Monday, December 10, 2007

Uhuru wa Tanzania wazua hoja Bunge la Marekani


*Msimamo wa Mwalimu, mtazamo wake waelezewa
* Lowassa aonya wanaobeza mafanikio ya uhuru

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

BARAZA la Wawakilishi la Marekani limeipongeza Tanzania kwa kutimiza miaka 46 ya Uhuru.

Katika hatua hiyo ambayo ni nadra kufanywa na Baraza hilo kwa mataifa ya kigeni, limempongeza pia Rais Jakaya Kikwete kwa juhudi zake za kupambana na rushwa na mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI.

Pongezi hizo zimekuja baada ya Baraza hilo kuunga mkono kwa kauli moja hoja iliyotolewa na Mwakilishi, Bw. Ryan kutoka jimbo la Wisconsin Jumatano iliyopita kuhusu, mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Tanzania.

Rekodi ya shughuli za Baraza hilo la 110,zilizopatikana mjini hapa, zinaonesha limempongeza Rais Kikwete kwa uongozi bora katika masuala mbalimbali na uwazi katika kuendesha Serikali.

Rekodi ya shughuli za Baraza hilo, iliwasilishwa kwa Rais Kikwete jana mjini hapa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Mark Green.

Balozi Green alikuwa mjini hapa kuhudhuria sherehe za Miaka 46 ya Uhuru wa Tanzania bara zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri na baadaye alikutana na Rais Kikwete Ikulu ndogo ya Chamwino.

Katika hoja yake Mwakilishi Bw. Ryan alikaririwa akisema “Nasimama kuadhimisha Kumbukumbu ya miaka 46 ya Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Tanganyika) na kuwapongeza viongozi na wananchi wa Taifa lile kubwa kwa yale yote ambayo wamefanikiwa kuyapata mpaka sasa.”

Aliongeza “Ni vigumu sana kuzungumzia historia na maendeleo ya Tanzania bila kumkumbuka mwanzilishi na Rais wa kwanza, Julius Nyerere. Mwalimu, ama 'Teacher' kama alivyojulikana kwa umaarufu, alikuwa mtu mahiri miongoni mwa viongozi wa Afrika wa wakati wake.”

Alimsifu Mwalimu Nyerere na kusisitiza, “Alijitolea maisha yake katika ujenzi wa hisia za umoja na utambulisho. Alitamani wananchi wake kujitambua na kujiona kama Watanzania kwanza na siyo kujigawa na kujitambulisha kwa dini zao ama makabila yao. Karibu nusu karne baadaye ni dhahiri kabisa kuwa ndoto yake hiyo bado inaendelea kujengeka vizuri.”

Kuhusu Rais Kikwete, Bw. Ryan alisema “Ni lazima pia kumpongeza Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa juhudi zake kuendeleza kazi nzuri ya Mwalimu na ya viongozi wengine wa Tanzania.”

“Kutoka kwenye uongozi wa kuongoza katika Kampeni ya Kitaifa ya Kupima Virusi vya UKIMWI (HIV/AIDS) hadi kwenye wito wake wa kuendesha Serikali yake kwa uwazi na mapambano yake dhidi ya rushwa. Rais Kikwete amejitolea bila kuchoka kujaribu kujenga nchi bora zaidi na maisha bora zaidi ya wananchi wake,” alisema Bw. Ryan.

Kuhusu Uhuru wa Tanganyika, Bw. Ryan aliitaka Marekani kusherehekea utamaduni wa Tanzania wa amani na utulivu.

“Vile vile tunaposheherekea uhuru huo ni lazima kuishukuru Tanzania kwa urafiki wake na Marekani na pia kuahidi kushirikiana kwa karibu zaidi na Rais Kikwete na wananchi wake kwa kadri wanavyosonga mbele, kwa kujiamini.”

Naye Joyce Kassiki anaripoti kuwa Rais Kikwete jana aliongoza maelfu ya wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa jumla katika kusherehekea Madhimisho ya Miaka 46 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Katika maadhimisho hayo, Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, alikagua gwaride rasmi lililoandaliwa na vikosi hivyo.

Kabla ya kukagua gwaride, Rais alipigiwa mizinga 21 kwa heshima yake.

Sherehe hizo zilipambwa na halaiki ya vijana 1,000 kutoka shule mbalimbali za sekondari mkoani hapa ambao walipita mbele ya Rais na kuonesha michezo mbalimbali.

Sherehe hizo zilihudhuria pia na viongozi wastaafu akiwemo Rais wa Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Frederick Sumaye na viongozi mbalimbali wa kitaifa.

Wakati huo huo Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa amewaonya watu wanaobeza mafanikio ya Miaka 46 ya Uhuru wa Tanzania Bara na kueleza kuwa jambo hilo linaweza kusababisha wananchi kukosa imani na Serikali yao.

Bw. Lowassa aliyasema hayo jana kwenye hafla fupi ya kukabidhi vyeti kwa taasisi na
kampuni zilizoshiriki kuchangia na kufanikisha maandalizi ya sherehe hizo.

Alisema wanaobeza mafanikio ya Miaka 46 ya Uhuru, wamekuwa wakipata nafasi hiyo kutokana na wadau mbalimbali kushindwa kutangaza mafanikio yaliyopatikana kupitia vyombo vya habari.

“Leo kuna baadhi ya vyombo vya habari vimetangaza Miaka 46 ya Uhuru hakuna kitu, yote haya yamesababishwa na wadau kushindwa kutumia nafasi ya kutangaza makala mbalimbali katika vyombo vya habari na kuwapa nafasi watu wabaya kubeza Miaka 46 ya Uhuru,”
alisema Bw. Lowassa

Bw. Lowassa alikabidhi vyeti kwa kampuni binafsi na taasisi za umma zilizochangia, ambapo jumla ya sh. milioni 349, zimetumika kuandaa sherehe hizo mwaka huu.

No comments: