Maggid Mjengwa
INAHUSU namna tunavyofikiri. Ni saikolojia. Kuna kisa cha timu moja ya soka mkoani Iringa. Kama ilivyo hulka ya klabu nyingi za soka nchini, timu hiyo iliyokuwa ikicheza ligi daraja la kwanza ilitumia muda na rasilimali zake nyingi katika kuendekeza imani za ushirikina.
Nje kidogo ya mji wa Iringa kuna sehemu inaitwa Tanangozi. Hapo ilisemekana kulikuwa na mganga mahiri wa kienyeji.
Viongozi wa timu ile walikwenda na kikosi kizima kumwomba mganga huyo awasaidie kwa mechi yao muhimu siku mbili zilizofuatia.
Mganga yule alisikiliza maelezo ya viongozi wale wa soka. Aliwaangalia wachezaji wale vijana. Akawaambia, kuwa uganga wake kwao ni kwa wao kurudi kambini.
Huko kambini wale, wanywe maji mengi, walale sana, wafanye mazoezi na kurudia " dozi" hiyo. Mganga yule hakutaka malipo yoyote kwa kazi yake hiyo.
Siku ya mechi ikafika. Vijana wale walicheza vizuri sana kuliko hata ilivyokuwa kawaida yao, wakapata ushindi mkubwa wa mabao 5-0.
Baada ya ushindi ule mkubwa, viongozi wale hawakukanyaga tena kwa mganga yule wa Tanangozi. Naam! Hawakumpenda mganga yule kwa vile hakuhitaji chochote kwa uganga wake.
Kwa vongozi wale, mganga asiyetaka pesa ina maana ya kuwa mganga huyo naye anawakosesha pesa viongozi hao. Maana, walikuwa na mazoea ya kwenda kwa wafadhili wa klabu kuomba michango ya kusaidia ‘Kamati ya Ufundi’.
Hivyo basi, hawakumpenda mganga aliyewaletea ushindi usio na maslahi kwao viongozi wa klabu.
Kisa hicho nilichosimulia ni kielelezo ya jinsi baadhi yetu tunavyofikiri. Na labda ni kielelezo cha ugonjwa unaoliathiri taifa letu kwa miaka mingi sasa.
Ni ugonjwa wenye kuambukiza. Ni ugonjwa wa kutelekeza, sio tu rasilimali za umma, bali hata fikra zenye maslahi kwa umma. Ni ugonjwa unaotokana na watu kuendekeza ubinafsi, tamaa ya mali na kujipendelea.
Mathalan, katika idara na taasisi nyingi za umma utakuta vifaa kama magari yametelekezwa.
Hakuna anayejali. Imefika mahala, kwa makusudi kabisa, kiongozi wa idara anatelekeza gari ya umma.
Yuko tayari aliweke gari juu ya mawe likiwa katika hali nzuri kabisa. Anafanya hivyo ili kujihalalishia yeye (kiongozi) kununua gari hilo kwa bei ya kutupa.
Sababu zitakazotolewa ni kuwa serikali haina fedha za kugharamia matengenezo, hivyo basi, imemwuzia mtumishi wake gari hilo ‘mkweche’!
Ni katika staili hiyo hiyo, kama nchi, tumekubali kuwa na viongozi walioshindwa kusimamia vema mashirika yetu ya umma. Mali za umma tukaacha zikitelekezwa.
Hata kama ilitokea kuwapo kwa Watanzania waliokuwa tayari kujitolea bure kusaidia kuyaokoa mashirika ya umma. Watanzania hao hawakupewa nafasi hiyo.
Ni kama ilivyokuwa kwa mganga yule wa Tanangozi, Iringa, msaada wao haukuwa na maslahi kwa waliosimamia mali hiyo ya umma.
Mifano ni mingi. Tumeona jinsi watumishi wa umma walivyoshindwa kusimamia nyumba za serikali. Wakazitelekeza, kisha wakapata sababu ya kufanya hila ya kuzinunua nyumba hizo kwa bei ya kutupa.
Nyumba zile za umma walizoshindwa kuzisimamia ikiwemo kuzifanyia ukarabati sasa wamezigeuza kuwa mahekalu ya kutisha baada ya kuzitia kwa hila kwenye miliki yao.
WATU kutoka India ambao walikuwa wanyapara wakati wa ujenzi wa reli yetu, leo wamekuwa wamiliki kwa sababu wenyewe tumeshindwa. |
Majuzi hapa tumesikia habari na kuona picha za magazetini kuhusu kuanza tena kwa safari za Reli ya Kati. Shughuli za uendeshaji wa shirika hilo wamekabidhiwa kampuni kutoka India.
Ikaandikwa magazetini; " Safari ya kwanza ya reli ya kati yaanza". Habari ile iliambatana na picha za Watanzania wenye nyuso za furaha.
Tukio lile linaacha tafsiri nyingi. Kwa wengi wetu lile haliwezi kuwa tukio la furaha. Hakika ni tukio la huzuni kubwa. Baada ya miaka 46 ya Uhuru wetu Reli yetu ya kati sasa inaendeshwa na kampuni ya Wahindi wenye takribani asilimia 50 ya umiliki.
Jambo hilo haliwezi kuwa ni jambo la kujivunia hata kidogo. Ni fedheha. Ikumbukwe, kuwa Wahindi wengi waliletwa na Waingereza Afrika Mashariki kuja kufanya kazi ya unyapara kwenye ujenzi wa reli.
Leo wamekuja kumiliki reli yetu. Naam. Nyapara amegeuka mmiliki! Na katika hali ya sasa, hakika baadhi ya Wahindi hawa waliokuwa manyapara wa Wakoloni wamerudia tena kazi yao ya zamani ya unyapara. Kazi ya kutusimamia sisi.
Makampuni mengi ya kigeni katika nchi zetu yanamilikiwa na raia wa mataifa yaliyotutawala huko nyuma. Wageni hawa wakija huku kwetu wanaajiri raia wa Kihindi kuja kusimamia vitega uchumi vyao.
Kuja kufanya kazi za nyapara. Kuja kutusimamia kama walivyosimamiwa babu zetu wakati wa ujenzi wa "Reli ya Mkoloni".
Tukirudi kwa ndugu zetu hawa Wahindi, nao pia walitawaliwa na Mwingereza. Lakini, uzalendo na uchungu kwa nchi yao umewafanya nao waanze kuwa na " Vikoloni" vyao hapa duniani.
Hakika, siri kubwa ya mafanikio ya India ni uzalendo na uchungu kwa taifa lao. Wahindi wanajivunia India yao. Mathalan, Rais George Bush alipotembelea India msafara wake ulikuwa ni wa magari yaliyotengenezwa India tu.
Katika nchi zetu za Kiafrika viongozi wanaona fahari kuendeshwa ama kuendesha magari yaliyotengenezwa Marekani, Ungereza na Japan.
Ni yale magari ya kifahari na ya gharama kubwa.Wahenga walinena: Mvunja nchi ni mwananchi na kinyume chake.
Inasemekana kampuni ya Kihindi inapopewa zabuni ya kujenga daraja na serikali yao.
Basi, Mhindi mwenye kampuni atahakikisha kuwa asilimia kumi ya fedha hizo inaingia mfukoni mwake, lakini asilimia tisini ya fedha itajenga daraja.
Mhindi hapo anaiangalia India kwanza, na si maslahi yake. Anajivunia India yake na anataka iwe na madaraja mazuri na imara kushinda ya nchi jirani ya Pakistan. Lakini mpe zabuni Mtanzania ajenge daraja.
Mkandarasi wa Kitanzania atahakikisha anaajiri ndugu zake na vibarua anaowalipa ujira wa kukatisha tamaa. Atahakikisha pia mifuko ya sementi ya kujengea daraja hilo itoshe pia kumalizia au kujenga nyumba mpya ya wageni.
Ni nyumba yake binafsi. Hajali, hata kama wageni wake wanapita kwenye barabara yenye mashimo na daraja bovu ili mradi tu amejijengea nyumba murua na ya kisasa.
Na labda hapo ndipo ilipo tofauti kubwa ya kifikra na kimtazamo baina ya Mhindi na Mtanzania. Mhindi anaiangalia India kwanza wakati Mtanzania anajiangalia yeye kwanza.
Huko nyuma hata sisi tulianza vizuri. Kulikuwa na maadili ya kiutendaji yaliyokuwa yakifuatwa. Waliokiuka waliadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Ikafika mahala tukatoka nje ya reli. Tukaruhusu wahalifu wafanye uhalifu wao wa kutelekeza na kuhujumu mali za umma mchana wa jua kali.
Ikumbukwe, kati ya mifano mingi. Huko nyuma tulikuwa na ATC- Shirika letu la Ndege. Tunaambiwa wajanja wachache wakawa wanatengeneza tiketi za kusafiria katika nchi ya Uingereza.
Tuliona ndege za ATC zikijaa na abiria kubaki. Kumbe! Abiria wote wale walikata tiketi za "wajanja". ATC ikafilisika. Shirika letu la Reli, TRC, huenda nalo imefikwa na yale yalioikumba ATC.
Leo tuna wanaotaka kupigiwa kura kwa kuahidi " kufufua na kufufua hiki na kile". Hakuna anayewaahidi wapiga kura kuwa anataka madaraka ili akawashughulikie " wauaji".
Na waliotelekeza na kuyaua mashirika yetu wengi bado wapo hai. Yawezekana kabisa, kuwa baadhi yao walikuwepo kushuhudia " Safari ya kwanza ya treni ya Reli ya Kati".
Huenda pia ni kweli, kuwa ni safari ya kwanza. Maana, safari zote za huko nyuma zilikuwa "safari hewa!". Yawezekana sehemu kubwa ya pesa za mauzo ya tiketi ziliishia mifukoni mwa wajanja.
Hakika haya ni maradhi kwetu; tunaugua ugonjwa wa kutelekeza mali zetu wenyewe.
0754 678 252
mjengwamaggid@gmail.com
http://mjengwa.blogspot.com
No comments:
Post a Comment