Thursday, December 06, 2007

WARAKA KUTOKA HUSTON, MAREKANI

Ili tuendelee tunahitaji watu (2)

Innocent Mwesiga.

nchi ya kwanza barani Afrika kujipatia uhuru. Usiku wa kilele cha sherehe za uhuru, Rais wa Ghana, Kwame Nkrumah alisema anayo furaha kuona, kwa mara ya kwanza, Waafrika wanapata nafasi ya kujiamulia mambo yao wenyewe. Kwa kipindi cha wastani wa takribani miaka 50 ya uhuru, nchi za Afrika zimetawaliwa na jumla ya marais wasiopungua 200.

Wakati wa shamra shamra za maadhimisho ya jubilee ya uhuru wa nchi za Afrika, ni vema kukubali ukweli kuwa matumaini aliyokuwa nayo Nkrumah ya Waafrika kujiamulia mambo yao wenyewe yanazidi kufutika kadiri muda unavyozidi kuyoyoma. Kati ya marais 200 waliozitawala nchi za Afrika, ni marais wasiozidi 10 tu wanaostahili kuigwa kutokana na juhudi zao binafsi za kutetea uhuru wa Mwafrika wa kujiamulia mambo yake mwenyewe.

Sehemu kubwa ya viongozi waliosalia imekuwa ni msalaba kwa nchi za Afrika. Kiwango cha mataabiko na umasikini unaowakumba Waafrika unawiana na tabia za marais waliozitawala nchi za Afrika. Makosa tuliyoyafanya ni kuwaachia watawala madaraka makubwa ya kuwaamria Waafrika mambo yanayohusu maisha yao.


MWALIMU Nyerere, mmoja wa viongozi bora ambao Afrika imepata kutoa

Mfano, katiba ya nchi itampaje mamlaka ya mwisho mtawala mithili ya Rais Jean-Bedel Bokasa aliyewaua wanafunzi waliokataa kuvaa sare za shule zenye picha yake? Au mtawala kama Rais Juvenal Habyarimana aliyesaidia kikundi cha Interahamwe kilichoteketeza malaki ya watu wasio na hatia. Au Rais Mengistu Haile Mariam aliyeanzisha kikundi cha Red Terror kilichowaua wapinzani wake wa kisiasa?

Katiba ya nchi itampaje mamlaka ya mwisho mtawala kama Rais Mobutu Sese Seko Kuku wa za Banga, aliyepora fedha na kujenga majumba ya kifahari katika nchi za Ulaya, wakati raia wa nchi yake wamegubikwa na umasikini wa kupindukia? Au Rais Sani Abacha aliyepora mamilioni ya fedha na kuziweka katika mabenki ya Uswisi?

Vioja ambavyo vimekwisha fanywa na watawala wa nchi za Afrika vimetufikisha mahala ambapo baadhi ya Waafrika wamekata tamaa.Wengine wamefikia mahala pa kudhani kwamba Mungu ndivyo alivyotuumba sisi Waafrika na hatuwezi kubadilika.

Nilipata kusikia mwandishi wa kitabu cha Waafrika Ndivyo Tulivyo akisema kwamba ubinafsi wa mtu mweusi ni mkubwa ukilinganisha na ubinafsi wa mzungu. Kwamba hiyo ni sababu mojawapo ya matatizo tuliokuwa nayo katika nchi za kiafrika.

Binafsi, siamini katika dhana kwamba, udhaifu wa watu unatofautiana kutokana na utofauti wa rangi ya ngozi yao, au utofauti wa nchi watokazo. Adolf Hitler wa Ujerumani, Iddi Amini wa Uganda, Mobutu Sese seko wa Zaire, Alberto Fujimori wa Peru, Ferdinand Marcos wa Ufilipino, na wengineo, ni baadhi ya mifano inayoonyesha kwamba, udhaifu wa mwanadamu hauna mahusiano na rangi ya ngozi au nchi atokayo.

Ni mang’amuzi ya udhaifu wa kawaida wa kibinadamu, yaliyowafanya wananchi katika nchi nyingi zilizoendelea, kutomwachia mtu mmoja, au kikundi cha watu wachache, mamlaka na nguvu za kupinga utashi wa walio wengi.

Kikatiba, watu wanaokabidhiwa dhamana ya kuwaongoza wenzao, wanawekwa chini ya mwanga wa kurunzi wa jamii nzima. Katiba imewapa wananchi mamlaka ya kukaa chonjo, kuangaliana, kukumbushana, kudhibitiana, kukosoana, na kuhojiana ili kupunguza madhara yatokanayo na udhaifu wa kibinadamu. Haitoshi kumkabidhi dhamana ya uongozi mtu aliyeonyesha mienendo na matendo mema kwa muda mrefu. Wamejiwekea utaratibu wa maisha ambao unahakikisha kwamba, siku mienendo ya kiongozi wa ngazi yoyote inapobadilika na kuwa kinyume cha matarajio ya wengi, basi, ama kwa hiari yake, huyo kiongozi anaachia ngazi kabla ya kipindi cha uongozi wake kukamilika, au wananchi wanampokonya madaraka. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Tonny Blair wa Uingereza na Richard Nixon wa Marekani.

Marekani ni miongoni mwa Nchi zilizoendelea duniani. Ilitawaliwa na Waingereza kama ilivyotawaliwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika. Tofauti na nchi za Afrika, Wamarekani walichukia utawala wa kikoloni pamoja na mambo yake yote. Hawakutaka kurithi Serikali kama ya kikoloni iliyokuwa na mamlaka kuzidi wananchi. Walitupa jongoo na mti wake kwa kumng’oa Mwingereza na mifumo yake ya utawala.

Wamarekani wanaamini kwamba, walikuwa na uhuru pamoja na haki zao kabla ya kuunda katiba. Hivyo basi, katiba yao iliundwa, pamoja na makusudio mengine, kuhakikisha uhuru na haki zote za wananchi zinapata hifadhi na kinga, sio tu dhidi ya hujuma za mataifa ya nje, pia, dhidi ya udhalimu kwa wananchi unaoweza kufanywa na Serikali yao wenyewe.

Haki za wananchi zilikuwepo kabla ya katiba kuundwa, ndio maana, ki msingi, katiba ya Marekani sio chombo cha kuchezea, kuwanyang’anya, au kuwapa wananchi haki zao, bali ni chombo cha kuhifadhi haki zote za wananchi.

Si kweli kwamba viongozi wote wa Marekani wana moyo wa kuipenda nchi yao kuliko wanavyojipenda wenyewe. Kama ilivyo katika nchi zote duniani, wapo viongozi wabinafsi na wala rushwa ndani ya Marekani. Hivi karibuni mbunge Bob Ney kutoka Ohio amekuwa ni miongoni mwa wabunge 40 kutoka ndani ya bunge la Marekani ambao wanatumikia vifungo jela kwasababu ya vitendo mbalimbali vikiwemo vya kula rushwa. Mbunge mwingine anapelelezwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za kuficha dola elfu kumi kwenye jokofu ambayo inadaiwa kupatikana kwa njia zisizo halali.

Binafsi, nadhani kuna viongozi katika historia ya Marekani ambao hawawezi kufua dafu kwa ubora mbele ya baadhi ya viongozi waliopata kuongoza baadhi ya nchi za Afrika. Kama ingekuwepo mizani ya kupima ubora wa viongozi, nadhani mashujaa kama Mandela, Kenyatta, Senghor, au Nyerere wangetoka washindi dhidi ya Rais Richard Nixon wa Marekani.

Hata maamuzi ya uteuzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali, kwa kiasi kikubwa, yanatokana na mashauriano na wananchi. Mfano, Rais wa Marekani anateua viongozi wa ngazi za juu, wakiwemo mabalozi wanaoiwakilisha Marekani nchi za nje, kwa kupata ridhaa ya wawakilishi wa wananchi (rejea ibara ya II kifungu kidogo (2) cha katiba ya Marekani).

Haitoshi kwa Rais wa Marekani kusema kuwa mtu fulani anafaa kuwa balozi wa Marekani nchi za nje. Lazima wawakilishi wa wananchi wakubaliane na Rais. Kama ilivyo Tanzania, hata Marekani kuna makampuni ya kitapeli yanayoingia mikataba na Serikali za miji, majimbo au Serikali Kuu kwa nia mbaya. Tofauti na nchi za nyingi za Afrika, katiba ya Marekani imehifadhi uwezo wananchi kumuondoa madarakani Rais au kiongozi yeyote wa kuchaguliwa kabla ya muda wake kumalizika, pindi wasiporidhishwa na utendaji wake wa kazi.

Matokeo ya hii hifadhi ya kikatiba, wamepata mfumo wa nchi unatoa viongozi wanaowaogopa na kuwatumikia wananchi. Madhara ya udhaifu wa kitaperi, wizi, ufisadi, udikiteta, na mengineyo, yanapunguzwa kwa kiasi kikubwa. Inawezekana ikawepo hoja kwamba Waafrika ndio wanakubali kuhongwa na kuwachagua viongozi wabovu. Sasa wakiwa na mamlaka ya kikatiba kama waliyonayo wananchi wa Marekani, si wataendelea kuwaweka madarakani viongozi wabovu? Jibu lake ni kwanza, haki za msingi za watu hazina mbadala.

Hakuna fikra yenye siha njema inayoweza kusita katika zoezi la kuondoa vigingi vinavyozuia mkondo wa haki za msingi za wananchi.

Pili, ni jambo la kawaida popote pale duniani kwa wananchi kufanya makosa ya kuwaingiza madarakani viongozi mithili ya Fredrick Chiluba, Bakili Muluzi, Mwai Kibaki, na wengineo. Lakini wananchi wana tabia ya kujikosoa wakigundua wamefanya makosa ya kuwaweka viongozi wabovu madarakani.

Mfano, miaka miwili iliyopita, Kikwete amechaguliwa kwa mbwembwe, lakini wananchi haohao waliokuwa wanamshabikia wameanza kumshikia mabango mitaani. Tatu, viongozi wanaoingia madarakani kwa kuhonga, kupiga ramli, wizi wa kura, na mtutu wa bunduki, hawawezi kujikosoa pale wanapokosea. Mambo yanapokwenda mrama hawawezi kuondoka madarakani kwa hiari yao.

Sitarajii marais kama Yoweri Museveni, Charles Taylor, Samweli Doe, Mobutu, Iddi Amin na wengineo, wafike mahala waseme tumekosea hivyo tunawajibika kwa kuachia ngazi!

Katiba ya nchi lazima itoe nafasi kwa wananchi kujikosoa wenyewe ili kumuondoa kiongozi wa kuchaguliwa wakati wowote wanapoona inafaa kufanya hivyo. Mfano, California ni jimbo ndani ya nchi ya Marekani, lakini inasemekana kuwa uchumi wake ni wa nne kwa ukubwa duniani.

Aliyekuwa mkuu (Gavana) wa jimbo, Gray Davis alikubali sera za kufanya mabadiliko katika sekta ya nishati. Mitambo ya kuzalisha umeme ya California iliangukia mikononi mwa kampuni ya Enron kutoka Houston.

Enron ilianza tabia za kitapeli za mgao wa umeme katika katika jimbo la California. Matokeo yake, bei ya umeme ikapanda na gharama za maisha ndani ya hilo jimbo zikapanda pia. Kwa sheria za Marekani, idara za Serikali kuu na sio Serikali za majimbo ndizo zenye mamlaka ya kuzuia ongezeko la bei ya umeme. Hivyo, Gavana Devis na Rais Bush walianza kutupiana lawama na kunyosheana vidole kuhusu suluhisho la tatizo.

Ndipo wananchi wa jimbo la California walipoamua kutatua chanzo cha tatizo lenyewe. Kwa kutumia uwezo uliohifadhiwa ndani ya katiba yao, walianzisha mchakato wa kumuondoa madarakani gavana wa jimbo, Gray Davis kabla ya muda wake kumalizika. Zoezi hilo lilifanikiwa kwa kuitisha uchaguzi mpya ambapo Arnold Schwarzenegger wa chama cha Republican aliibuka mshindi. Pia, huo ulikuwa mwisho wa vitendo vya kitapeli vya kampuni ya Enron.

Tanzania tumewahi kupata mkasa unaofanana na huo wa California lakini utatuzi wake ulikuwa tofauti kutokana na mfumo wetu wa kuwalimbikizia madaraka watu wachache. Mfano, ripoti ya Transparency International, mwaka 1995, inaonyesha kuwa Serikali ya Tanzania iliridhia kusainiwa mkataba wa ununuzi wa umeme baina ya Tanesco na kampuni ya IPTL. Katika vuta ni kuvute ambayo mantiki yake haieleweki, iliamriwa kuwa Tanesco itakuwa inailipa IPTL dola milioni 2.5 kwa mwezi kwa kipindi cha miaka 20 iwe IPTL inazalisha umeme au haizalishi. Ingawa wananchi wanachangia gharama za kuilipa IPTL kila mwezi, lakini bado wanakabiliwa na makali ya mgao wa umeme.

Serikali mpya ilijaribu kulitatua hili tatizo kwa ambayo imeundiwa kamati na Bunge letu. Toka mwaka 1995 mpaka sasa, tatizo la umeme halijapatiwa ufumbuzi. Hii inatokana na dhana ya kuwaachia waliolisababisha walitatue. Matokeo yake, wananchi wanaongezewa matatizo mengine.

Kikatiba, nchi ya Marekani hakuna mtu yoyote mwenye uwezo wa kukopa fedha kwa niaba ya nchi isipokuwa Bunge la Wawakilishi wa wananchi (Congress) (rejea ibara ya I kifungu kidogo 8 cha katiba ya Marekani).

Bunge la Wawakilishi wa wananchi ndio chombo pekee chenye uwezo wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha na ukusanyaji kodi. Hii inawapa wananchi nafasi ya kusikiliza mijadala bungeni na kujua kiasi cha fedha kilichokopwa na kwa sababu gani.

Kikatiba, wabunge wa Tanzania wamenyimwa haki ya kutunga sheria ya kutoza kodi au kubadilisha kodi kwa namna yoyote isipokuwa kupunguza. Jukumu la fedha ni la ridhaa ya Rais (rejea ibara ya 99 (1)- (2) kifungu kidogo (a) cha katiba ya Tanzania). Matokeo yake, fedha inakopwa kwa niaba ya wananchi lakini hata wanaopashwa kuwa wawakilishi wa wananchi hawana maamuzi ya kusitisha mikopo ya hovyo.

Mfano, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2004/2005, ilisema Serikali ilipata hasara ya shilingi bilioni 140 kwa sababu ya kukosa nidhamu katika matumizi ya fedha.

Lakini mwaka uliofuatia Mei 9, 2006, Benki ya Dunia ilitoa taarifa namba 2006/400/AFR kwenye vyombo vya habari mjini Washington (press release) kwamba iliipatia Serikali ya Tanzania mkopo wa dola milioni 40 kwa ajili ya uwajibikaji, uwazi, na uadilifu (accountability, transparency and integrity program).

Mikopo ya namna hii isiyoelekezwa katika uzalishaji ndio inayotutia umasikini. Inawezekana ikawepo hoja ya kwanza kwamba Watanzania lazima wawe na mifumo yao ya maisha ambayo sio lazima ifanane na ya Wamarekani au nchi nyingine zilizoendelea. Jibu la hii hoja ni kweli, lakini kipimo cha mifumo ya maisha sio Wamarekani, bali ni jinsi gani hiyo mifumo inavyowasaidia watu kuyabadili mazingira yao.

Kama mifumo haiwasaidii watu kubadilisha maisha yao, basi haitufai na inabidi ing’olewe. Inawezekana ikawepo hoja ya pili kuwa mifumo yetu lazima iendane na hali halisi ya nchi na izingatie historia yetu. Jibu lake ni kwamba hakuna mwanadamu ambaye hali halisi yake ni kutapeliwa, kuongopewa, na kunyang’anywa haki zake za msingi alizopewa na Mungu.

Kama historia yetu ni kukubali kuibiwa, basi tunaweza kusema kwa sauti moja kuwa tumechoka kuibiwa na tukaifuta. Inawezekana ikawepo hoja ya tatu kwamba eti kwasababu Wamarekani wameendelea sio lazima tuwaige. Pia, hakuna ushahidi kwamba hata tukiwaiga tunaweza kufanikiwa.

Jibu la hii hoja ni kwamba viongozi wetu wameiga mambo mengi kutoka Marekani na bado wanaendelea kuiga. Mfano sera za soko huria, utandawazi, ujasirimali, ubaperi, mgombea mwenza (rejea makala ya Pius Msekwa, Raia Mwema toleo Na.1), mitindo ya mavazi na mengineyo.

Kila kukicha viongozi wetu wanakwenda Marekani kuomba misaada ya kifedha. Kwa nini tusichote busara kutoka katika kisima cha Wamarekani zinazowafanya waendelee na wapate fedha za kuwasaidia viongozi wetu?

Hata hivyo, hoja yangu haikujengeka katika mifumo ya maisha kama ubepari au staili za uongozi kama ugombea wenza. Ninachokiongelea ni haki za msingi za binadamu ambazo huwa haziigwi bali tumepewa na Mungu.

Haki ya kushiriki katika maamuzi ya maisha yako, haki ya kuwawakilisha wenzako au kuwakilishwa katika taasisi zinazotunga sheria za nchi ni ya kila mmoja wetu na hapashwi kuwekewa sharti. Hoja ya nne ni kuwa Roma haikujengwa kwa siku moja kwani nchi yetu ni changa ambayo ina umri wa uhuru wa miaka 46 ukilinganisha Marekani ambayo ina umri wa zaidi ya miaka 200.

Jibu lake ni kweli Roma haikujengwa kwa siku moja, lakini ujenzi wa Roma ulianzia katika msingi sio paa. Msingi wa Roma haujawahi kubomolewa tokea ujengwe. Kinachofanyika ni kuweka madoido kwa maana ya kupaka rangi kuta na kuongeza vito vya thamani vinavyoninginia.

Katiba ya marekani ina umri wa miaka zaidi ya 200 lakini imebadilishwa kwa wastani wa mara 17. Mabadiliko yaliyofanyika yalilenga kuziba nyufa za msingi uliojengwa na waasisi wa taifa lao.

Mfano, ilibadilishwa ili kuwarudishia haki ya kupiga kura wanawake pamoja na watu weusi. Mtoto wa nyoka akikomaa anakuwa nyoka si mjusi.

Mifumo ya kuwapa madaraka yasiyo na mipaka watu wachache ikikomaa inakuwa ni ya kiimla au kidikteta. Bunge lenye watu wanaoteuliwa bila kupata ridhaa ya moja kwa moja kutoka kwa wananchi likikomaa linakuwa Bunge la vikaragosi na si Bunge linalo wakilisha maslahi ya wananchi.

Madhumuni ya waraka wangu sio kupendekeza mfumo ambao Rais wetu atakuwa hana madaraka ya kiutendaji kama alivyo Malkia wa Uingereza, la hasha! Nia yangu sio kupendekeza mfumo ambao wananchi wanakuwa na nguvu na madaraka ya kufanya kila watakacho, hiyo itakuwa vurugu mechi.

Waraka huu una nia ya kupendekeza mfumo wa haki ambapo wananchi watakuwa na nguvu na mamlaka ya kujiamulia masuala yanayohusu maendeleo yao.

Kutoka Raia Mwema wiki hii.

No comments: