaka kukuficha kilichomkasirisha akwambie.

Ni hayo tu kwa leo, tuonane tena wiki ijayo kwa makala nyingine ila kama una ushauri, maoni kuhusiana na jambo lolote la maisha ya kimapenzi.

Wasiliana nami kupitia namba 0784-600047 au
barua pepe: zekaima@yahoo com

Kutoka GlobalPublishers TZ


No comments: