Wednesday, December 19, 2007

SHAFI ADAM SHAFI


Ni vigumu, nasema ni vigumu.Haiwezekani.Huwezi kuizungumzia fani ya uandishi wa fasihi (literature) nchini Tanzania na usimzungumzie Shafi Adam Shafi (pichani) na bado ukaeleweka unazungumzia nini. Huyu si tu mwandishi, bali hazina ya historia ya nchi yetu, mila na tamaduni zetu, uandishi wa riwaya uliobobea. Ingawa kitabu chake cha KULI ndicho ambacho wengi wanakitambua zaidi( ni mojawapo ya vitabu vinavyofundishiwa mashuleni kwenye somo la Kiswahili), Shafi anavyo vitabu vingine kama vile Kasri ya Mwinyi Fuad (ambacho kimetafsiriwa kwa Kifaransa, Kijerumani na Kirusi); Vuta n’kuvute (ambacho kilimpatia tuzo ya mwandishi bora nchini Tanzania mwaka 1998) na Haini ambacho ni cha hivi karibuni zaidi. Vitabu vyote vya Shafi ni riwaya.

Hivi majuzi alikutana na mwandishi mwingine mahiri, Freddy Macha, huko Milton Keynes nchini Uingereza. Waliketi kitako kwa zaidi ya masaa manne.Waliteta,wakazoza,wakapeana historia,wakapashana habari.Wakachambua umuhimu wa waandishi na wasanii. Lakini kabla hatujakuambia pa kwenda ili usome alichoandika Freddy Macha kuhusu “mkutano” wao, hii hapa historia fupi ya gwiji huyu wa fasihi.

Adam Shafi alizaliwa mjini Zanzibar mwaka 1940. Baada ya elimu yake ya shule ya msingi alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Seyyid Khalifa (sasa Chuo cha Ualimu cha Nkrumah) mwaka 1957 hadi mwaka 1960. Alipata Diploma juu katika fani ya Siasa ya Uchumi katika Chuo cha Fritz Heckert, katika iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani mwaka 1963. Alipata mafunzo ya uandishi wa habari mjini Prague, nchini Czechoslovakia (sasa Jamhuri ya Czech) mwaka 1964 hadi mwaka 1965, nchini Sweden mwaka 1982 na nchini Marekani mwaka 1983.

Adam Shafi alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA) kuanzia 1998 hadi 2002. Alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la maendeleo ya Vitabu Tanzania (BAMVITA) mwaka 2002.

Haya twende sasa. Bonyeza hapa ili usome alichokiandika Freddy Macha kuhusiana na mkutano wake na Shafi Adam Shafi. Mahojiano yetu na Freddy Macha mwenyewe yatawajieni hivi karibuni.Hutaki kuyakosa mahojiano hayo!

Picha kwa hisani ya Freddy Macha.

Historia ya Shafi kwa msaada wa Longhorn Publishers.

Hizi habari toka Bongo Celebrity.

No comments: