Friday, December 14, 2007

FIKRA MBADALA


Waafrika na ‘Mashkolo Magenyi’

Ayub Rioba

BADO naendeleza mjadala kuhusu chanzo cha matatizo yetu sisi Waafrika, hasa watu weusi. Nilisema leo hii tunaishi maisha ambayo tukiletewa chochote kigeni tunakipokea na kukitukuza.

Tunalamba miguu na nyayo za wageni. Tunaishi kwa sera zao, tamaduni zao, mila zao, imani zao, lugha zao, majina yao na vitu vitu vyao.

Wiki iliyopita, kwa mfano, nchi yetu imetimiza miaka 46 ya uhuru huku asilimia 46 ya bajeti ya taifa ikiwa inatoka kwa wahisani! Wakati sisi tukisherehekea uhuru, wahisani nao pia wanasherehekea zaidi kutokana na jinsi wanavyoendelea kuvuna yale waliyokuwa wakiyavuna wakati wa utumwa na vile vile wakati wa ukoloni kabla hatujawatimua.

Wakati tunasherehekea uhuru asilimia 40 ya utajiri wa mali na fedha kutoka Afrika imefichwa na viongozi waroho na washirika wao mafisadi huko ng’ambo.

Kana kwamba hii 40 ni namba yenye nuksi kwa Afrika, asilimia 40 ya mazao yanayovunwa mashambani kwetu hupotea wakati wa kuvuna, kusafirisha na kuhifadhi.

Hivyo miaka 46 baada ya uhuru, kwa mfano, bado tunapoteza asilimia 40 ya chakula tunacholima wenyewe kwa shida kwa sababu tu tunakosa kuwekeza katika umakini miongoni mwa wakulima wetu.

Miaka 46 baada ya uhuru wetu bado katika kila akina mama 100 wanaokwenda kujifungua ni lazima mmoja atafariki dunia kabla ya kukiona kichanga chake.

Na vivyo hivyo katika kila watoto 10 wanaozaliwa leo, kati ya mmoja na wawili hawatahudhuria sherehe ya kutimiza miaka mitano ya kuzaliwa kwao. Wanakuwa tayari kaburini.

Lakini viongozi wetu wakiumwa mafua kidogo watapelekwa kutizamwa ng’ambo kwa gharama kubwa. Na hili limekuwa ni mazoea.

Miaka 46 ya uhuru bado ndiyo kwanza tunatangaza kwamba nchi yetu imefanikiwa kuhakikisha kwamba asilimia 87 ya watu wake wanakwenda kujisaidia vyooni.

Miaka 46 ya uhuru, balozi wa Japan anakaa na Katibu Mkuu wa Wizara yetu wakitiliana saini makubaliano ambapo Tanzania itasaidiwa shilingi milioni 200 kutengenezea kituo cha umeme kidogo Oysterbay! Hiyo ni thamani ya Toyota Landcruiser VX mbili!

Juma lililopita nilizungumzia ujio wa wafanyabiashara wa kiarabu na jinsi baadaye babu zetu walivyojikuta wakijikana na kuanza kuvaa utamaduni mpya, ilhali wakiamini kwamba maisha yao hapo awali yalikuwa gizani.

Nikaeleza pia jinsi walivyokuja wazungu na kufanya kama walivyofanya waliowatangulia. Ni vyema nieleweke kwa wasomaji kwamba sijaribu kupotosha historia kwa kutokutambua ukweli kwamba walikuwapo babu zetu majasiri kweli kweli ambao walijitoa muhanga kwa ajili ya kukataa kutawaliwa.

Wapo babu zetu waliopigana kwelikweli wakiwa na silaha zao hafifu. Lakini walikuwa na dhamira inayoweza kulinganishwa na silaha za maangamizi (WMD).

Tatizo ni kwamba wasaliti wao walikuwa ni watu weusi pia. Walikuwapo watu weusi waliokuwa wepesi kujikana mara tu walipoona vitu vigeni.

Wasukuma huviita “Mashkolo Magenyi” Sifa hii ya usaliti tunaishuhudia hadi leo pale baadhi ya watu weusi wa leo wanapoamua kuwasaliti wenzao kwa sababu ya “Mashkolo Magenyi”. Afrika Kusini ya kibaguzi ilikuwa na wanajeshi na polisi weusi ambao walishiriki kuwatesa weusi wenzao kwa sababu tu wao walivalishwa “Mashkolo Magenyi” na makaburu!

Wakoloni wa mwanzo walifanikiwa kuwachota kisaikolojia watu weusi si kwa sababu hawakuwapo akina Mfalme Isike wa Tabora, Mfalme Mkwawa wa Iringa au Jemedari Kinjekitile Ngwale wa vita ya Maji Maji ambao walipandisha juu bendera ya jeuri ya Mwafrika; la hasha. Walifanikiwa kuwachota akili watu weusi kwa sababu wanafiki na wasaliti waliwageuka majasiri wao.

Wakoloni wa mwanzo wakafanikiwa kuwaambia babu zetu waache mila zao za kishenzi. Wakawazuia kuabudu mizimu. Wakawaambia wamgeukie Mungu wa Abrahamu na Yakobo.

Babu zetu wakamwacha Mungu wa Nswanzugwako na Kokushoborwa. Wakoloni wa mwanzo wakawazuia babu zetu hata kupiga zumari na ngoma ya ritungu kanisani.

Lakini wao wakaingiza gitaa lao kanisani likachezwa kama kawaida. Kana kwamba Mungu wa Abraham na Yakobo asingeweza kutambua mirindimo ya muziki uliotokana na teknolojia iliyotengeneza ritungu au zeze.

Wamissionari wakoloni wakatuambia majina ya Nswanzugwako na Kokushoborwa hayatamkiki.Kana kwamba Mungu wa Abrahamu na Yakobo angepata taabu kuyatamka majina yale kwani yalikuwa magumu kwelikweli.

Wakatupatia ya kwao. Wataalamu wanasema kile kitendo cha mtu kukubali kujikana kuanzia jina, imani, mila, desturi, staili ya maisha n.k. kina tabia ya kuzalisha binadamu asiye halisia. Kwa vile binadamu huyo si halisia basi hawezi kufikiri sawa sawa au kubuni njia za kutatua matatizo yake.

Mtu fotokopi huishia tu kuigiza na kuendelea kuwa tegemezi. Kisaikolojia, wanasema wataalamu, huyu mtu asiye halisia ni lazima atamtegemea yule aliyeamua kujibadilisha kumfuata.

Asiye halisia ni fotokopi tu. Fotokopi ni lazima ifuate ni nini kilikuwa katika original hata kama ni makosa. Wanamuziki wa Tanzania wanatambua ni nini maana ya kurekodi nyimbo halafu ukaambiwa umuuzie mtu ‘master’.

Ile master ndiyo halisia. Hizi zingine tunazonunua mtaani zinakuwa fotokopi. Bei ya master ni aghali mno. Wajapani sasa hivi wanatengeneza midoli ya robot ambayo inaweza kufagia nyumba, inaweza kuimba, inaweza kupiga kinanda n.k. lakini mwisho wa yote inabaki midoli tu.

Si imetengenezwa na Mjapani? Midoli hiyo itafanya kile alichotaka mtengenezaji wake ikifanye; itaimba wimbo iliyotengenezewa katika programu; itacheza = staili aliyoiprogramu mtengenezaji. Kwa kifupi, midoli ile haiwezi kufikiri nje ya kile alichotaka mtengenezaji.

Upo ukweli kwamba karibu kila jamii ya binadamu imeiga; kujifunza kutoka kwa wengine; au kutohoa mambo fulani fulani kutoka kwingine ili kuboresha kile walichokuwa nacho awali.

Ni Waafrika weusi tu ambao wamefanywa kuamini kwamba hawakuwa na chochote cha kuigwa na binadamu wengine walioonekana kuwa na akili zaidi.

Wiki ijayo nitajaribu, kwa maoni yangu, kuonyesha kwamba kuendelea kwetu kuuza malighafi ng’ambo kwa bei ndogo huku tukifakamia kila kinachotengenezwa ng’ambo, hata kama ni feki, ni matokeo ya kukosa uhalisia.


Niandikie: ayubrioba@hotmail.com

Kutoka Raia Mwema wiki hii.

No comments: