Na Ali Suleiman, Zanzibar
MGOGORO mkubwa umeibuka kati ya wananchi wa kijiji cha Kiwengwa na wawekezaji wa hoteli ya Bravo, ambao wanadaiwa kufunga njia ya asili iliyokuwa ikitumiwa na wanakijiji hao kitendo ambacho ni kinyume na makubaliano yao.
Mwakilishi wa jimbo la Kitope, Bw. Makame Mshimba, amethibitisha kuibuka kwa mgogoro huo na kuitaka Serikali na taasisi zake kuingilia kati kuupatia ufumbuzi haraka mgogoro huo.
"Ni kweli mgogoro umeibuka kati ya wananchi na wawekezaji wawili wa hoteli ya Bravo na Sea Club, ambao wameifunga moja kwa moja njia muhimu ya asili iliyokuwa ikitumiwa na wanakijiji hao...wamenilalamikia na wanataka suala hilo lipatiwe ufumbuzi wa haraka," alisema Bw. Mshimba.
Alisema wawekezaji hao waliifunga njia hiyo kinyume kabisa na makubaliano ya awali, wakati walipokuwa wakijenga hoteli hizo, baada ya kuuziwa ardhi na wanakijiji.
"Wametubadilikia na kukiuka makubaliano yetu ya msingi...hatukubali, tunataka kutekelezwa kwa makubaliano yetu ambapo njia hiyo lazima itumiwe na wananchi kwa ajili ya shughuli zao za kila siku," alisema mwanakijiji wa Kiwengwa, Bw. Sheha Juma.
Lakini pia wanakijiji hao wanawalaumu wawekezaji hao, kushindwa kutekeleza mikataba iliyopo, ambapo katika shughuli za utalii, ikiwamo kuuza samaki na vyakula vya mbogamboga, basi wa kunufaika na soko hilo ni wanakijiji.
Wawekezaji hao wanadaiwa kupuuza mikataba hiyo na sasa kununua baadhi ya bidhaa nyingi za chakula na samaki kutoka mjini Unguja, wakati bidhaa hizo zinapatikana kijijini hapo.
Wiki iliyopita, wakati akifungua hoteli ya Fairmont, Kiwengwa, Rais Amani Abeid Karume, aliwataka wawekezaji kuhakikisha miradi yao inawanufaisha pia wanakijiji.
Alisema miradi hiyo kama itashindwa kuwanufaisha wanakijiji hao kutaibuka malumbano kiasi cha kuhatarisha amani na utulivu wa miradi waliyowekeza.
Ukanda wa Kaskazini wa Pwani ya Kiwengwa na Pwani mchangani ni maarufu sana kwa hoteli za kitalii zenye hadhi ya juu, lakini hadi sasa wanakijiji wameshindwa kufaidika na kuwapo kwa miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment