Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuipa ruksa ya kufanya chochote kilicho ndani ya uwezo wake kughughulikia mafisadi nchini, sasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, TAKUKURU, ni noma kweli kweli.
Chini ya mikakati yake mipya, TAKUKURU imeapa kuyakomba mapesa yote yaliyotwaliwa kwa njia za rushwa na baadhi ya vigogo Serikalini na watu wengineo nchini kabla ya kwenda kuyaficha kwenye akaunti za mabenki yaliyo nje ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa toka kwa chanzo chetu ndani ya TAKUKURU, ni kwamba chini ya mkakati huo, baadhi ya vigogo wenye tabia za ulafi wa mali za umma wataipata freshi.
Kimesema chanzo hicho kuwa hadi sasa, mkakati huo uko katika hatua muhimu inayoweza kuzaa matunda katika kipindi kisichokuwa kirefu kuanzia sasa.
Chanzo hicho kimeihabarisha Alasiri kuwa hatua hiyo, ni sehemu ya mbinu za kisasa zinazoendelea kubuniwa na TAKUKURU katika kukomesha vitendo vya rushwa kubwa kubwa (grand corruption), ambayo hurudisha nyuma nia njema ya Serikali katika kuwaletea maisha bora wananchi wake.
`Mara zote, wala rushwa kubwa kubwa hukimbizia mapesa yao katika akaunti za nje ya nchi sasa TAKUKURU iko katika mchakato wa kuhakikisha kuwa mapesa hayo yanarejea nyumbani ili yatumike kwa maendeleo ya nchi,`kikasema chanzo chetu.
`Mkono wa TAKUKURU utafika Uingereza, Ufaransa, Italia, Uswis na kokote kule duniani pia wahusika watachukuliwa hatua za kisheria, tena bila kujali nafasi zao katika jamii,` kikaongeza chanzo hicho.
Aidha, katika kuthibitisha kuwa sasa TAKUKURU imepania hasa kuwaletea noma wala rushwa vigogo almaarufu kama mapapa, jana Mkurugenzi wake mkuu Dk. Edward Hosea alizungumzia suala hilo la kurejeshwa kwa fedha na mali zilizosafirishwa nje ya nchi kwa njia ya rushwa jana.
Dk. Hosea alizungumzia suala hilo wakati akiwa kwenye semina ya masuala ya rushwa iliyofanyika katika hoteli moja Jijini ambapo mwezeshaji mmojawapo katika semina hiyo alikuwa Bw. Alan Bacarese.
- SOURCE: Alasiri
No comments:
Post a Comment