Halima Mlacha
HabariLeo; Monday,December 17, 2007 @00:09
HabariLeo; Monday,December 17, 2007 @00:09
MWANAFUNZI wa darasa la sita katika Shule ya Msingi ya Maarifa iliyopo Gongo la Mboto, Dar es Salaam, Zainabu Ibrahim (14), ameuawa kwa kile kinachoaminika kubakwa na watu wasiofahamika wakati alipohudhuria sherehe za ngoma ya kumtoa mwali mtaani kwao. Kwa mujibu wa majirani wa eneo ambako maiti ya binti huyo ilitelekezwa, mwili wa binti huyo ulionekana majira ya saa 11:30 alfajiri katika nyumba namba 594 Gongo la Mboto Mtaa wa Mazizini, ukiwa hauna nguo zaidi ya kipande kimoja cha kanga kilichokuwa kimetupwa pembeni. Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto Jack aliyeigundua maiti hiyo ambayo ilitupwa chini ya dirisha la nyumba hiyo mali ya mzee aliyejulikana kwa jina moja la Mkuchu, alisema hakuna kelele zozote zilizosikika usiku wa tukio zaidi ya mbwa wa jirani kubweka sana. “Sisi kwa kweli hatukusikia kitu chochote ila mbwa wa jirani yetu alibweka sana, mtoto wangu Jack ambaye nilimwamsha ajiandae ili twende kanisani ndiye aliyeigundua maiti ya binti huyo na kututaarifu na sisi tukamtaarifu mjumbe wa mtaa,” alisema mama huyo. Alisema maiti hiyo ya Zainabu ilikuwa imevuliwa nguo zote na nguo yake ya ndani ikiwa imening’inia miguuni na miguu yake ikiwa imetanuliwa; jambo ambalo lilisababisha mama huyo akimbilie nguo ndani ili auhifadhi mwili huo. Kwa mujibu wa Mjumbe Msaidizi ambaye pia ni mtoto wa Mjumbe, Gideon Mwakalange, alipata taarifa za kutokea tukio hilo alfajiri na hivyo kuthibitisha kutokea kwa kifo hicho na ndipo alipotoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mazizini. Alisema baada ya Polisi kuwasili walichunguza na kubaini kuwa mtoto huyo inawezekana hakuuliwa katika eneo ambako mwili wake umetupwa, bali sehemu nyingine na mwili wake kutelekezwa eneo hilo. Naye mama mlezi wa binti huyo, Sikudhani Puga, alisema mwanawe alitoka na wenzake juzi usiku akienda kwenye sherehe ya mkesha wa rafiki yake umbali wa mita 100 kutoka nyumbani kwake, ambako kulikuwa na mwali anatolewa na baada ya hapo hafahamu chochote kilichotokea huko. “Mimi sifahamu chochote kilichoendelea huko zaidi ya kujua kwamba alienda kwenye sherehe ya rafiki yake na kwamba wenzake walimtafuta bila mafanikio mpaka asubuhi hii tulipoletewa taarifa ya kifo chake,” alisema Puga. Alisema kwa mujibu wa wenzake wakati wanamtafuta Zainabu, waliambiwa kuwa ameondoka na kijana anayefahamika kwa jina moja la utani Sikomi, ambaye naye katika tukio hilo alijeruhiwa vibaya na panga na amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku hali yake ikiwa mbaya. Binti huyo huenda akazikwa leo baada ya Polisi kumaliza uchunguzi wao. Maiti iko Hospitali ya Amana. Awali Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Kandihabi, alisema maiti ya binti huyo ilikutwa imesokomezwa kitambaa mdomoni huku ikiwa imevuliwa nguo ya ndani; jambo lililoashiria alibakwa. | |
No comments:
Post a Comment