Miaka miwili ya uongozi wake.
SWALI: Naomba kukupongeza. Halafu swali langu la msingi ni; Wakati unaingia madarakani na ulipokuwa ukizungukia wizara mbalimbali ulikuwa ukizungumiza sana hili suala la kuwawezesha wafanyabiashara wa kati na ulisema kwamba uchumi wa nchi hauwezi kukua iwapo hatutakuwa na kada ya kati ya wafanyabiashara. Sijui kama ndiyo sababu lakini naona ndiyo chanzo cha fedha maarufu kama Mabilioni ya Kikwete yalipotoka kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara hao na hatua kadhaa zikachukuliwa kama wamachinga kuwapeleka Kigogo-Sambusa. Napenda kupata tathmini yako, hivi ndivyo ulivyokuwa unapanga ifanyike?
Hatua tuliyoifikia sasa hivi na je, umeridhishwa na matumizi ya Mabilioni ya Kikwete jinsi yalivyotumika na kama ukiamua kutoa fedha nyingine unaweza kuzitoa katika utaratibu ule ule ambao uliutoa wakati uliyopita?
Naomba niunganishe pia na hili kwamba kuna makubaliano ya nje kwa mfano EPA, EBA na AGOA. Je, nini tathmini yako kuhusu wafanyabiashara wetu? Wamepeleka bidhaa? Wameweza kutimiza fursa yetu. Swali la mwisho. Ipo minong”ono kuwa Serikali yako ni kubwa, je, wewe unaiona hivyo?
KIKWETE: Kuwawezesha wafanyabiashara wa kati mabilioni nimeridhika. Na yanavyotumika na kama utatoa mengine, utatoa katika mfumo huu? Hayo mabilioni si ya wafanyabiashara wa kati. Haya mabilioni haya kwa kweli ni ya wale wa chini kabisa, wa chini. Ya kuwawezesha watu waweze kuwa na miradi midogomidogo.
Kwa maana hii mimi nilikuwa nazungumzia kuunda, daraja la kati linahitaji misaada ambayo zaidi ni ya sekta ya kibenki ili waweze kupata mikopo, waweze kutumia mikopo ile kwa ajili ya kukua.
Hizi nyingine hizi ni kiasi kidogo. Huwezi kusema mfanyabiashara wa kati anakwenda kukopa 300,000. Nia ni kuwasaidia wale wadogo kabisa ili waweze kupata mitaji midogo midogo, waweze kujenga misingi yao.
Tunaendelea kulifanyia kazi tuone tutafanyaje. Kwa hili ambalo ni la mabilioni, Je umeridhika? Kuna maeneo nimeridhika, kuna maeneo mengine, lazima tufanye marekebisho makubwa.
Kwanza, kilichojitokeza kwa mpango huu tulioanza nao wa kwanza kupitia hizi benki mbili za NMB na CRDB. CRDB wao kazi yao kubwa ni kwenye SACCOS, NMB wanakopesha watu mmoja mmoja na vikundi vikundi.
Si kila mahali benki hizi zipo. Kwa hiyo kuna wilaya nyingine zimekosa kwa sababu ya kutokupatikana kwa fedha na ndiyo tuna ile awamu ya pili ya bilioni 10 na nusu zilizobakia ambazo tunazipata. Sasa hizi Microfinance Institution (zinazotoa mikopo midogomidogo ya fedha) kama Pride na wengine sasa kwenye hii awamu ya pili tunazitumia hizi.
Hizi tunadhani ndizo zitakazoweza kufika kwenye maeneo mengi sababu hawa sasa wana mtandao mpana zaidi kuliko ule wa haya mabenki. Yapo mapungufu ambayo kwamba ni mafunzo tu kwa sababu ndiyo kwanza tumeanza na ambayo tunayatumia katika hizi tutakazozitoa katika hii ya 10.5 na tutakapotoa tutatoa katika mfumo huo huo.
Lakini nadhani yale mapungufu yote ambayo yamejitokeza sasa ni mambo ambayo tutayazingatia ili tuyaepuke, ili wengi zaidi waweze kupata katika utaratibu wake, lakini jambo la kutia faraja ni kwamba ulipaji unaridhisha sana, sababu kitu kikubwa cha kwanza ambacho mabenki yalikuwa yanahofu sana ni kwamba walikuwa hawaamini kwamba hawa wakopaji wadogo hawa wanalipa, lakini wenye benki wanashangaa, kumbe wakopaji wadogo ni walipaji wazuri.
Wakopaji wadogo tatizo lao kubwa lilikuwa ni dhamana ili waweze kupata hizo hela, watu wanakopa milioni moja, mbili na wanalipa vizuri. Kwa hiyo naweza kusema hivyo.
EPA, EBA, AGOA.EBA (Everythings But Arms), kwamba tumeambiwa kule Ulaya tunaweza kuuza chochote kasoro silaha, AGOA kuna bidhaa 5,000 tunaweza kuuza Marekani Duty Free (Bila kulazimika kulipa kodi). Tanzania hatuja-perform vizuri sana kwenye AGOA na hata Balozi wa Marekani aliyepita yule siku moja alikutana na wafanyabiashara akasema amewachoka wafanyabiasha wa Tanzania, wananung’unika tu. Wenzao wanauza, wao wananung’unika tu (kicheko).
Eeeh, sisi ukilinganisha na wenzetu wengine hatujafanya vizuri sana. Wengine wanauza sana. Sasa hivi ndiyo tumeanza kuongezeka hasa kwenye soko la nguo. Kwa hiyo, ni eneo ambalo lazima tufanye vizuri zaidi,
Kwa Everything But Arms (EBA), Ulaya ndiko soko letu kubwa, tunauza vizuri lakini bado kwenye mpango huu wa EBA tungeweza kuuza vingi zaidi ya hivi tunavyouza sasa.
Kitu kipya kimeongezeka pale ni minofu ya samaki, lakini ukiacha ile minofu ya samaki bado tunauza vitu vyetu vile vya tangu enzi na enzi, kwa hiyo bado ipo kazi kubwa kwa upande wetu kutumia nafasi hizi za biashara.
EPA ni Economic Partnership Agreement. Sasa hizi ndiyo tuko kwenye mchakato wake. Ni mapema mno kufanya tathmini yapi tumefanikiwa, vipi ama hatujafanikiwa vipi.
Na nadhani tunaelekea sasa mwishoni halafu tuone baada ya hapo itakuwaje. Lakini kwa maana ya hizi EPA, kwa nchi masikini kama zetu, bado tunaendelea na utaratibu huu wa zamani. Sasa hivi tulikuwa na mkataba ule wa kuuza kila kitu katika nchi zile za Ulaya, sasa EPA ni kwamba mnauziana, kwamba wale wanafungua masoko yao na nyie nmatakiwa mfungue masoko yenu. Kwa sasa inazihusisha zaidi nchi nyingine. Sisi hadi itakapofika kwenye kiwango.
SWALI: Kuna madai kwamba Serikali inafanya mambo mengi baada ya kushinikizwa na wapinzani, kwa mfano uundwaji wa kamati ya kufuatilia mikataba ya madini.
KIKWETE: Ninachoweza kusema ni kwamba kwanza kusikiliza wananchi. Kusikiliza ni wajibu. Tunasikiliza wananchi, vyama vya upinzani, tunasikiliza mtu ye yote yule.
Kwenye hili la madini nilichokuwa nafanya mimi, nilichotaka ni tuondoe zile kelele. Unajua watu walikuwa wanajenga dhana kwamba sisi katika Serikali hatujali maslahi ya nchi hii. Kwamba raslimali zinachukuliwa tu, zinapondwa tu, watu wananufaika tu na sisi tumekaa kimya.
Kwanza nilisema kwenye hotuba yangu ya Bunge tarehe 30 Desemba (2005) kwamba tutayatazama. Nililokuwa nalo kichwani ilikuwa kwanza nianze na maeneo haya na ilipofika mwezi Machi (mwaka jana) nilipotembelea Afrika Kusini ndiko nilipotoa tamko la kwanza pale kwamba mikataba ya madini tutaitazama.
Kwenye press conference (mkutano na waandishi) niliyokuwa nazungumza na Rais Thabo Mbeki sikuulizwa, nikasema. Nikajua kwamba pale pale Afrika Kusini ndipo penyewe-kwenye kitovu cha migodi. Na kwa kweli. Nimepokea simu sijapata kuona. Watu wakaanza kusema “sasa wamerudi kwenye yale yale ya zamani. Sisi tulijua tu nchi hii haina maana”!
Nikawaambia hapana. Sasa pale ndiyo tukawa tumeeleza. Lakini nimelisema lile ikiwa tayari nimekwisha kuanzisha ndani ya Serikali timu ambayo ilikuwa inaangalia maeneo yenye upungufu kwenye sheria ya madini na kwenye mikataba yetu ya madini ili tufanye marekebisho yatakayowezesha kwamba sisi Mungu bahati nzuri katupa rasilimali, lakini bahati mbaya hakutupa utajiri wa fedha za mitaji.
Hatukubahatika kuwa na ujuzi wa raslimali watu, hatukujaliwa kuwa na teknolojia. Sasa kuna wenzetu hawana madini lakini wana fedha, wana ujuzi, wana teknolojia. Sasa lazima tuingie kwenye mfumo ambao wao wanapata na sisi tunapata.
Lakini sasa kwenye hizi za madini kumekuwa na mambo mbalimbali na mimi nayafuatilia kwamba yana vitu ambavyo ni lazima tuvifanyie marekebisho ili na sisi ambao hatukujaliwa kuwa na fedha, teknolojia wala ujuzi wa kutosha na utaalamu bado tunaweza kunufaika kwa rasilimali ambazo mwenyezi Mungu ametujalia.
Lakini muundo ulivyokuwa ni kwamba wananufaika zaidi wale wenye teknolojia, wenye mitaji na wenye utalaamu. Kwa hiyo, tumekaa pale timu ya Masha (Laurence). Walikuwa wanakwenda kuangalia na wakati nilipokuwa nazungumza Afrika Kusini wakati huo kwamba nilikuwa nimeshafanya uamuzi kwamba sasa la kwanza tunaloanza nalo ni lile la kufanya marekebisho ya kile kipengele cha sheria-maana ya sheria.
Wala si sheria ya juzi, ni sheria ya mwaka 1973. Baadaye katikati iliondolewa, lakini ikarudi tena mwaka 1998.
Kwamba hiki kipingele kiondoshwe maana kipengele hiki kinamlinda mwekezaji asipate hasara kwa hiyo wewe mwekezaji ukipata hasara, kama mtaji wako hukuufidia unapewa capital allowance ya asilimia 5 unaendelea.
Kwa hiyo kwanza mtatakiwa depreciate kwa 100% ndio uanze kulipa kodi. Sasa (mwekezaji) akisema “jamani mambo yangu hayakwenda vizuri mnampa msamaha wa asilimia 50. Kwa hiyo kila mwaka anasema “mambo hayakwenda vizuri” mnamwongezea mnampa msamaha wa asilimia 50.
Kwa hiyo makampuni yale mengine yangekaa maisha yao yasingelipa kabisa. Ndiyo tukasema hili ndilo la kuanza nalo, kwa sababu kwenye sheria ya madini ambayo ndiyo sheria iliyopo, hiyo haina mazungumzo na mtu, eti kwamba waziri na mwekezaji wanakaa wanazungumza.
Sheria imetamka asilimia tatu mrahaba, asilimia 30 kodi ya kampuni, asilimia 25 katika huduma za kiufundi, asilimia 15 menejimenti na asilimia 10 gawiwo.
Ile imetamkwa ile. Ile haina mazungumzo. Mazungumzo yanakuwa kwamba; “sasa sikiliza bwana. Hii nataka kuwekeza bwana lakini pale yule amewahi bwana. Sasa vipi?”
Unasema, “ngoja sasa tutabadili hizi karatasi ili ionekane wewe umewahi”. Haya ndiyo yanaweza kuwa mazungumzo. Umemdhulumu mtu.
Lakini ule mgawo wa Serikali hauna mazungumzo na mtu kwa sababu ni vitu vilivyotamkwa kwenye sheria na ndiyo maana tukasema maadamu imetamkwa katika sheria yetu na sheria ikatamka tena kwamba kama ile kodi ya asilimia 30 inalipwa akishalipia gharama zake zote za uwekezaji weka asilimia 100. Huu ni utaratibu popote duniani na wala si utaratibu wetu sisi peke yetu. Hapana. Unaanza kulipa kodi ukishakuwa umepata capital allowance.
Lakini sasa walipoingiza ile asilimia 15 ni kwamba sasa ile yeye ni juu yake ni kwamba haiishi sasa. Yeye atasema; “ bado, bado”. Ni kwamba inatuzuia sisi kupata zile allowance. Sasa tukasema sisi hapa hii asilimia 30 tukipata tumepata ya kutosha.
Lakini kwa sababu ipo kwenye sheria yetu si kosa la yule mwekezaji hata kama ndiyo kulikuwa na na mazungumzo huko, maana wanasema sijui wakubwa gani walitushauri hata kama walishauri, tulishakubali, tumekubali wenyewe si kosa lake, tumempa wenyewe usiende ukasema; “sasa unajua kuanzia sasa kila mmoja ile asilimia 15 imefutwa, na wote waliopata huko nyuma hakuna”.
Kwa sheria, itaanza kwa wale toka siku ile umetangaza lakini huyu wa nyuma ambaye una mkataba naye haibadiliki hivyo, Vinginevyo uamue kutaifisha. Kwa hiyo tukasema hawa sasa jawabu letu sisi kama waungwana ni kuzungumza nao.
Ndiyo tukaanza ule mchakato. Tukaanza na Barrick, Resolute na Anglogold. Hawa ndio wakubwa, lakini yapo mengine ambayo tumekuwa tunaendelea nayo. Tumekuwa tukiendelea nayo sisi ndani kiserikali lakini kuna wenzetu huko nje wanadhani kwamba sisi ndani ya serikali huku ni mkusanyiko tu wa majitu yasiyokuwa na uchungu wa nchi hii. Nikasema basi.
Haya tunayofanya sisi hebu tuwashirikishe na wenzetu nao waone. Ndio msingi wenyewe, maana nilikuwa nadhani kwamba ni jambo zuri tu. Nilidhani uamuzi ule ni uamuzi wa busara kulingana na mazingira yetu.
Nadhani uamuzi huo ni uamuzi unaotusaidia. Nchi imetulia sasa, maneno hayapo. Nimesikia juzi juzi wakubwa walikuwa huko wanasema; “sasa tunataka na ile ya Masha nayo tupewe”!
Ile kamati ilikwisha kupewa na wanaifanyia kazi, lakini mimi nashukuru angalau (wapinzani) wanakiri kwamba kumbe kulikuwa na kazi iliyokuwa inaendelea na tuliyokuwa tunatekeleza.
Sisi tunatekeleza kwa mujibu wa yale tuliyokuwa tumeyaona. Tumeanza na lile la asilimia 15, kwa hiyo tunakwenda kwenye mambo mengine ambayo tutaendelea nayo.
Kamati hii itachangia, itaongeza mchango mkubwa zaidi kulikoni ile ya maofisa wa Serikali. Maofisa wa Serikali wale watakuwapo kama msaada kuona vile walivyokuwa wanafikiria. Nadhani baada ya hapo tutapata jambo jema.
Kwa hiyo sisi kama Serikali tupo tayari kusikiliza. Tutasikiliza mpinzani, tutasikiliza NGOs, tutamsikiliza hata mtu binafsi. Mimi nasikiliza sana. Hata kwenye simu zangu wakiniletea mimi nikisikia ni jambo la maana nalifanyia kazi, nalichukulia hatua. Nadhani ndiyo wajibu wetu.
SWALI: Sasa ni miezi mitatu Gavana wa Benki Kuu hayupo nchini na hakuna taarifa zozote za Serikali. Tumesikia kuwa amekimbia kutoka na ukaguzi unaoendelea Benki Kuu (Rais anacheka). Nilikuwa naomba ufafanuzi.
KIKWETE: Gavana anaumwa. Gavana anaumwa na amekuwa kwenye matibabu. Si kwamba amekimbia. Hapana, ni ugonjwa tu, anatibiwa.
SWALI: Watu wategemee nini ili ikifika mwaka 2010 kusiwe na kusutana? Na je, kuna ukweli gani kuhusu uvumi unaoenea mitaani na kuwaweka watu matumbo joto kwamba kuna mabadiliko ya Baraza la Mawaziri?
KIKWETE: Watu wategemee nini 2010? Mimi nasema kitu cha kutegemea ni kwamba kama nilivyosema nadhani narudia yale yale kwamba kuna kitu ambacho tumewaahidi Watanzania. Tumeahidi kwenye ilani yetu, tumeahidi huko. Kuna yale ya papo kwa hapo. Jitihada tunazohitaji sasa ni ikifika 2010 waseme tuliyoahidi yametimia, nisingependa tufike 2010 tusutwe; Tulisema hili, hakuna tulisema hili hakuna. Mimi nadhani kwamba tutatekeleza ahadi.
Uvumi wa Baraza la Mawaziri ni uvumi tu. Baraza la mawaziri nalibadilisha wakati wote ni uvumi tu. Ikiwapo haja tutabadili. Kama hakuna haja tutaendelea. Lakini kwa sasa tuchukulie kwamba ni uvumi au ni matakwa ya watu.
Kutoka Raia Mwema wiki hii ya mwisho wa mwaka 2007
No comments:
Post a Comment