Wednesday, December 19, 2007


Matokeo darasa la saba 2007:

Kiingereza na Hisabati ngumu

*Waliofaulu wapungua kuliko mwaka jana
*Mtihani wa Kiswahili waonewa na wengi
*200 wasitishiwa matokeo, 800 wafutiwa
*Watahiniwa Dar es Salaam mbendembende
*Pwani, Dodoma, Shinyanga, Singida oyee

Na Rehema Mohamed

KIWANGO cha kufaulu kwa wahitimu wa mtihani wa darasa la saba mwaka huu, kimeshuka kwa asilimia 16.3 ikilinganishwa na mwaka jana, huku masomo ya Hisabati na Kiingereza yakiongoza kwa kuvurundwa.

Matokeo hayo pia yanaonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kufanya vibaya huku mikoa ya Pwani, Dodoma, Shinyanga na Singida, ikiongoza kwa kufaulu.

Akitangaza matokeo hayo Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bibi Margaret Sitta, alisema matokeo hayo ni ya wanafunzi 773,550 sawa na asilimia 97.41 waliofanya mtihani, kati ya 794,102 walioandikishwa, ambapo watahiniwa 20,552 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali.

Bibi Sitta alisema jumla ya watahiniwa 419,198 sawa na asilimia 54.18 ya watahiniwa wote, walifaulu wakiwamo wasichana 170,844 sawa na asilimia 45.39, huku wavulana wakiwa 248,354 sawa na asilimia 62.52. Matokeo hayo yanaonesha kuwa mwaka huu, wavulana wameongoza kuliko wasichana.

Jumla ya watahiniwa 354,405 hawakufaulu mitihani hiyo wakiwamo wasichana 205,618 sawa na asilimia 54.61 na wavulana 148,787 sawa na asilimia 37.48 ya waliopewa matokeo yao, ikilinganishwa na mwaka jana ambapo wanafunzi 468,187 sawa na asilimia 70.48 walifaulu.

Pia jumla ya watahiniwa 209 waliofanya mitihani hiyo wakiwamo wasichana 93 sawa na asilimia 44.5 na wavulana 116 sawa na asilimia 55.5, wamesitishiwa matokeo yao huku watahiniwa 878 wakifutiwa wakiwamo wavulana 455 sawa na asilimia 51.82 na wasichana 423 sawa na asilimia 48.18 kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya udanganyifu katika mitihani.

Akizungumzia ufaulu wa kimasomo, Bibi Sitta alisema somo linaloongoza ni Kiswahili ambalo wastani wake wa kufaulu ni asilimia 80.23, likifuatiwa na Sayansi asilimia 66.66, Maarifa asilimia 56.39, Kiingereza asilimia 31.31 huku Hisabati ikiwa na asilimia 17.42.

"Wizara itafanya tathmini ya kubaini maeneo ya masomo ambayo watahiniwa hawakufanya vizuri, ili hatua za kuboresha ufundishaji zichukuliwe, mfano somo la Kiingereza ambalo mwaka jana wastani wake wa kufaulu ulikuwa asilimia 47.6 huku Hisabati ikiwa asilimia 45.84," alisema Bibi Sitta.

Akizungumzia matokeo ya wanafunzi wenye ulemavu, Bibi Sitta alisema kati ya 301 waliofanya mitihani, wakiwamo wasichana 1,153 sawa na asilimia 50.83 na wavulana 148 sawa na asilimia 49.17, waliofaulu ni 212 sawa na asilimia 70.43 wakiwamo wasichana 103 sawa na asilimia 67.32 na wavulana 109 sawa na asilimia 73.65

Alisema idadi hiyo ni sawa na ongezeko la wanafunzi 96 ikilinganishwa na mwaka jana, ambapo wanafunzi 205 walifanya mitihani.

Bibi Sitta alisema kuwa kwa matokeo hayo wanafunzi waliobahatika kujiunga na kidato cha kwanza mwakani katika shule za Serikali, ni 378,506 sawa na asilimia 90.29 wakiwamo wasichana 159,543 sawa na asilimia 93.39 na wavulana 218,963 sawa na asilimia 88.17 kati ya wanafunzi 419,198 waliofaulu.

"Ukiangalia utaona kuna baadhi ya wanafunzi wamekosa nafasi za kuingia kidato cha kwanza ingawa wamefaulu, hii ni kutokana na kila mkoa kuchagua idadi ya wanafunzi wanaoweza kuwachukua na ndiyo maana Serikali ilikuwa inahimiza ujenzi wa madarasa kwa shule za sekondari kwa kila kata," alisema.

Alisema wanafunzi walioachwa wanaweza kuchaguliwa katika awamu ya pili, hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kujenga madarasa, ili wanafunzi hao waweze kujiunga na kupata elimu ya sekondari.

Akizungumzia kushuka kwa ufaulu, Bibi Sitta alisema hajui kilichosababisha hali hiyo lakini alieleza kwamba inawezekana suala hilo limechangiwa na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wizara katika kusimamia vyema mitihani hiyo na kudhibiti udanganyifu.

"Ni heri kuwa na matokeo kama haya kuliko kuwa na mazuri yaliyojaa udanganyifu, Wizara kwa kushirikiana na maofisa elimu na walimu wakuu wote nchini, tutapanga mikakati ya kuweka juhudi ili kiwango hicho kiongezeke lakini si kwa udanganyifu," aliahidi.

Waziri Sitta alisema umefika wakati kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, kushirikiana na uongozi wa shule kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa, wanahudhuria masomo na kubaki shuleni hadi watakapohitimu elimu ya sekondari.

Waziri Sitta alisema umefika wakati kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, kushirikiana na uongozi wa shule kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa, wanahudhuria masomo na kubaki shuleni hadi watakapohitimu elimu ya sekondari.
Habari zingine kuhusu matokeo ya darasa la saba mwaka huu:

No comments: