Na Anti Flora Wingia
Wiki hii nimepokea email ambapo jamaa mmoja anajaribu kumwokoa rafiki yake aliyesongwa na vitimbi vya mke aliyedhani ni mke wa kutulizana kumbe kiruka njia kisichoeleweka.
Je, alimchunguza kabla ya kumuoa na kumuingiza ndani kama mke? Swali hili tulijibu baadaye mimi na wewe msomaji wangu.
Awali ya yote tupate ujumbe muhimu katika email hiyo, kisha tutoe maoni yetu.
Aliyetuma email hii anasema hivi (nanukuu baadhi ya sehemu kutokana na urefu wa ujumbe wake)
Nina rafiki yangu amenijia anataka ushauri kuhusu ndoa yake ambayo imedumu karibu miaka ishirini na tano hivi, ambayo haina raha kabisa.
Rafiki yangu alioa mwishoni mwa mwaka 1981. Yeye na mchumba wake walikutana chuoni walikokuwa wakisoma pamoja huku wakitoka mkoa mmoja ila wilaya tofauti.
Kwa kuwa mwanamme alitangulia kuondoka, mwanamke alibaki chuoni akisaidia kazi.
Katika kuanza kutafuta mke wa kuoa, huyu rafiki yangu akamkumbuka yule dada ambaye walijuana hapo chuoni tu na wala hakumfahamu zaidi ya hapo.
Wawili hawa wakakubaliana kuoana. Lakini bibie huyu akaamua kwanza kuelezea historia ya maisha yake ambapo alisema;-``nilipokuwa na umri wa miaka kumi na tano, wazazi wangu walinioza kwa mwanaume na huyo mwanaume alikuwa na mke mkubwa ambaye ndiye alitumika kuja kunichukua kijijini na kunipeleka wilaya nyingine walikokuwa wanaishi...lakini sikuzaa naye``. (Pigo la kwanza).
Hata hivyo, pamoja na taarifa hii, bwana huyu alimsisitizia bibie kuwa bado anampenda ingawa wazazi wake walipinga ndoa isifungwe mbele ya mchungaji. Hatimaye ndoa ilifungwa.
Miezi mitatu baadaye, bibie akaanza vituko.
Mwanamke akasema ``nasikia deni na kuwiwa moyoni...``nilipoachana na yule mume wa kwanza niliona siwezi maisha ya nyumbani hivyo niliamua kwenda kufanya ukahaba na kupika pombe za kienyeji.
Katika purukushani zangu nikakutana na mwanaume ambaye tulipendana sana na kuamua kuishi kinyumba, na nikiwa katika hali hiyo ndipo nikajiunga na dini, na nikaamua kumuacha kwa sababu ndoa yetu haikuwa ya kidini, alimaliza.
(Pigo la pili).
Baada ya maelezo haya toka kwa bibie, mumewe kwa mshtuko akamuuliza,``kwanini hukuniambia kabla hatujaoana kama ulivyofanya kwa yule mwanaume wa kwanza?
Akajibu ``niliona kuwa unaweza kuniacha nami nilitaka kuolewa nawe muda mrefu hata kabla hujanitafuta``.
Pigo hili la pili lilimsumbua sana jamaa huyu japokuwa marafiki zake walishauri avumilie tu kwani maji yalishamwagika.
Baada ya mwaka mmoja vitimbi vikaongezeka.Mke huyu akawa mkali kwa mumewe, hataki aulizwe kitu.
Mume akitaka waende wote outing hataki, kununua mahitaji ya familia pamoja hataki, ili mradi kila kitu alimkatalia mumewe. Hata ukaribu chumbani ilikuwa mgogoro.
Mwanamke pale anapotaka kupata mimba tu ndipo atakuwa huru kwa mumewe na akipata mimba tu shida iko pale pale.Walibahatika kuzaa watoto watano. Hata kanisani kila mmoja huenda kivyake, hakuna kuandamana. Hili ni pigo la tatu.
Bwana huyu kwa kuwa ni mtu wa dini, akaamua kutafuta safari za mbali(ng`ambo) ambako alibahatika kupata masomo fulani.
Wakati fulani akarejea na kutaka mke na watoto awapeleke huko ng´ambo lakini mke akaweka vizingiti, ikashindikana.
Jambo lingine ambalo linamsumbua jamaa huyu ambalo laweza kuwa pigo la nne, ni kwamba mkewe huyo anaye mwanaume mwingine wanayefahamiana naye tangu chuoni lakini hajamuacha. Japokuwa mwanaume huyo naye ameoa na familia yake, lakini wanapokutana na mwanamke huyu wanaheshimiana mno.
Mwanamke huongea kwa adabu kubwa mno utafikiri ndiye mume wake, huonyesha heshima ya hali ya juu ambayo hajawahi kuionyesha kwa mumewe.
Jambo hili linamuua sana mumewe. Baba huyu aliyeghubikwa na misukosuko anauliza, je, nifanye nini?
Huku ulaya niliko nina amani ambayo sijawahi kuipata maishani mwangu, sijawa tajiri lakini nina amani tele. Sasa nifanye nini?
Maana mke huyu pamoja na kuwa mbali bado akipiga simu wanagombana katika simu vibaya sana.
Naomba Anti Flora, uliza wasomaji wako wote popote walipo watoe maoni yao na yako
Wako Sifa David. Hivi ndivyo inavyomalizika email yake.
Mpenzi msomaji, bila shaka umempata vema jamaa yetu huyu aliyedhani kapata mke, kumbe amepatikana. Kila kukicha ni purukshani zisizoisha.
Binafsi, kosa moja kubwa ninaloliona kwake ni kule kukurupuka na kuoa mwanamke ambaye hakumfanyia utafiti wa kutosha kujua tabia yake.
Hata pale bibie yule alipomtaarifu juu ya maisha yake ya kuolewa mara kadhaa na hata kujiingiza katika ukahaba, bado hakughairi.
Si unajua tena msemo ile, sikio la kufa halisikii dawa? au inzi kufia kidondani ni halali. Sasa matokeo yake ndiyo hayo ya kukaliwa utosini kama mzigo usiobanduka.
Na hakika, maji ukiyavulia nguo, sharti uyaoge. Jamaa hana ujanja, kang`ang`ania mke anayempenda, kaona, sasa yanamtokea puani. Chunguza kabla hujajitosa mzee.
Wanawake wengine ni wajanja sana. Wapo wanaotaka waolewe na mtu fulani kwa sababu fulani fulani. Pengine ni tajiri sana, au ni mpole sana ili akamkandamize ndani ya himaya yake au ili kusafisha aibu fulani aliyotenda huko nyuma.
Kwa msingi huu, wanawake katika makundi haya, aghalabu huficha makucha hujifanya watakatifu ili tu kumpumbaza mwanaume.
Akishaingia mtegoni ndipo hufungua makucha na kuonyesha sura zote kama yaliyomkuta mwenzetu katika email niliyodokeza hivi punde.
Mpenzi msomaji, nisimalize uhondo peke yangu. Kama mtuma kisa hiki alivyoniomba, hebu nawe toa maoni yako au ushauri kumsaidia jamaa yetu huyo anayeungua ndani ya nyumba yake mwenyewe lakini anajikaza kisabuni.
Hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.
Wasalaam.
Email: fwingia@yahoo.com
- SOURCE: Nipashe
No comments:
Post a Comment