Tuesday, December 04, 2007


Hoja ya OIC yachemka

na Irene Mark

HOJA kuhusu nchi kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu ya OIC (Organisation of Islamic Conference) inaanza kuzua mjadala, huku watu wakitoa maoni tofauti kuhusu suala hilo.

Suala hilo, ambalo miaka kadhaa iliyopita lilizusha mjadala wa kitaifa, liliibuliwa wiki iliyopita na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, waliojenga hoja kuwa wakati umefika sasa kwa Zanzibar kuruhusiwa kujiunga na OIC kwa sababu sera ya mambo ya nje, imebadilika.

Wawakilishi hao, wakizungumza katika semina hivi karibuni, walisema miaka ya mwanzo ya 1990 Zanzibar ilizuiwa kujiunga na umoja huo kwa sababu nchi ilikuwa inafuata sera ya nje iliyokuwa ikiongozwa kwa misingi ya kisiasa zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

Kwa mujibu wa wawakilishi hao, sera ya sasa ya diplomasia ya uchumi inayotumiwa na serikali zote inatoa fursa kwa visiwa hivyo kufikiria kujiunga katika jumuiya hiyo, lengo likiwa ni kufuata masilahi ya kiuchumi.

Msimamo huo wa wawakilishi ulisababisha mwanasiasa na kiongozi wa Kikristo, Mchungaji Christopher Mtikila kuonya kuhusu kile alichokiita hatari ya jambo hilo kuzungumzwa ndani ya Serikali ya Muungano.

Tangu Mtikila atoe maoni yake kuhusu suala hilo juzi, watu mbalimbali wamejitokeza wakiunga mkono au wakipinga hoja za Mwenyekiti huyo wa Chama cha DP, anayeongoza Kanisa la Full Salvation.

Wanaomuunga mkono, wanaitaka serikali kutojihusisha na suala la kutafuta uanachama wa OIC, wakisema hatua hiyo itakuwa ni kwenda kinyume cha Katiba ya nchi.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, kiongozi wa umoja wa makanisa Wilaya ya Mwanga, ambaye amepata kuwa mwanasiasa, Nathaniel Mlaki, alisema suala hilo lilizusha mgogoro miaka ya nyuma na kuamuliwa.

Akitoa maoni yanayoweza kuibua ukinzani mkubwa siku zijazo, Mlaki alionya kuhusu kile alichokielezea kuwa ni ushirikiano wenye ajenda za siri kati ya Tanzania, Iran na Misri, akirejea ziara ya hivi karibuni iliyofanywa na Makamu wa Rais, Dk. Shein nchini Iran.

Kwa mujibu wa Mlaki, hatua hiyo inaielekeza nchi hii katika mwelekeo wa kutaka ijiunge na umoja huo wa nchi za Kiislamu, hatua ambayo miaka ya mwanzo ya 1990 iliibua malumbano makali ya hoja.

“Huu mgogoro wa IOC tulishaumaliza… ulizua utata sana wakati fulani, lakini yakaisha. Tunaiomba serikali kutojihusisha na suala hili. Kwanza Iran inajiandaa kwa vita ya nyuklia.

“Hatukubali kuingizwa kwenye ushirikiano huu, wanataka kutuletea IOC kupitia Zanzibar lakini hatutakubali,” alisisitiza Mlaki.

Kiongozi huyo aliishutumu Iran na Misri, kwa kujihusisha na silaha za nyuklia.

Msomaji mwingine wa gazeti hili, aliandika ujumbe mrefu kupitia barua pepe, akisema kuwa awali alikuwa akiamini kuwa Mchungaji Mtikila ni mtumishi wa Mungu na mtu makini.

“Sasa naanza kupatwa na mashaka juu ya umakini wake!! Hii zaidi ni kwa yeye kushindwa kufahamu siasa za dunia, aelewe kuwa shutuma inazopewa Iran kwa kurutubisha uranium ni ‘Global propaganda’ za Magharibi zikiongozwa na Marekani kwa mataifa mengine wanayodhani kuwa ni tishio kwa ustawi wao, yeye haelewi suala hili?” alihoji.

Msomaji huyo, alisema kuwa Tanzania ina ushirikiano na Marekani, ambayo ubalozi wake tu hapa nchini unashinda jengo lolote la serikali kimiundombinu wakati inafahamika kuwa nchi hiyo inarutubisha hayo madini ya uranium.

Alisema kuwa, hoja zinazotolewa na Mchungaji Mtikila zinamuonyesha kama mtu ambaye ametawaliwa na udini zaidi kuliko mtazamo yakinifu.

“Suala la watu kusaidiwa kidini, hapa ndiyo anyamaze kabisa kwani hata kanisa lake linapata misaada mingi kutoka kwa wahisani wa mataifa ya kigeni na yeye binafsi ndiyo tegemeo la maisha yake kwa misaada hiyo,” alisema msomaji huyo.

Kama ilivyo kwa watu hao wawili, wananchi wengine kadhaa waliowasiliana na gazeti hili kwa simu au kwa ujumbe wa maandishi, walionyesha ama kukerwa na hoja za Mtikila au kuunga mkono dhamira ya kutaka Tanzania iwe mwanachama wa OIC.


Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: