Wednesday, December 26, 2007

Ballali aumiza vichwa.

HALI ya afya ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Ballali (65), taarifa za kujiuzulu kwake na nani atakayemrithi ni mambo yanayomgusa Rais Jakaya Kikwete, akiwa mapumzikoni kaskazini mwa Tanzania.

Bado hakuna taarifa rasmi hasa za kujiuzulu kwa Ballali, pamoja na kuwapo habari zenye uzito kuthibitisha taarifa hizo lakini yote hayo yanamfanya Rais Kikwete, aguswe zaidi na yanayomhusu Ballali, huku akitafakari ni nani hasa anayeweza kuchukua nafasi yake.

Kikwete amekwisha kuziba nafasi zote nyeti zilizokuwa zikishikiliwa na watu aliowarithi kutoka kwa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, isipokua BoT ambako Ballali ambaye aliongezewa muda wa miaka miwili mwaka 2003, amekaa kwa zaidi ya miaka 10.

Kwa mujibu wa sheria, gavana hukaa kwa vipindi vya miaka mitano na katika siku za karibuni ndani ya awamu moja ya utawala. Ballali amefanya kazi katika awamu mbili, ya Mkapa na hii ya Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kuadhimisha miaka miwili ya utawala wake, Jumatano iliyopita, Rais Kikwete, alikiri kufahamu kuhusu kuugua kwa Ballali, lakini alikanusha uvumi kwamba Gavana Ballali amekimbia tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa BoT.

Inaelezwa kwamba siku Kikwete alipokutana na waandishi wa habari Jumatano iliyopita, ndiyo siku ambayo barua inayoelezwa kuandikwa na Ballali ilipotumwa na kupokewa Ikulu lakini hakuna taarifa rasmi za kuthibitisha hilo ambazo zimetolewa hadi sasa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Rais Kikwete yuko likizo na kwamba “kama kuna barua kama hiyo hushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi serikalini” na Rais kuifanyia kazi atakapomaliza likizo.

Ballali yuko Marekani kwenye Jimbo la Massachusetts, jiji la Boston, ambako alifanyiwa upasuaji mkubwa. Yuko huko sasa kwa zaidi ya miezi mitatu, lakini afya yake bado haijatengemaa kiasi cha kuweza kurejea nchini kuendelea na kazi.

Aliondoka nchini kimya kimya na hakuna mtiririko mzuri wa taarifa za hali yake ya afya pamoja na baadhi ya watu kusema kwamba ni lazima taarifa hizo zitolewe kwa mujibu wa taratibu za ‘kiserikali.’

“Wakati Baba wa Taifa (Julius Nyerere) anakwenda London 1999, Serikali ilitangaza ya kuwa anakwenda kuangaliwa afya yake kama kawaida yake na hata hali ilipozidi kuwa mbaya, Serikali ilisema anaendelea vizuri na matibabu. Hiyo ndiyo lugha ya kiserikali,” anasema mmoja wa watu wanaofuatilia suala hili kwa karibu.

Hakuna ambaye ameweza kuzungumzia kwa ufasaha suala hilo la Ballali, na hasa juu ya habari kwamba amekwisha kujiuzulu. Nakala ya barua ambayo inaaminika kuwa ni yake kwenda kwa Rais, na ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuiona na kuichapisha, Gavana Ballali anasema ya kuwa kutokana na "sababu za kiafya" hatoweza kuendelea na wadhifa huo na hivyo anaomba idhini ya kupumzika.

Zimekuwapo taarifa hata hivyo, kuwa baadhi ya maofisa na viongozi waandamizi wa serikalini wamekwenda kumjulia hali Gavana Ballali, akiwamo Rais Kikwete mwenyewe alipokuwa ziarani nchini Marekani hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman, ambao wote wanaelezwa kuguswa na kuumwa kwake.

Mmoja wa waandamizi hao anaelezwa kumtembelea Ballali Jumapili ya Desemba 2, 2007 ambako alielezwa kuonyesha mshangao wa dhahiri wa jinsi “muujiza wa Mwenyezi Mungu” ulivyomsaidia Ballali kupambana na maradhi yanayomsumbua.

Mbali ya kuguswa na “muujiza wa Mwenyezi Mungu” mazungumzo hayo yaligusia uwezekano wa Ballali kujiuzulu ili kutoa nafasi ya kuteuliwa kwa mrithi wake, lakini pia suala nyeti la kurejea ama kutorejea kwake lilikuwa sehemu ya mazungumzo hayo.

Hata hivyo, habari zinasema suala la kutorejea nchini kama afya yake itaruhusu haliipendezi kabisa familia ya Ballali kutokana na kuwa ni nyumbani kwao ambako mama yake mzazi na ndugu zake bado wanaishi.

Ballali ambaye anapewa heshima ya juu na jamii ya Kitanzania nchini Marekani na hata watu wa mataifa mengine waliopata kufanya naye kazi, ana nyumba yake binafsi eneo la Bethesda, Maryland Kaskazini Magharibi mwa Washington, D.C.

Ballali mbali ya kwenda Marekani kama mwanafunzi mwaka 1959 alifanya kazi kwa miaka mingi akianzia na Sauti ya Amerika (VOA) kabla ya kufanya kazi Benki ya Dunia (WB) kwa takriban miaka 25, kazi ambazo zilimuwezesha kujijengea makazi nchini humo huku akitajwa kuwa na hati ya ukaazi ambayo wafanyakazi wengi wa hadhi yake hupatiwa.

Kuugua kwake na hatimaye kutangazwa kuwa amejiuzulu, kumekuwa na maswali mengi bila majibu na wakati wote taarifa zake zimekuwa zikitolewa nusu nusu bila kuwa na undani wa kutosha na hadi sasa Wizara ya Fedha, ambayo ndio mwajiri wake haijawahi kutoa taarifa ya wazi kuhusiana na hali yake wala kuhusu kujiuzulu kwake.

Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, aliwaambia waandishi wa habari kwamba hajapokea barua ya kujiuzulu kwa Ballali, kwa maelezo kwamba taratibu zinamtaka kuwasilisha barua kwake na si kwa Rais kama ilivyoripotiwa. Hata hivyo, Meghji alikiri kufahamu kuugua kwake.

RAIA Mwema limeelezwa kwamba Gavana Ballali alilazimika kuwasiliana na wasaidizi wake walioko Dar es Salaam, ambao waliandika barua hiyo kwa maelekezo yake na baadaye ilipelekwa Ikulu kwa faksi kabla ya barua halisi kupelekwa kwa njia ya kawaida na kupokewa.

“Kwa sasa kinachoumiza watu vichwa si kujiuzulu ama kutojiuzulu kwa Ballali, bali ni nani atakayebeba jukumu la kuiongoza BoT ambayo imechafuliwa kwa tuhuma luluki za ufisadi na ukiukwaji mkubwa wa maadili,” kinaeleza chanzo cha habari serikalini.

Agosti mwaka huu Rais Kikwete alifanya uteuzi wa Manaibu Gavana watatu kama sheria mpya ilivyotaka. Walioteuliwa ni; Profesa Benno Ndullu, Lila Mkila na Juma Reli. Uteuzi wa Profesa Ndullu ndio uliogusa zaidi hisia za wengi kutokana na kutajwa kama mmoja wa wanaotajwa kuwa na uwezo wa kumrithi Ballali.

Profesa Ndullu anatajwa kuwa na historia ya utendaji mzuri tokea akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anaelezwa kushiriki katika mchakato wa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kipindi ambacho Kikwete alikuwa Waziri wa Fedha.

Anaelezwa kwamba aliondoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1989 kwenda Nairobi, Kenya kuwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa African Economic Research Consortium kabla ya kujiunga na Benki ya Dunia akifanya kazi Dar es Salaam na baadaye makao makuu, Washington D.C kabla ya uteuzi wa kuwa Naibu Gavana.

Profesa Ndullu anaelezwa kuwa karibu sana na washauri wa Rais wa mambo ya uchumi kutokana na kufanya nao kazi muda mrefu lakini pia kuna wanaosema kwamba alihusishwa katika kuteuliwa kwao.

Wengine wanaotajwa ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Blandina Nyoni, ambaye aliwahi kuwa Mhasibu Mkuu wa Serikali; Dk. Natu Mwamba wa BoT; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, ambaye alitokea BoT; Naibu Katibu Mkuu, Mipango Joyce Mapunjo, ambaye alitokea Hazina na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei.

BoT imekua ikisakamwa kutokana na tuhuma mbalimbali na hivi sasa inasubiriwa ripoti ya wakaguzi wa kimataifa kutoka Kampuni ya Ernst&Young iliyokabidhiwa kazi hiyo na Serikali kupitia ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG).

Taarifa kuhusu ripoti hiyo zimetolewa zikiwa zinatatanisha baada ya Waziri Meghji kusema itatolewa wiki hii baada ya kupitiwa na CAG, huku CAG mwenyewe, Ludovick Utoh akisema kwamba ndio kwanza ameipokea Jumapili iliyopita na kwamba atamkabidhi Rais Januari, 2008.

Kutoka Raia Mwema wiki ya 52 ya mwisho mwaka 2007.

No comments: