Friday, December 07, 2007
Ng'anzo anavyozungumzia biashara ya madini
*Asema inaweza kuinua kwa kasi uchumi wa Tanzania
*Asikitika kwamba hilo limebaki kuwa kitendawili
Na Eben-Ezery Mende
"TANZANIA ni nchi tajiri ila namna ya wazawa kuumuliki utajiri huo ndio huwa kitendawili. Kwa maneno mengine utajiri wa nchi ya Tanzania unamilikiwa na wageni kutoka nje ya nchi hii.
Hivyo ndivyo anavyoanza kueleza Mkurugenzi Mtendahi wa Kampuni ya Mega Gems Ltd Bw. Ally Ng'anzo, kampuni inayojishughulisha na biashara ya madini madogo nchini.
Kufikiwa kwa Bw. Ng'anzo na kufanikiwa kufanyiwa mahojiano na mwandishi wa makaya hii ilikuwa ni katika siku ya kilele ya kutunukiwa tuzo kwa mshindi ambaye atashinda katika kinyang'anyiro cha kubuni biashara itakayofanya vizuri sokoni kitaifa na kimataifa, iliyofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.
Katika shindano hilo, Bw. Victor Mfinanga kutoka mkoani Morogoro aliweza kuibuka mshindi na kujinyakulia kitita cha sh. milioni 12 fedha taslimu kwa ubunifu wa biashara ya maziwa ya mgando.
Kwa ushindi huo umemfanya Bw. Mfinanga kuweza kushiriki shindano la kimataifa litakalofanyika nchini Nethalend na mshindi atakaepatikana katika shindano hilo ataweza kuondoka na kiasi cha fedha taslimu euro elfu 20.
Tukirejea kwa Bw. Ng'anzo ambae nae alishiriki katika shindano hilo kwa kuitambulisha biashara yake ya madini madogo aliweza kuvutia mashindano hayo kulingana na bidhaa alizokuwa amezitandaza mezani na kuwaeleza watu mbalimbali waliokuwa wakitaka maelezo kuhusu madini aliyokuwa nayo.
Bw. Ng'anzo alieleza kuwa Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali lakini bado nchi inaendelea kuwa tegemezi na uchumi kuzidi kudidimia kutokana na kukosa wahamasishaji wa ukuzaji wa sekta ya nishati na madini.
"Nasema haya kwa kuwa mimi niko ndani ya biashara hii ya madini na nimetembea nchi mbalimbali kutafuta soko na nimepata maoni mbalimbali ya watu. Kama hatutabadilika Tanzania kuhusu uongozi kweli tutazidi kuishi umasikini na utajiri wetu wakiufaidi watu wengine."alisema Bw. Ng'anzo.
Akielezea madini aliyokuwa anayauza katika biashara yake kuu ya madini alisema Tanzania ina madini ya aina mbalimbali na kuna madini ya aina mbalimbali ambayo hayapatikani katika nchi nyingine yoyote isipokuwa Tanzania lakini kutokana na ukosefu wa vitendea kazi na kutokuthamini wachimbaji wa madini hali inabaki kuwa kama inavyo onekana hivi sasa.
Anasema ipo mikoa ambayo hasa ndiyo hutoka madini hayo ambayo ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro katika eneo la Same, Dodoma eneo la Aneti na Kondoa pia Tanga eneo la Handeni.
Yawezekana ukawa hauyatambui madini ambayo yanapatikana katika nchi ya Tanzania na ambayo yanasoko kubwa nchini Tailand, China na Ujerumani kwa nchi zilizo nje ya bara la Afrika na nchini Afrika ya Kusini, Botwasa na kwa nchi za bara la Afrika.
Pamoja na madini ambayo ulizoea kuyasikia kuwa Tanzania inachimba ikiwemo madini ya chumvi, tanzanite na dhahabu lakini pia haya ni madini ambayo yamo katika nchi ya Tanzania na yanasoko kubwa nje ya nchi lakini kutokana na tatizo la mashine za kuchimba madini hayo yameonekana kuwa adimu sokoni.
Madini hayo kama yalivyoainishwa na mtaalamu wa biashara hiyo, Bw. Ng'anzo ni pamoja na iolcte, white quarte, yellow tourmaline, sun stone, red garnet, green kynite, aquandline, nut sapphere, red ziituone, amethyst, moon stone, green tourmalne, blue kaynite, rose quarte.
Madini mengine ni feldisber, chgstonsphrase, yellow Opac, golden shine-feldisper, rub-cabochon, plimk toumaline cabochon, chrystal quarts, white opac, rhodolite-garnet na yellow scarpolite.
Hayo yote ni madini ambayo yanapatikana nchini Tanzania na soko lake kubwa kama ilivyoelezwa hapo juu kuwa ni nchini Tailand na Hong Kong China.
Kwa nini Soko kuu likawa nchini Tailand?
Bw. Ng'anzo anasema kuwa historia inaeleza kuwa awali nchi hiyo ilikuwa inachimba madini aina ya rub-cabochon ila sasa madini hayo yameshakwisha. Kutokana na kuwepo kwa madini ya aina hiyo hapo awali walikuwa ni wachongaji wazuri wa madini hayo na nchi hiyo ilikuwa kitovu cha ununuzi wa madini ya aina hiyo duniani.
Pamoja na madini ya rub-cabochon pia Tailand ni nchi inayoongoza kwa kuwa wanunuzi wakubwa wa madini ya amethyst na red ganet.
Ziara alizozifanya Bw. Ng'anzo katika nchi mbalimbali kufanya utafiti wa soko la madini linavyokwenda, anasema aliweza kubaini kuwa katika nchi ya Tailand na China kuna uhitaji mkubwa wa madini hayo lakini hata robo ya kupunguza kiu ya wahitaji haijafikiwa.
"Ni uwezo na vifaa vya kuchimba madini havipo lakini kama ingekuwa kuna mitambo hiyo vijana wengi wangeweza kupata ajira na kuondokana na tatizo la ajira kama inavyo onekana hivi leo,"anasema.
========
Pengine anasema Serikali inatakiwa kuangalia eneo hili kwani katika eneo ambalo Serikali imeonekana kulisahau ni pamoja na hili la uchimbaji wa madini kwani ukijitokeza uwekezaji katika eneo hili na kupewa masharti yakuzingatia kuwajali wazawa maendeleo yataonekana kwa kipindi kifupi.
==========
Ofisa Mipango wa Kampuni hiyo ya Mega Gems Ltd Bi. Lilian Maulambo anasema kuwa ipo mikoa ambayo imebarikiwa nchini Tanzania kuwa na bidhaa adimu si Tanzania peke yake bali barani Afrika na pengine duniani.
Anasema mikoa hiyo ni pamoja na ile ambayo inapatikana madini ya kawaida kama Mkoa wa Morogoro, Songea, Singida, Arusha na Kilimanjaro.
Anasema mfano mkoa kama Kilimanjaro umejaliwa vitu vingi ikiwa ni pamoja na kupatikana madini aina ya iolite, white quatre na yellow tourmaline. Lakini pamoja na kupatikana kwa madini hayo pia mkoa huo umejaliwa kwa kilimo cha migomba, mahindi na maharage.
Bi. Maulambo anasema kubwa lililoipatia sifa Tanzania na Afrika kama si dunia ni kumiliki mlima mkubwa kuliko yote barani Afrika.
Anasema mikoa kama Arusha, Songea, Singida na Morogoro ni mikoa ambayo imejaliwa kuwa mikoa yenye vivutio vya kitalii lakini pia imepatikana kuwepo kwa madini ambayo hayapatikani katika nchi nyingine yoyote.
==========
"Siwezi kuwa mbali na usemi alioutoa mwenzangu kuwa Tanzania ni nchi tajiri tena sana kupitia kwenye eneo hili la madini lakini sielewi kwa nini hili halionekani na Serikali. Ningependa nitoe ushauri kwa Serikali kuwa waangalie eneo hili ili nchi iweze kuinuka kiuchumi na vijana ambao ndio mhimili wa nchi yoyote waweze kupata kazi."anasema Bi. Maulambo.
============
Akielezea matumizi ya madini hayo ambayo huyauza Bw. Ng'anzo anasema madini hayo hutengenezea vito vya urembo kama hereni, pete, vikuku na mikufu ya shingoni.
Mbali na utengenezaji wa bidhaa hizo pia madini hayo yamekuwa yakitumika katika kutengenezea sakafu za tezaro ambazo hasa hutumika katika maeneo ya kumbi za starehe, sehemu za choo ama bafu na maeneo ya jikoni.
Bw. Ng'anzo anaendelea kusema kuwa katika aina ya madini aina ya white opac huweza kutumika katika kutengenezea mapambo ndani ya nyumba kama fremu za kuhifadhia picha na wakati mwingine hutengenezea vinyago.
Kama madini ya aina yote hii yanapatikana Tanzania sioni sababu ya kuendelea kuwa tegemezi na kuwekeza katika sekta ambazo wananchi wenyewe hawaoni faida zitokanazo na uwekezaji wenyewe.
Nakubaliana na usemi wa wajasiriamali Bw. Ng'anzo na Bi. Maulambo kuwa Serikali haijatambua sehemu ambayo inatakiwa iangaliwe ili kuinua maisha ya Watanzania na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mfano Bw. Ng'anzo anasema tathmini aliyoifanya nchini China kuhusu wingi wa watu wanaohitaji madini na madini ambayo yanawafikia alibaini kuwa uhitaji uliopo kwa watu wa nchi hiyo ni asilimia 80 lakini bidhaa wanayo fikishiwa ni asilimia 12.
Natumaini kama maisha bora kwa kila Mtanzania hayatakuwa hadithi bali kitu cha kutekelezeka, Serikali itayachukua kila maoni ya wananchi ambayo yametolewa katika kuhakikisha Tanzania inabadilika na kupiga hatua ya mafanikio na kuyafanyia kazi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment