Atarudi Marekani karibuni
KUNA vitu ambavyo vinalingana na vile ambavyo havilingani. Kuna matukio ambayo yanafanana na yale ambayo hayafanani. Kuna watu wanaofanana na wale ambao hawafanani. Kuna wanaofanana kwa sababu ya undugu wa damu (mapacha n.k) na wale ambao wanafanana kutokana na sababu za kinasibu tu.
Kwa upande wa binadamu, hata hivyo, hata wale wanaofanana utakuta wanatofautiana kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, kuna wakati ambapo kufanana kwa watu fulani kunatusukuma kujenga hoja mbalimbali kuhusu watu hao licha ya kujali tofauti walizonazo.
Mfano mzuri ni kumlinganisha Mahatma Gandhi na Dk. Martin Luther King Jr. Watu hawa wanatofautiana sana katika mazingira ya jiografia waliyoishi, na ingawa ni watu wa nyakati moja walitofautiana kinasaba na kihistoria.
Hata hivyo, utaona kuwa wanalingana katika mambo ya msingi kama vile wote wawili walipigania haki za watu wao kwa kutumia njia zisizo na matumizi ya nguvu, na wote wawili walijenga hoja ya watu wao kupata heshima na hadhi ya kutambuliwa utu wao.Wote walikataa uonevu wa mwanadamu mmoja kwa mwingine na hatima ya wote wawili ni kuwa walikufa kutokana na vitendo vya mahasidi wao.
RAIS Jakaya Kikwete |
Ni katika kutafakari kulingana kwa watu, matukio na mambo mbalimbali nilijikuta nikimuangalia Rais Jakaya Kikwete na kujaribu kutafuta mtu wa kihistoria ambaye anafanana naye kimsingi. Baada ya kuangalia kwa muda mrefu nimejikuta na mtu mmoja ambaye sisi watu wa Afrika ya Mashariki tunalijua jina lake vizuri kwani mtu huyo amepitia katika maeneo yetu karibu miaka mia tano iliyopita. Huyu si mwingine bali ni msafiri, mwanasiasa na mvumbuzi wa Kireno, Vasco Da Gama.
Ndiye huyo ambaye historia inamrekodi aliyeweza kuonesha njia ya kutoka Ulaya kwenda India kuzunguka kusini mwa Afrika. Rais wetu Jakaya Kikwete anafanana sana na Vasco da Gama na ni kufanana huko ambako leo kunanituma kuangalia safari za Rais Kikwete nje ya nchi, safari ambazo kwa hakika siyo tu zimekuwa za uvumbuzi bali ni za utambuzi, ugunduzi na kwa hakika zimekuwa ni safari za mwanasiasa, mwanadiplomasia na za kiongozi.
Mwanzoni mwa utawala wake na mara alipoanza safari hizi za kwenda nje ya nchi, tuliambiwa kuwa Rais wetu anafanya hivyo ili kujitambulisha kwa viongozi wa nchi za kigeni kuwa yeye ndiye “Rais mpya wa Tanzania”. Wengi tulikubali dhana hiyo bila kuihoji kwa undani kwa sababu tuliamini kabisa kuwa mataifa ya kigeni hayakufuatilia uchaguzi wa Tanzania na kwa hakika hawakujua Rais mpya wa Tanzania ni nani.
Na kwa vile Rais Kikwete alitaka atambulike hivyo ilibidi aende yeye “mwenyewe” kuwaonesha sura yake na tabasamu lake la kukata na shoka. Hivyo safari zake za mwanzo kwenye nchi jirani zilikuwa na lengo la kujitambulisha. Hivyo ndivyo tulivyoambiwa. Miaka miwili baadaye safari za Rais Kikwete na wapambe wake zimezidi kupamba moto bila kukoma. Hivi karibuni Rais Kikwete ataondoka tena kwa ziara ya siku kadhaa huko Marekani.
Kati ya vitu ambavyo tunaambiwa kuwa Rais Kikwete anaenda kufanya ni kutangaza rasmi ujio wa Mkutano wa Kimataifa wa Taasisi ya Sullivan ambao utafanyika nchini mwakani. Kinachoshangaza sisi ambao ni wachunguzi wa mambo ya kisiasa nchini ni ulazima wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kutuutangazia ulimwengu ujio wa mkutano huo nchini.
Hivi ni kweli kuna ulazima wa Rais kwenda kufanya jambo hilo na hakuna kiongozi mwingine anayeweza kumuwakilisha kwenye tukio hilo? Imepangwa kuwa katika hafla hiyo Rais Kikwete atatumbuizwa na kundi la muziki lililotamba mwanzoni mwa miaka ya tisini la Boyz II Men.
Endapo tumefikia mahali kuwa Rais wetu ni lazima aende kwenye vihafla hivi na vimkutano hivi, kwa kweli kuna jambo moja tu ambalo ni dhahiri; nalo ni kwamba Rais Kikwete anapenda kusafiri sana, na safari zake hizi za uvumbuzi na utambuzi zimeanza kukaribia zile za yule msafiri wa Kireno, Bw. Da Gama.
Hata hivyo, watetezi wa safari hizi na makada wa chama tawala wanatuambia kuwa safari hizi siyo za utambuzi tu bali pia ni safari zenye “maslahi makubwa kwa Taifa”. Wanapotetea safari hizi makada hawa wanajaribu kutushawishi tuamini kuwa pasipo Rais Kikwete kwenda huko anakokwenda (iwe Uarabuni, Marekani au Ulaya), basi, misaada hiyo na uwekezaji huo hautakuja.
Mfano mzuri unaotolewa ni ahadi ya kutoka Shirika la Changamoto ya Milenia ambapo tumeambiwa kuwa Tanzania itapata karibu dola nusu bilioni miaka michache ijayo. Ilipotangazwa habari hii miezi michache iliyopita, Rais Kikwete alikuwa Marekani na waliopiga baragumu la ushindi wakatuambia kuwa (japo si kwa maneno hayo moja kwa moja) kuwa tumepata msaada huo toka Marekani kwa sababu Rais Kikwete alikwenda huko.
Kitu ambacho hawakutuambia ni kuwa Tanzania haikuwa nchi peke yake iliyopewa ahadi kama hiyo baada ya kutimiza vigezo fulani fulani. Lesotho, nchi yenye watu milioni 2.3 (chini ya idadi ya watu wa Jiji la Dar), imepewa msaada kama wa kwetu wa dola milioni 362), Mongolia, yenye watu kama milioni 3 hivi, na wenyewe walipata msaada kama wa kwetu wa dola milioni 285 na El Salvador, yenye watu karibu milioni sita, wao wamepewa msaada huo toka kwenye akaunti ya Changamoto ya Milenia wenye kiasi cha dola milioni 461.
Hivyo, kufikiri kuwa tulipata msaada huo kwa sababu ya Kikwete kwenda huko ni kujidanganya. Ukweli wa mambo ni kuwa kuna misaada tunayoipata ambayo inaweza kuja bila ya Rais Kikwete kwenda huko kuomba au kuonesha sura yake. Endapo tutaweza kutimiza masharti au malengo fulani fulani wahisani wataona na watasaidia kama wanataka.
Binafsi, naamini kabisa kuwa baadhi ya safari hizi na msururu mzima unaoandamana na Rais Kikwete kwenda nje ya nchi siyo za lazima na zinaweza kufanywa na kiongozi mwingine ye yote yule kama Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Mfano mzuri ni ziara iliyopita ya Makamu wa Rais huko Iran na Misri. Kwa nini Makamu wa Rais hapewi mojawapo ya hizi ziara za kwenda Marekani? Kwa nini Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano asiende kwenye mojawapo ya misafara hii?
Isitoshe, safari hizi ni gharama kubwa kwa walipa kodi masikini wa Tanzania. Kwa mfano, kwa mwaka jana peke yake, inakadiriwa kuwa ziara za Rais zilitumia karibu shilingi bilioni 20 (safari, posho, na masurufu mbalimbali). Mwaka huu peke yake sina uhakika, lakini kama kuna mtu atakuwa tayari kutuambia ziara za Rais na viongozi wa juu zimegharibu kiasi gani, tunaweza kupatwa na shinikizo la moyo.
Kwa wale wanaokumbuka, wakati wa kusainiwa mkataba wa Buzwagi kule London, Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Edward Lowassa wote walikuwa nje ya nchi. Msiniulize kwa nini?
Wapambe wanaofuatana na Rais kuanzia wasaidizi, maafisa usalama na wengine kadhaa wanalipwa posho za safari. Na niwahakikishie hizo posho hazilipwi kwa hela ya madafu. Baadhi yao ambao tumepata nafasi ya kugongana nao kwenye mitaa ya New York na Washington DC, na wale ambao tuliweza kupiga nao soga pale London, walikuwa na hela utadhani Bill Gates. Baadhi yao walipotualika hotelini kwao walikuwa wanachomoa toka kwenye mifuko yao “tudola” utadhani wameziokota.
Hawana uchungu nazo na hawana wasiwasi wa matumizi yake. Kuna wengine kwa uwezo walionao (na ni maafisa wa chini) ambao hutumia nafasi hizi za safari kufanya “shopping za nguvu”. Nakumbuka mmoja wao alichepukia pembeni kidogo kuja kuangalia kama anaweza kujipatia “ka-usafiri” ka-Hammer II au Cadillac ambako “hakakuwa” ka bei ndogo. Huyo ndugu alikuwa anafanyia kazi “kabajeti kake” ka dola elfu chache. Sasa sijui kama alikuwa anatania au alikuwa “very serious”.
Wasafari wanaoambatana na Rais kwa hakika ni lazima na wenyewe “waambulie” kidogo. Mojawapo ya safari zake Rais Kikwete aliambatana na watu karibu 30 (sina uhakika msafara wa kawaida huwa na maafisa wa ngapi), lakini kwa Rais wa nchi ya daraja la tatu, na ambayo licha ya kelele za viongozi wake bado haijaanza kupaa, inasikitisha kuwa tunatumia fedha nyingi katika misafara hii. Nina uhakika kabisa endapo safari za viongozi wote kwenda nje ya nchi zikifanyiwa hesabu bila ya shaka jumla yake itatushangaza.
Sitoshangaa kabisa kuwa tukijumlisha fedha zilizotumika katika safari za Rais, Makamu, Waziri Mkuu na Mawaziri wengine kwenda nje ya nchi kwa miaka iliyopita, madarasa mengi tu ya shule za sekondari na zahanati vingejengwa, na wananchi husika wasingelazimika kuchangia!
Leo hii tunahangaika kuchangisha fedha za kujenga madarasa jijini Dar-es-Salaam. Hivi safari moja ya Rais inaweza kujenga madarasa mangapi? Je msafara mmoja wa Makamu wa Rais au Waziri Mkuu unaweza kusaidia kujenga vyoo vingapi vyenye maji katika shule ya Azania? Je ile misafara ya watetezi wa bajeti walioenda mikoani ingeweza kuweka mapaa mazuri na kununua vifaa vingapi vya zahanati?
Binafsi, naamini kabisa tunaweza kupima mafanikio ya ziara hizo kwa kuangalia hesabu nyepesi. Endapo misaada ambayo tumeahidiwa katika ziara za viongozi wetu pamoja na uwekezaji ambao umefuatia ziara hizo unazidi kwa kiasi kikubwa gharama za kuwasafirisha kina Vasco da Gama wa kileo, basi, taifa linakuwa limepata faida.
Hata hivyo endapo misaada hiyo na uwekezaji huo hauzidi gharama zilizotumika kuitafutia, basi, Watanzania hatunufaikinazo. Na hapa sizungumzii misaada na ahadi zote, ila ile tu ambayo “bila ya ziara za viongozi” isingewezekana.
Leo hii kuwaaimbia wimbo wa uwekezaji Wamarekani na Waingereza ni kama kurudia kibwagizo kile kile kwa kwaya yako. Wamarekani wangekuwa wanavutiwa na Tanzania wangeshaanza kuwekeza muda mrefu uliopita. Siyo kwa sababu hawajui; ni kwa sababu Tanzania haina maslahi makubwa kwa Wamarekani.
Urafiki na Marekani kimsingi unatokana na maslahi na hata wanapommwagia sifa rais wetu na kumpamba kwa pambio na maua tujue kuwa wanafanya hivyo kwa sababu moja tu; Rais wetu anakidhi maslahi yao katika eneo la Afrika ya Mashariki na hasa katika maslahi ya Marekani ulimwenguni.
Kitu ambacho mimi, na bila ya shaka wachambuzi wengine, tumeanza kukiona ni kuwa Marekani inaanza kuvutiwa na Tanzania siyo kwa sababu za kiuchumi hasa bali kwa sababu za kiusalama. Ndio maana wapo wale ambao tunaamini kuwa ziara hii ya Rais Kikwete Marekani inahusiana kabisa na maslahi ya kiusalama ya Marekani. Siamini hata kidogo kuwa Rais wetu anafunga safari kwenda Marekani kusimama kwenye kipaza sauti kutangaza mkutano wa Sullivan na kurudi!
Ni matumaini ya Watanzania kuwa mwaka ujao Rais Kikwete atautumia kukaa nyumbani na watu wake na ataanza kuwaamini viongozi wengine kuwa wanaweza kumwakilisha nje ya nchi vizuri kabisa. Watanzania watapata moyo mkubwa endapo Rais Kikwete ataweza kukaa nchini kwa miezi mitatu mfululizo.
Rais Kikwete na timu yake hawana budi kukaa chini na kuamua kwa umakini mkubwa ni safari gani za msingi na za lazima ambazo zinamuhitaji Rais. Vinginevyo, Rais wetu ataonekana ni Rais msafiri hasa ukimlinganisha na marais jirani zetu. Inakuwaje watu kama kina Kibaki, Kagame, Museveni, Kabila na wengine majirani wanakaa nchini mwao na wanaenda mara moja moja huko ng’ambo, isipokuwa wa kwetu?
Nafahamu kuwa serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa Rais hafanyi kazi kwa shinikizo la mtu yeyote. Ukweli ni kuwa isingekuwa wahisani kumpa shinikizo au kuweka shinikizo kwa serikali yetu kuna mambo ambayo yasingefanyika. Uchunguzi wa Richmond, BoT, na mikataba haukutokana na shinikizo la wapinzani kama wao wanavyopenda kudhania. Serikali ya CCM haioni tishio lolote la msingi toka vyama vya upinzani, tishio pekee ambalo CCM wanalihofia ni kutoka kwa wahisani.
Wahisani wakitaka Rada ichunguzwe itachunguzwa na wakitaka Richmond ichunguzwe itachunguzwa. Na ni wahisani ambao wakitaka sheria ya rushwa ipitishwe itapitishwa na nina uhakika kama wakitaka Katiba yetu ifanyiwe marekebisho ya msingi itarekebishwa. Sasa tusifike mahali wahisani wakamwambia Rais wetu apunguze safari za nje!
lulawanzela@yahoo.co.uk
Kutoka Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment