Innocent Mwesiga
WIKI iliyopita (Desemba 4, 2007) Waziri wa nchi, ofisi ya Rais (siasa na Uhusiano wa Jamii), Kingunge Ngombale Mwiru alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa “madai ya viongozi wa vyama vya siasa ya kutaka katiba mpya hayawezi kutekelezwa kwa vile hata wananchi wenyewe hawalifahamu kiundani suala hilo”.
Alisema kuwa “katiba ni suala la sera ya chama husika, kama kuna jambo kubwa linalohusiana na katiba ni lazima liwekwe kwenye ilani ya chama husika”.
Sikubaliani na wale wanaotaka mabadiliko ya katiba ili CCM itoke madarakani, au wale wanaotaka katiba ibadilishwe ili viwepo vipengele vya kuwaingiza madarakani kirahisi. Vilevile sikubaliani na wanaotaka katiba isibadilishwe ili CCM iendelee kukaa madarakani.
KINGUNGE Ngombale-Mwiru |
Napingana na mawazo ya Kingunge kwamba katiba ya nchi ni suala la sera ya chama, hivyo jambo linalohusu katiba lazima liwekwe katika ilani ya chama husika.
Kama nilivyoandika katika makala zilizotangulia, makusudio ya kuwa na katiba ni kuhifadhi haki za msingi za wananchi ambazo zilikuwapo kabla ya uundaji wa katiba, na kabla ya uwepo wa vyama vya siasa. Naamini kwamba suala la katiba ni la wananchi na si la vyama vya siasa.
Kingunge amekaa katika uongozi kwa muda mrefu kuzidi kiongozi mwingine yeyote katika safu ya uongozi wa Kikwete. Ameshuhudia mabadiliko ya katiba yakifanywa bila kuombewa ridhaa ya wananchi kupitia katika ilani ya uchaguzi.
Matokeo yake, tumeambulia katiba yenye viraka vingi vinavyopingana vyenyewe kwa vyenyewe.
Mfano, ibara ya 20 (4) ya katiba ya Tanzania inapiga marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote au shirika lolote. Na ibara ya 13 (2) inapiga marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamuhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake. Na ibara 13 (5) imefafanua maana ya neno kubagua.
Hivyo basi, kila raia alikuwa na haki ya kuchaguliwa kuwawakilisha wenzake bila kulazimishwa kujiunga na chama cha siasa. Mwalimu alipata kutuhadithia mkasa uliompata alipokwenda jimbo la Mbulu kumpigia kampeni mgombea ubunge kupitia tiketi ya chama cha TANU.
Alisema juhudi zake hazikuzaa matunda kwani wananchi walimchagua Chifu Sarwat aliyeomba kuwa mwakilishi wao bila kupitia katika chama cha siasa.
Pamoja na kudumazwa na mfumo butu wa chama kimoja, lakini haki ya uwakilishi ilikuwa ni ya kikatiba na haikuwahi kufutwa au kuwekewa sharti lolote.
Waswahili wanasema ukuukuu wa kamba si upya wa ukambaa. Mfumo wa vyama vingi ulikuja na kasoro zake. Mwaka 1992, Serikali, bila ridhaa ya wananchi, ilifanya mabadiliko ya katiba na kuiwekea sharti haki ya mtu kuchaguliwa kuwa mwakilishi. Sharti liliwekwa katika ibara ya 39 (1) (c), 47 (4) (c), na 67 (1) (b), kwamba mgombea yeyote wa urais, umakamu wa urais, au ubunge, lazima awe mwanachama wa chama cha siasa, na aliyependekezwa na chama cha siasa.
Sharti lingine liliwekwa katika ibara ya 38 (2) (c), na 71 (1) (e) kwamba Rais au Mbunge ataachia kiti chake endapo ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa kuwa Rais au mbunge.
Masharti yote haya yanabagua asilimia kubwa ya watanzania ambao sio wanachama wa vyama vya siasa, na yanapendelea asilimia ndogo sana ya Watanzania ambao ni wanasiasa.
Kwa kutumia haki yake ya kikatiba ibara ya 30 (3), Christopher Mtikila, alifungua shauri namba 9 mwaka 1993 katika Mahakama kuu ya Tanzania kupinga viraka ndani ya katiba vilivyowapora watu haki zao za msingi.
Mwaka 1994 Jaji Kahwa Lugakingira, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, alikubaliana na hoja za Mtikila. Alitoa muda maalumu kwa Serikali kufuta hayo masharti ndani ya katiba.
Serikali ilikata rufani kupinga uamuzi wa Mahakama. Ajabu, iliondoa rufani na badala yake ikawasilisha muswada mpya bungeni.
Hata hivyo, Mtikila alifungua shauri jingine namba 10 katika Mahakama Kuu mwaka 2005 na kushinda kesi. Tokea mwaka 1992 mpaka leo, Serikali haijawahi kutoa maelezo ya kinaga ubaga kwa wananchi kuhusu sababu zilizoifanya iwanyang’anye raia haki zao za msingi za kuwawakilisha wenzao.
Maelezo pekee ya Serikali yanapatikana katika rufani ya kupinga uamuzi wa Mahakama kuu. Mwanasheria Mkuu wa Serikali anasema uamuzi wa Mahakama Kuu unawanyima wananchi mfumo wa kisheria wa kushiriki katika utawala wa Serikali.
Muda wote Serikali imeazima busara za watoto wadogo wachezao mchezo wa buguyu-buguyu au kibafute wa kukisia idadi ya vitu vilivyofumbatwa katika gao la mkono wa mwingine.
Suala la kutoa maelezo limeachwa mikononi mwa mashabiki ambao wanaishia kuhisi na kubuni hoja zilizofumbatwa ndani ya viganja vya Serikali.
Kwanza, suala zima limefanywa lionekane kama ni ushindani wa malumbano kati ya Serikali na Mtikila. Pili, limepotoshwa ili ionekane kwamba, aliyenyang’anywa haki yake sio raia bali ni kitu kinaitwa mgombea binafsi.
Ukosefu wa maelezo ya kina kutoka Serikali na upotoshaji wa hoja ufanywao na mashabiki, haviondoi ukweli kwamba aliyenyang’anywa haki yake ya msingi si mgombea binafsi, bali ni wananchi wa Tanzania.
Hili si suala kati ya Mtikila na Serikali, bali ni kati ya wananchi na Serikali. Kuendelea kuwapo kwa haya masharti, kumetufikisha mahala ambapo, wabunge ambao kikatiba wanatakiwa kuwawakilisha wananchi, wanaviwakilisha vyama vya siasa bungeni.
Katika biashara ya ajira, kuna mwajiri na mwajiriwa. Sifa kuu ya mwajiri ni uwezo wa kumwajiri, kumlipa, na kumwachisha kazi mwajiriwa. Na sifa kubwa ya mwajiriwa ni uwezo wa kuchapa kazi kadri ya maelekezo ya mwajiri, ujuzi, na nidhamu ya kazi ya kufuata kanuni zilizowekwa na mwajiri wake.
Mwajiri asiye na sifa nilizozitaja hathaminiki. Vivyo vivyo kwa mwajiriwa. Katika duru za kisiasa, wananchi wanapaswa kuwa waajiri na wabunge wanapasha kuwa waajiriwa wa wananchi, na si vinginevyo.
Binafsi, nadhani mfumo wa vyama vingi ulilenga kuwaongezea wananchi sifa kamilifu za uajiri na kuwawekea wabunge mazingira mazuri ili wawe waajiriwa bora.
Masharti yaliyowekwa kwenye katiba yaliwanyang’anya wananchi sifa ya uajiri na kuikabidhi mikononi mwa vyama vya siasa. Wabunge wamebakia na sifa nzuri za kuwa waajiriwa bora wanao chapa kazi kadri ya maelekezo ya waajiri wao ambao ni vyama vya siasa.
Mathalani, Kamati Kuu ya CCM ina mamlaka ya kumfuta mwanachama yeyote uanachama wa CCM kadri ya taratibu zilizowekwa na chama. Ikitokea mbunge wa jimbo lolote aliyechaguliwa na wananchi akafutwa uanachama wa CCM, au chama chochote alichokuwa nacho wakati anapata ubunge, anapoteza kiti chake cha ubunge kadri ya sharti lililoko ibara 71 (1) (e).
Pia, Rais wa nchi aliyechaguliwa na wananchi akifukuzwa uanachama wa chama alichokuwa nacho wakati anapata urais, anapoteza kiti cha urais kadri ya ibara ya 38 (2) (c) ya katiba ya Tanzania.
Faida ya mfumo wa namna hii inalalia kwa vyama vya siasa zaidi kuliko kwa wananchi. Wabunge wanalazimika kuwa na mshikamano wa kutekeleza maelekezo na sera za chama wakijua kuwa wasipofanya hivyo, watapoteza ubunge wao.
Pia ni mfumo mzuri wa wanachama kudhibiti mienendo na matendo ya Rais akiogopa kufukuzwa uanachama na kupoteza kiti chake cha urais.
Hakuna chama kinachopenda kupoteza wabunge kwa sababu, mosi, chama kinahitaji idadi ya kubwa ya kupiku wabunge wa vyama vingine wakati wa kupitisha miswada bungeni.
Pili, vyama vya siasa vya siku hizi sio kama vya zamani vilivyoimarika kutokana na michango ya wanachama. Hivyo, faida nyingine ni upatikanaji wa ruzuku ambao unawiana na idadi ya wabunge katika chama husika.
Kumpoteza mbunge, ni kupoteza ruzuku. hivyo mfumo huu unawaning’iniza wabunge ndani ya vyama walivyopatia ubunge wao. Faida nyingine ni kuwabana wabunge wanaopenda kuhama vyama bila sababu za msingi au wanaoweza kupeleka bungeni hoja zinazopingana na sera za vyama vyao.
Mfano, mwaka 1993, wabunge machachari wajulikanao kama G55, walijiandikisha kupeleka bungeni hoja ya kudai Serikali ya Tanganyika, kwa madai kwamba hayo yalikuwa matakwa ya wananchi. Mwasisi wa CCM na Serikali ya Muungano Mwalimu Nyerere aliwakalia kooni akidai hiyo haikuwa sera ya chama chake.
Katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, anaandika kwamba “Serikali haiwezi kwa hila za viongozi, ikapitisha bungeni sera iso na idhini ya Chama wala ya Umma.”
Pia anaandika kuwa “jambo hili ni lao tu, hawakutumwa na watu. Kama wanalo haraka, kusubiri wamechoka, basi wasiwe ajizi, waitishe uchaguzi, ufanywe hata mwakani, waliombee idhini.”
Zilikuwepo tetesi za kuwavua uanachama wabunge wote wa kundi la G55 kama wangeendelea kung’ang’ania hoja ya Serikali ya Tanganyika.
Ushahidi uliopo ni kwamba aliyekuwa katibu wa chama, Horace Kolimba na aliyekuwa kiongozi wa Serikali bungeni, Samwel Malecela walipoteza nyazifa zao kutokana na huo mtafaruku, na huo ndio ulikuwa mwisho wa hoja ya Serikali ya Tanganyika.
Lakini mfumo huu una hasara kuliko zilivyo faida. Tanzania tuna mtindo wa kofia mbili ambapo Rais wa nchi ndiye mwenyekiti wa chama, na mjumbe wa Kamati Kuu yenye uwezo wa kumvua mtu yeyote uanachama.
Viongozi wa juu wa Serikali wako katika Kamati Kuu pia. Uongozi wa Chama chini ya usukani wa Mwenyekiti wake unapokosa dira na kupoteza mwelekeo, moja kwa moja, Serikali ambayo inaongozwa na huyo mwenyekiti inazama. Kumbuka wosia kwamba Chama legelege huzaa Serikali legelege.
Katika uongozi wa namna hii wenye kasi isiyo na dira wala mwelekeo, kinga pekee ya kulinusuru taifa katika janga la kuzama ni kuwa na Bunge linaloweza kuirudisha Serikali katika mstari wake kwa niaba ya wananchi.
Lakini chini ya mfumo huu vyama vya siasa ndio waajiri wa wabunge hivyo wanalazimishwa kukubali maelekezo na kanuni za uongozi uliokosa dira na mwelekeo, ama sivyo vitumbua vyao vitaingia mchanga.
Hivyo, mshikamano wa wabunge na viongozi wao unakosa dira pia.
Mfano, katika kikao cha bunge cha mwaka 2006, Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM) alimlalamikia Waziri wa Miundombinu, Basili Mramba (CCM), kwa kujitengea bilioni 17 kujenga barabara ya Marangu-Tarakea yenye urefu wa kilomita 9, wakati barabara ya Nyakanazi-Sumbawanga yenye urefu wa kilomita zaidi ya 400, imetengewa shilingi milioni 300 tu.
Naye Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba (CCM), alisema Mramba alijiongezea sehemu nyingine ya barabara kutoka Rongai hadi Kamanga.
Lucas Selelii alipania kutounga mkono makadirio ya matumizi ya Wizara ya Miundo mbinu kwa madai kwamba, kipaumbele kilitakiwa kuwekwa kwenye barabara za kuunganisha mikoa badala ya kuunganisha kata.
Lakini suala lenyewe lilitatuliwa kwa mshikamano wa kichama na bajeti ikapita. Hapa ndipo linapoonekana kusudio la masharti yaliyowekwa kwenye katiba kwamba hayakuwa na lengo la kumdhibiti mgombea binafsi, bali kuwadhibiti wabunge, ili Serikali iweze kupitisha madudu yake bungeni.
Ibara ya 44 (d) ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010 imeongelea ujenzi wa barabara zote zilizoongelewa isipokuwa ile ya kutoka Rongai hadi Kamanga. Hivyo Lucas Selelii na John Komba walikuwa na haki ya kudai kile walichokiombea idhini kwa wananchi katika majimbo yao ya uchaguzi.
Waliokosa haki za kujengewa barabara sio mgombea binafsi, bali ni wananchi wa majimbo ya Mbinga na yale yanayounganishwa na barabara ya Nyakanazi- Sumbawanga.
Hakuna kitu kinaitwa mgombea binafsi, bali kuna kitu kinaitwa haki za raia na ndicho kilichofutwa.
Katika hali ya sasa, hakuna njia ambayo wabunge wanaweza kubishana na waajiri wao ambao ni viongozi wa vyama.
Kama Komba na Selelii wangeendeleza msimamo wao, wangeweza kufutwa uanachama kwa kukwamisha shughuli za chama bungeni, hivyo kupoteza nafasi zao za ubunge.
Lakini masharti haya yakiondolewa, wabunge mithili ya Komba na Selelii wanaweza kung’ang’ania msimamo wao wa kukirudisha chama kwenye msitari, kwani hata wakifutwa uanachama, hawapotezi viti vyao vya ubunge.
Dhana hii itawalazimisha viongozi wa vyama vya siasa kutekeleza yale waliyoyaombea kibali kutoka kwa wananchi. Kasoro kubwa katika mfumo wetu wa sasa ni uwezo ambao sio wa kikatiba walionao viongozi wachache wa vyama vya siasa wa kuwafuta kazi viongozi waliochaguliwa na wananchi.
Majuzi Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliposimamishwa na Bunge, vimekuwapo vilio kuwa wananchi wa Kigoma hawakutendewa haki.
Kamati Kuu ya CCM yenye watu wachache sana, tena ambao hawakuchaguliwa na wananchi, isipokuwa wanaCCM wenyewe, ikiamua kumfuta uanachama Rais aliyechaguliwa na mamilioni ya Watanzania, anapoteza kiti chake cha urais.
Au ikimfuta uanachama Mbunge aliyechaguliwa na maelfu ya Watanzania, naye anapoteza kiti chake cha Ubunge. Je, hii ni haki? Je, anayepoteza haki yake ni mgombea binafsi au ni wananchi waliopiga kura?
Je, tunahitaji kusubiri CCM ipate ndoto nzuri ya kubadilisha katiba ya namna hii ili wananchi warudishiwe haki zao zilizoporwa?Kutoka Raia Mwema wiki hii
No comments:
Post a Comment