Saturday, December 01, 2007

RAI YA JENERALI ULIMWENGU

Kura: Tuwazomee wauzaji na wanunuzi

TUMEJADILI kwa muda mrefu suala la biashara ya uchaguzi, yaani ununuzi na uuzaji wa kura kwa njia ya fedha na vishawishi vinginevyo. Vitendo vya ufisadi katika chaguzio mbali mbali nchini vimepigiwa kelele na kulaaniwa kila unapofanyika uchaguzi, ama ndani ya chama cha siasa ama katika michakato ya uchaguzi wa wakilishi katika majlis mbali mbali.

Kinachoonekana hivi sasa ni kwamba, pamoja na kelele zote hizo, na pamoja na laana zote zilizotolewa kutoka kwa watu na asasi mbali mbali, bado tatizo linazidi kuwa kubwa na kila uchaguzi unaofanyika unadhihirisha ufisadi mkubwa zaidi kuliko uchaguzi uliotangulia.

Inaonekana kama vile kadri ufisadi unavyozidi kujichimbia katika mifumo ya uchaguzi ndivyo mafisadi wengine wanavyozidi kushawishika kuingia katika siasa.

Hatari za mwenendo huu zimekwisha kujadiliwa, na watu mbali mbali wametutahadharisha kuhusu mchezo huu mchafu. Kifupi, ni kwamba huu ni mchezo ambao hatima yake ni kufuta kabisa heshima ya michakato ya uchaguzi, kuvunja imani ya wananchi kwa uchaguzi na matokeo yake na kuudharaulisha mfumo wa utawala unaotokana na ufisadi huo uliokithiri.

Hatari ya msambaratiko wa kijamii na kitaifa si jambo la kufikirika tu, ni jambo lililo dhahiri. Wahenga walisema, “ Asiyejua kifo aangalie kaburi “ . Nasi tunapaswa kuangalia wenzetu waliokumbwa na matatizo makubwa kutokana na ufisadi uliogubika michakato yao ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na uchaguzi.

Nitachukua mfano wa nchi moja tu niliyoidurusu kidogo, Sierra Leone.

Niliwahi kwenda Freetown mara kadhaa katika miaka ya 70 na kujionea mwenyewe jinsi nchi ilivyokuwa inaendeshwa kwa ufisadi wa kutisha.

Wanasiasa karibu wote walichaguliwa kwa kumwaga mapesa kama njugu, mara nyingi wale wasiokuwa na fedha zao wakipigwa jeki na wafanya biashara ya Kilabnani. Kila mwanasiasa maarufu, wabunge, mawaziri, na hata rais, alijulikana kuwa ni ‘mali’ ya Mlabnani fulani.

Mara ya mwishoi nilipokwenda Freetown nilikwenda Rais Siaka Stevens, ambaye alikuwa kachoka kwa umri mkubwa, kapoteza kumbukumbu, mezani kwake amewekewa ‘vijitoi’ vya kuchezea, kama mtoto mchanga.

Kawekwa pale kama picha huku wala-nchi wanaendelea kujichotea mapesa haramu kutokana na magendo ya almasi. Mafisadi wasivyokuwa na haya, wameendelea kumweka madarakani mzee ambaye alikwisha kuwa zezeta, haelewi kinachoendelea, alimradi waendelee kuiba watakavyo.

Tunajua kilichotokea hatimaye : mauaji ya kinyama, kukatana viungo vya mwili, ubakaji wa watoto wadogo, uchomaji moto wa vijiji vizima vizima, n.k.

Sierra Leone, ambayo ilikuwa inajulikana sehemu nyingi barani Afrika na nje ya Afrika kwa ukarimu na upole wa watu wake, ikageuka jehanam iliyojaa kila aina ya mashetani , na hali haikutulia hadi majeshi ya nje yalipoingilia kati na kurejesha utu kidogo.

Sasa, jambo ambalo sikutaraji hata kidogo ni kwamba baada ya hali kutengamaa kidogo, na Rais Ahmed Tijan Kabbah kurejeshwa madarakani, ufisadi ule ule uliokuwa ukifanywa na wanasiasa kabla ya machafuko ukarudi kwa kasi mpya kabisa.

Nilipata mshituko baada ya miezi michache pale nilipomsikia mkuu wa asasi ya kupambana na rushwa wa nchi hiyo alipokuwa akieleza (mkutanoni, mjini Nairobi) matendo ya rushwa yaliyokuwa yanafanywa na wanasiasa hao baada ya kurejea madarakani.

Nilipomuuliza ni jinsi gani wanasiasa hao wangeweza kuwa wamesahau madhila yaliyoikumba nchi yao jibu lake lilikuwa rahisi : Wanasiasa hao walikuwa wa kwanza `kupanda ndege na kukimbilia ughaibuni mara matatizo yalipoanza, na wa mwisho kurejea mara hali ilipotengamaa. Kwa hiyo matatizo yote ya nchi yao katika kipindi hicho waliyasikia kwenye redio na kuyaona kwenye televisheni, kama watu wa mataifa mengine.

Kwa maana hiyo, hawana kumbukumbu ya moja kwa moja ya yale yaliyotokea. Isistoshe, akaongeza ofisa huyo, ikitokea zahma nyingine, watapanda ndege waende ughaibuni tena, na safari hii hawatahangaika sana kwani familia zao wameziacha nje’.

Ni wazo la kutisha kwamba wanasiasa wanafanya vurugu za kila aina kiasi cha kutibua amani, lakini hali ikilipuka, wao na familia zao haoo ! Na waliobaki nchini ndio watafune ubuyu walioukaanga. Haishangazi, basi, kwamba bara hili lina watawala wengi wanaofanya mambo kama vile hawakusudii kuishi muda mrefu ndani ya nchi zao.

Sasa, kwa kuwa watawala waliozama katika vitendo vya rushwa wanao mwanya wa kutoroka hali inapochafuka, hawawezi tena kuwa na ari ya kupambana na vitendo hivyo ambavyo wanafaidika navyo angalau kwa wakati fulani. Hii ina maana kwamba jukumu la kukemea, kupiga vita na hatimaye kuteketeza ufisadi katika uchaguzi wetu lazima liwe jukumu la kila raia mwema.

Kila raia mwema ajue kwamba kwa kukubali kupewa bakhshish ili ampigie kura mwanasiasa au akipigie kura chama fulani anakuwa si tu ameuza utu wake, lakini pia anakuwa amejinyima haki ya kudai kuhudumiwa na huyo aliyemnunua, kwa sababu anunuaye bidhaa haitumikii.

Haiyumkiniki kwamba mtu ananunua kondoo halafu anakuwa mtumishi wa kumhudumia kondoo huyo. Kinachoeleweka ni kwamba, hata akimlisha vizuri na kumwangalia afya yake, hatima ya kondoo ni kuchinjwa.

Rai yangu ni kwamba wananchi wakatae kuwa bidhaa, kuwa kondoo wanaouzwa sokoni. Wawakatae wanasiasa wanaopitapita kugawa fedha na vishawishi vingine. Wawazomee. Inapowezekana waviarifu vyombo husika kuhusu matendo ya wanasiasa hao.

Ninapendekeza kuundwa kwa umoja wa raia wema wanaokataa kabisa mchezo hatari wa ununuzi na uuzaji wa kura. Tunaweza tukawa na matawi katika kila mkoa au hata wilaya, tukayaeneza nchi nzima, vikawa ni vituo vya kupashana taarifa kuhusu vitendo vinavyovuruga michakato ya kisiasa, na kuwataja mafisadi wanaobainika kuviendeleza.

Naamini kwamba harakati kama hii haiwezi kuwa na gharama kubwa, na hata hizo gharama za kupata vitendea kazi hatuna budi kuchangishana ili kuwa na mfuko mdogo wa kuendeshea harakati hizo. Kuna mantiki gani ya kuchanga mamilioni ya shilingi ya kula na kunywa siku moja harusini kisha tushindwe kuchangia shughuli ya kuliokoa Taifa kutoka katika makucha ya nyang’au wa hatari?

Hatuna budi kuongozwa na imani kwamba uchaguzi ni zoezi takatifu. Kiongozi ana sehemu ya ‘uungu’ fulani ambao tunamkabidhi sisi wenyewe kwa kutambua kwamba huo ‘uungu’ anaumudu. Anapogeuka kuwa dalali anayenunua au kuuza kura anapoteza huo ‘uungu’ na kuwa tapeli wa kawaida. Anastahili kudharauliwa na kutupwa nje.

Nimekwisha kusema kwamba namuunga mkono Jakaya Kikwete kwa msimamo aliouchukua wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM. Kila raia mwema anatakiwa amuunge mkono kwa dhati. Akifanya kazi ya kuwatambua na kuwaadhibu mafisadi ndani ya chama chake atakuwa amelifanyia kazi Taifa zima.

Lakini hakuna anayeweza kujidanganya kwamba kazi hiyo itakuwa rahisi kutokana na jinsi mizizi ya ufisadi ilivyojiimarisha katika chama hicho.

Jawabu si kuongeza makachero wa TAKUKURU, kwa sababu hili si tatizo la kipolisi; ni tatizo la kimaadili, suala la kitamaduni. Linatakiwa kushughulikiwa kimaadili na kiutamaduni. Hilo ndilo nataraji kujadili hapo baadaye. Itaendelea

Kutoka Raia Mwema wiki hii

No comments: