NIMEPENDEKEZA kwamba tuwazomee wagombea wote wanaojitokeza kila muhula wa uchaguzi unapowadia na kumwaga mapesa na vishawishi vingine ili tuwape kura. Madhara ya tabia hii na kuiendekeza kwetu nimekiwsha kuyaeleza, na pale ambapo labda maelezo yangu hayakufua dafu, wenzangu nao wameeleza. Hata Mwenyekiti wa CCM mwenyewe alitoa ufafanuzi mzuri kabisa katika hotuba yake mbele ya mkutano mkuu wa chama chake muda si mrefu.
Lakini tusiishie kuwazomea tu. Hawa ni wahalifu, watu wanaofanya matendo ambayo tayari yanatambulika kama rushwa na ambayo hayakubaliki kisheria kwa sababu ni makosa ya jinai. Pamoja na maelezo yangu kuhusu dhana ya munkari (ukiweza ondoa kwa mkono wako; huwezi kemea usikike; huwezi hata hilo, nuna uonekana umechukia), bado kuwazomea watu wanaotenda makosa ya jinai hakutoshi.
Iko sugu iliyojengeka hivi leo, na sugu hiyo wamejivisha mafisadi wa kila aina nchini kama kinga dhidi ya mashambulizi yote yanayoelekezwa kwao alimradi tu mashambulizi hayo ni ya maneno matupu na wala hayawasababishii maumivu ya kimwili wala hasara ya kifedha.
Wanazisikia shutuma dhidi yao; wanasoma magazeti, au hata kama wameacha kusoma kwa kutotaka kujiona wanavyodhalilishwa, bado wanaambiwa na ndugu zao na maswahiba zao jinsi wanavyoandikwa na kusemwa na kulaaniwa, lakini wao wamekuwa wasadiki wakubwa wa falsafa ya ‘maneno matupu hayavunji mfupa’ au ‘watasema mchana, usiku watalala”. Alimradi hakuna hatua madhubuti za kuwafanya walipe na waumie kutokana na matendo yao hawatakuwa na motisha wa kuyaacha, hasa kama yanawaletea manufaa fulani fulani, na manufaa haya tunayajua.
Dawa mujarrab ya kuwafanya wakome kufanya upuuzi wao ni wa kuwafanya walipe gharama kubwa ili upuuzi wao uwe ghali. Hii ndiyo njia pekee ya kutokomeza utamaduni wa kutoadhibika (impunity) ambao umetawala mwenendo wa siasa katika Tanzania.
Nimefuatilia jinsi ambavyo vyombo vya kisheria vilivyoingizwa katika mchakato wa uchaguzi ndani ya chama-tawala, na jinsi baadhi ya wakubwa walioshukiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa walivyotiwa msukosuko kidogo. Inawezekana hatua hizo dhidi yao zilichukuliwa kwa dhati, na kwamba wapo watu katika ngazi za juu za chama hicho waliodhamiria kukisafisha chama hicho kwa kuwaengua na kuwachukulia hatua wale wanaobainika kwamba wamefanya mambo machafu katika mchakato wa uchaguzi wa chama.
Lakini nitawaomba radhi wakuu hao: nitawaomba waniruhusu niwe Tomaso Mwenye Shaka au Doubting Thomas. Hapa naomba nitoe maelezo machache. Kwanza sina uhakika kwamba ‘Mwenye Shaka’ ndilo jina lake rasmi katika Kiswahili ingawa sina tatizo kuhusu jina lake kwa Kiingereza. Pili waumini wa dini husika nawaomba radhi kwa kutumia mfano mwingine kutoka maandiko (yao) matakatifu labda kwa makosa. Tatu inawezekana Tomaso angekuwa anaishi enzi tulizo nazo leo labda siyo tu angetia shaka lakini labda pia angesema kwamba hapendi utani kuhusu masuala mazito.
Lakini wanasayansi yakinifu wanaweza kumweleza Tomaso kama mwanasayansi aliyekataa kupokea maelezo ya juu juu na aliyetaka uthibitisho yakinifu kuhusu kufufuka kwa Bwana Yesu, ambaye Tomaso alikuwa na uhakika kwamba alikuwa amekufa Msalabani. Nami nakiri kwamba nahitaji ithbati isiyobahatisha kwamba kile ambacho kimekuwa ndio mwenendo wa uchaguzi katika chamatawala kwa muda mrefu, na ambacho kimelelewa tukikiona hadi kimefikia hatua ya kuwa ndio utamaduni ndani ya chama hicho, sasa kinapigwa vita kwa dhati na wale wale walioingia madarakani kwa kukitumia hicho hicho.
Isitoshe, naamini kwamba ninayo sababu nzuri zaidi ya kuhitaji uthibitisho ulio thabiti zaidi kuliko Tomaso kwa sababu angalau Tomaso alikuwa ameshuhudia, au amesimuliwa jinsi Bwana Yesu alivyokuwa amefufua wafu na kutenda miujiza mingine huko Kapernaum na kwingineko, kiasi kwamba ingekuwa rahisi zaidi kwake kuamini kwamba aliyewafufua wengine naye kafufuka. Hadi wa leo mimi binafsi sijaiona Kapernaum yetu.
Hii ina maana mzigo wa kuthibitisha kwamba ipo nia ya kweli ya kupambana na ufisadi huu wa uuzaji na ununuzi wa kura uko mabegani mwa wakuu wa chama-tawala, ambao wanatakiwa wathibitishe hivyo kwa matendo, na si kwa maneno matupu. Ada ya mja hunena, muungwana ni vitendo. Aidha tusijiruhusu kusahau kwamba suala la kukomesha ufisadi ndani ya chama-tawala na ndani ya jamii iliyo pana si suala la kipolisi, kama ambavyo nimekwisha kusema. Ni suala la kisiasa, kimaadili na kiutamaduni. Kuziingiza asasi kama vile TAKUKURU na nyingine za kisheria katika kuwadhibiti mafisadi wa kisiasa kunaweza kuwa na maana pale tu ambapo tuna uhakika kwamba walio wengi katika mchakato husika wamefanya mambo yao, ikiwa ni pamoja na kampeni kiungwana na wamefuata kila taratibu inayofaa kuhusiana na maadili, na kwamba ni watu wachache tu ambao wamekuwa na ufedhuli wa kukiuka maadili yanayofuatwa na wengi.
Kile tunachokijua hivi leo hakitupi wasaa wa kuamini hivyo. Inawezekana si wote walioingia katika mchakato huo walijihusisha na ununuzi na uuzaji wa kura, na nimekwisha kutoa mfano wa yule kijana aliyetamka hadharani, tena kwa kuringa, kwamba yeye hakutoa hata ndururu. Lakini, hata kama samaki mmoja akioza si wote wameoza, (kama alivyodai mmoja wetu majuzi), je, mvuvi atamwuzia nani tenga la samaki mia wakati ndani ya tenga hilo wamo samaki watatu waliooza? Na, je, si kweli kwamba nazi mbovu harabu ya nzima?
TAKUKURU na asasi nyingine zitamkamata nani na nani zitamwacha? Je, vyombo kama hivyo, hata kama vingekuwa na nguvu za uadilifu miongoni mwa wakuu wake, vinaweza hata siku moja vikadiriki kusema kwamba labda robo ya wajumbe walioingia katika Halmashauri Kuu walitumia rushwa na kwa hiyo hawafai kuwa wajumbe bali wanapelekwa mahakamani kujibu tuhuma za rushwa katika uchaguzi?
Au, kuna ye yote mwenye shaka kuhusu malalamiko kwamba angalau robo ya waliochaguliwa walihusika na vitendo vya aina hiyo, baadhi vikiwa vimeelezwa na mwenyekiti wa chama-tawala na baadhi vikiwa havijatajwa kabisa? Potelea mbali, hata tungekubaliana kwamba waliohusika walikuwa ni nusu ya robo, au hata robo ya robo, ni hatua gani za maana zimechukuliwa hadi sasa?
Imejengeka tabia ya kulizungumzia tatizo juu juu na kulilaani kiulainilaini, na kisha kuliacha lilivyo kama vile tunaamini kwamba likichoka litajiondokea. Haliondoki, ng’o! na wale waliotafuta uongozi kwa udi na uvumba hawana budi kujua kwamba walichokitafuta ni kushughulikia masuala kama haya, tena bila ya kumwonea haya mtu ye yote, hata kama mtu huyo aliwasaidia katika upatikanaji wa nafasi zilizokaliwa bila kufanyiwa kazi.
Kama kweli kuongoza ni kuonyesha njia, wale wanaotaka kuwa viongozi (na si maofisa tu) watuonyeshe njia ya kuondokana na balaa hili. Hata kama nimezungumza kirefu kuhusu chama-tawala, nataka kurudia tena kwamba uoza ninaoujadili hauko ndani ya chama hicho peke yake. Hapana shaka kwamba uoza huo umekwisha kujijenga sana ndani ya serikali na vyombo vingine vya dola, kwa sababu tumekwisha kuona ni jinsi gani imekuwa vigumu kutofautisha baina ya chama-tawala na dola, lakini uoza umo pia hata ndani ya vyama vya upinzani, na hata ndani ya jamii iliyo pana, kwani sote tunatokana na kisima kimoja kilichochafuka.
Tofauti kati ya chama-tawala na vyama vingine ni kwamba chenyewe ndicho kimeshika dola na kinaweza kumzawadia kinayetaka kumzawadia na kumnyima (na hata kumwadhibu) kinayetaka kumnyima (au kumwadhibu). Kwa maana hiyo ushindani ndani ya vyama vingine bado ni mdogo, ingawa tunaweza kuhisi, kwa kuangalia yanayotokea leo, kwamba siku moja kimojawapo kikishika madaraka ya dola siku moja, kitakuwa nacho ni chama-tawala, pamoja na udhaifu wote tunaouona katika chama-tawala cha leo.
Siku moja (labda katika maisha yangu, au nikiwa nimekwisha kuyoyoma) kutakuwa na chama-tawala kingine. Watu wengi, na hasa matajiri na wakwasi wengine ambao leo wanaonekana kama wasioweza kutengana na chama-tawala cha sasa, watajiunga na hicho chama-tawala kipya, watajifanya wafadhili wake wakubwa na mambo yatakuwa yale yale, kama hayakurekebishwa sasa.
Hata hivyo, chama-tawala cha leo ndicho kilichopata ridhaa ya kuongoza nchi hii. Iwapo kitaamua kuitawala badala ya kuiongoza ni hiari yake, lakini hapo baadaye hakiwezi kumlaumu ye yote mwingine. Kikiamua kuwa chama-kiongozi kitaigwa na vyama vingine vyote na kitapata wafuasi wengi katika jamii (hata wasiokuwa wanachama), watu waliokata tamaa kwa sasa kwa sababu wanaelewa kwamba matatizo yao hayawezi kushughulikiwa na wanunuzi wa kura wanaotumia fedha, pilau na pombe kuwaghilibu wananchi wawaweke madarakani ili washibishe matumbo yao.
ItaendeleaKutoka Raia Mwema wiki hii
No comments:
Post a Comment