SERIKALI imeanza kuchunguza sehemu ya fedha za baadhi ya Watanzania ambazo zipo nje kuona kama zimepatikana kwa njia ya rushwa.
Miongoni mwa nchi ambazo ufuatiliaji huo unafanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) chini ya Mikataba ya Kimataifa ni zile ambazo zipo katika mwambao wa Bahari ya Hindi na nyingine za Asia.
Fedha hizo zinachunguzwa chini ya mikataba hiyo ambayo ni pamoja na wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Rushwa, Mkataba wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, ambayo Tanzania imeridhia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, alilithibitishia gazeti hili ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki iliyopita kuhusu ufutiliaji wa fedha hizo.
Hata hivyo, Marmo alikataa kutaja majina ya mabenki hayo ambayo uchunguzi huo unafanyika kwa ushirikiano na vyombo vya nchi husika.
Lakini alifafanua kwamba, Tanzania imetia saini mikataba hiyo ambayo kwa ushirikiano na nchi nyingine inaiwezesha kuwakamata na kuwarejesha nchini watuhumiwa ambao watakuwa wakichunguzwa kwa kutorosha fedha kwa njia ya rushwa.
Waziri Marmo alisema zipo fedha nyingi ambazo wanazichunguza kuona ukweli wake na watuhumiwa. "Zipo fedha nyingi tu tunazichunguza kuona kama zimetoroshwa na watuhumiwa warushwa," alisema Marmo.
"Tunajua kuna watu wanaweza wakawa wamekimbia, lakini tunachosema chini ya mikataba hiyo watarejeshwa wakibainika," alisema. Alisema chini ya mikataba hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru anaweza kuwasiliana na wa nchi husika na kuonya kwamba watuhumiwa wote watakaobainika watarejeshwa nchini.
Hata hivyo, alifafanua kwamba uchunguzi huo hauhusu watuhumiwa ambao wameweka fedha zao halali nje na kwamba wako huru kufanya hivyo. "Lakini Marmo anaweza kuweka fedha nyingi, bora tu zisiwe fedha haramu zilizopatikana kwa njia ya rushwa," alisema.
Kuhusu biashara ya fedha haramu nchini, Marmo alikiri kuwepo tatizo hilo ambalo alisema Tanzania imekuwa ni moja ya vituo vikuu. Alisema hata uamuzi wa kuanzisha Kitengo cha Kupambana na Fedha Haramu, haikuwa ya kukurupuka bali ilitokana na serikali kubaini hilo.
"Biashara ya Fedha haramu ipo kweli nchini, fedha zinatoka katika baadhi ya nchi kama za Asia, ndiyo maana tulipoanzisha kitengo cha kuzuia fedha hizo, tulijua," alisisitiza Marmo. Waziri Marmo alisema baadhi ya biashara hizo za fedha haramu zilikuwa ni kutoka katika baadhi ya nchi za Asia.
No comments:
Post a Comment