Thursday, December 06, 2007

Hakimu Dar adakwa usiku kwa rushwa


*Yadaiwa aliomba milioni 5/- akatanguliziwa m.1/-
*TAKUKURU yaweka mtego yamkamatisha kwa 700,000/-
*Alisubiri mzigo wake katika hoteli ya kimataifa

Na Mwandishi Wetu

WAKATI mahakama zikiwa na tuhuma nzito ya kujihusisha na rushwa, Hakimu wa Wilaya ya Temeke, Bibi Jamilah Nzota, amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), akipokea rushwa ya sh. 700,000 kutoka kwa mlalamikaji wa kesi ya madai anayoisikiliza.

Mbali na Hakimu huyo pia watu wengine wanne nao wamekamatwa wakituhumiwa kushawishi wa kupokea rushwa katika matukio tofauti.

Hakimu huyo alikamatwa juzi saa 4 usiku katika hoteli ya Slipway, Msasani na maofisa wa TAKUKURU, ambao waliweka mtego huo baada ya kupewa taarifa na mwombwa rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa wa Temeke, Bibi Domina Mukama, alisema Bibi Nzota alipokea rushwa hiyo ambayo ilikuwa ni sehemu ya malipo aliyokubaliana na mtoa taarifa huyo ya sh. milioni tano, ili ampe ushindi katika kesi anayodai.

"Hakimu huyo tayari alishapokea sh. milioni moja kwa hiyo hii ilikuwa ni mara ya pili, ambapo mdaiwa alifika hapa na kutupa taarifa na sisi tulitoa sh. 700,000 kwa ajili ya mtego wa kumkamata," alisema Bibi Mukama.

Kesi iliyosababisha Hakimu huyo kukamatwa na rushwa ni namba 33/2007 ambayo ilikuwa inatakiwa kusikilizwa mahakamani hapo juzi, lakini Hakimu huyo aliiahirisha na kumtaka mlalamikaji katika kesi hiyo, kumalizia kiasi cha fedha alichokuwa akikitaka.

"Alipofika hapa alisema wamekubaliana kukutana saa 9 alasiri, lakini Hakimu hakutokea muda huo hata hivyo waliendelea kuwasiliana kwa simu na ilipofika saa 4 usiku, Hakimu alikuja na mtego wetu ukawa umefanikiwa.

"Lakini kitendo cha maofisa wangu kukaa muda mrefu pale kilisababisha watu wengine kutoa taarifa Polisi ya kutowaamini na polisi walifika hapo, lakini waliwaeleza nia iliyowafikisha pale hivyo waliendelea na kazi yao," alisema Bibi Mukama.

Baada ya kukamatwa, Hakimu huyo alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam na kuwekwa rumande na jana alichukuliwa kwa ajili ya mahojiano na kwa mujibu wa Bibi Mukama, atapewa dhamana huku taratibu za kumfikisha mahakamani zikiendelea.


Katika tukio lingine ambalo lilitokea juzi Kigamboni, maofisa wa TAKUKURU waliwakamata watu watatu wanaodhaniwa kuwa vishoka wa TANESCO, baada ya kushawishi na kupokea rushwa ya sh. 250,000 ili kurudisha nyaya za umeme ambazo zilikuwa zimekatwa katika mazingira ya kutatanisha, katika eneo la Ugindoni, Kibada.

Watuhumiwa hao ni Bw. John Kasambala, Bw. Frank Japhet na Bw. Simba Kasambala, ambao walibainika kuwa na tabia ya kukata nyaya za umeme kisha kuomba fedha kwa wananchi ili kurejesha umeme huo na awali walikuwa wametaka rushwa ya sh. 400,000, lakini walipunguza hadi kiasi hicho.

Wakati huo huo, TAKUKURU imemkamata Koplo Anthony Mwakanyamale, ambaye alipokea rushwa ya sh. 40,000 kutoka kwa mtoa taarifa wa TAKUKURU, ambayo aliiomba ili kumaliza kesi inayomkabili ya kuharibu mali ya mtu na kuhakikisha haifiki mahakamani.

Bibi Mukama alisema baada ya kukamilisha taratibu zote, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani, ili kujibu tuhuma zao.

Naye Patrick Mabula anaripoti, kwamba TAKUKURU wilayani Kahama, Shinyanga, imemfikisha mahakamani, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Ubagwe, Bw. Saakumi Mihayo, kwa kuomba na kupokea rushwa.

Ilielezwa kuwa Mwalimu Zakayo anadaiwa kuomba rushwa ya sh. 160,000 kutoka kwa Mkandarasi waliyekuwa wamempa kazi ya kutengeneza madawati 20 ya shule ya msingi mpya ya Mulungu waliyokuwa wamejenga wananchi kwa nguvu zao, iliyokuwa ikisimamiwa na mwalimu huyo.

Akisoma mashitaka hayo juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Kahama, Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Bw. Lupyana Mwakitobe, alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Novemba 15 mwaka huu.

Mwendesha Mashitaka huyo aliendelea kusema mbele ya Hakimu, Bw. Juma Hassan, kuwa Mwalimu Zakayo aliomba kiasi hicho cha pesa akiwa Kahama ili kiwe kishawishi ya kumwidhinisha malipo yake mkandarasi huyo ambaye alikwenda kutoa taarifa TAKUKURU na mtego ukaandaliwa.

Bw. Mwakitobe alisema katika mtego huo, mshitakiwa alipokea sh. 90,000 kama kishawishi cha kumwidhinishia malipo ya mkandarasi huyo, kama malipo ya awali, ndipo alipokamatwa kutokana na mtego uliokuwa umewekwa na TAKUKURU.

Mwalimu Zakayo alikana mashitaka hayo mbele ya Hakimu Hassan na dhamana yake ilikuwa wazi, lakini alikosa wadhamini na kurudishwa rumande hadi Desemba 10 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.

No comments: