Ufisadi unakomazwa na viongozi
walioko madarakani
Aristariko Konga
SUALA la ufisadi, kula mali za umma na mikataba isiyoeleweka, ni gumzo hapa nchini hivi sasa. Hakuna ubishi tena, kwamba kuna mtu ambaye anaweza kusema mambo yako shwari. Amkani si shwari tena. Wiki iliyopita, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Method Kilaini, alitoa maoni yake binafsi, kuhusu mambo hayo. Hebu fuatilia.
Askofu Methodius Kilaini |
“Ninakumbuka kuwa tulianza kulizungumzia suala la ufisadi tangu miaka ya 1990. Suala zima hili linahusu kula mali ya umma, kuwa na mikataba yenye mashaka na kila aina ya uovu katika kuendesha serikali yetu.
“Kwa hiyo, suala la ufisadi halikuanza hivi leo. Sisi tulianza kulijadili muda mrefu. Kelele zinazosikika hivi sasa zinaonyesha kuwa sasa tatizo limekuwa kubwa zaidi, kuliko wakati ule.
Tunao wajibu wa kuendelea kulipiga vita suala hili, ingawa vita yake ni ngumu sana.
“Kwa bahati mbaya sana tulipoachana na ujamaa, watu kadhaa, tena wachache wetu, wakajiingiza kwenye ufisadi. Mwanzo tulizungumzia rushwa ndogo ndogo, lakini hivi sasa imeshamiri rushwa kubwa, tena inayohusisha watu wachache… Watu wachache, rushwa kubwa.”
Askofu Kilaini anasema kwamba wakati wa uongozi wa Awamu ya Tatu, chini ya Rais Benjamin Mkapa, kwa kufuata falsafa yake ya Ukweli na Uwazi, nchi iliingia katika ufisadi wa kimataifa, yaani rushwa kubwa.
Kwamba, wawekezaji kutoka nje, wanapoingia hapa nchini, wanakuwa na lengo la kutafuta masoko ya vitu vyao.
Kwa hiyo hata wanapoingia mikataba na nchi, basi wanakuwa na lengo la kujinufaisha kwa kutafuta masoko yao.
“Sasa, unaposema kwamba ufisadi wa kimataifa una maana kwamba serikali za nje zinaingia kutafuta masoko hapa kwetu. Wanaingia mikataba na sisi, na mikataba yenyewe ina mashaka mashaka kwa upande wetu.”
Askofu anasema kwamba vita dhidi ya ufisadi wa kimataifa inakuwa ngumu sana kwa sababu utiaji wa mikataba yenyewe una usiri mkubwa, kiasi kwamba hata wale ambao wanatarajiwa kuwa wa kwanza kuupiga vita, wanashindwa kupata taarifa mapema kutokana na kificho hicho.
“Wale ambao wanapaswa kuwa wa kwanza kupiga vita suala hili, wanashindwa kupata taarifa na hata wanapokuja kuzipata, wanakuwa wamechelewa sana na mambo yamekwisha kufanyika na kuleta athari.”
Mara kadhaa wabunge wamekuwa wakilalamika ndani ya Bunge, kwamba mikataba hiyo ingekuwa inawekwa wazi mbele yao, lakini upande wa serikali umekuwa ukipinga dhana hiyo kwa madai kuwa mambo mengi ni ya siri baina ya wale wanaoingia kwenye makubaliano ya mkataba.
“Lakini pia mambo ya ufisadi yana usiri mkubwa kwa kuangalia mikataba ya makubaliano, kiasi kwamba wanaopaswa kukemea ubovu wa mikataba hii hawapati habari wala nafasi kutokana na usiri huu.
“Kutokana na usiri huu, kazi ya kupigana vita na ufisadi inakuwa ngumu sana. Hapa ndipo dhamira ya Rais (Jakaya) Kikwete inakuwa vigumu kutekelezeka,” anasema Askofu Kilaini.
Askofu Kilaini ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, la Kanisa Katoliki. Yeye ndiye namba mbili wa Mkuu wa Jimbo hilo, Polycarp Kardinali Pengo.
Kilaini anasema kwamba, ufisadi huu wa kimataifa (rushwa kubwa) unalindwa sana na viongozi walioko madarakani, kiasi kwamba mtu mdogo anapokuwa na ari ya kulinda maslahi ya taifa, hushurutishwa na wakubwa wake kwamba anapaswa kunyamaza na kuwasilikiza wao tu.
“Ufisadi wa kimataifa ambao ndio unaolisumbua taifa hivi sasa, unalindwa sana na walioko madarakani. Mtu akijaribu kuingilia kati anaambiwa ‘nyamaza’.
“Kwa hiyo serikali yetu ina kazi kubwa sana, na hasa Rais wetu Kikwete, ambaye ameonyesha moyo wa kutaka kupambana na tatizo hilo… Ana kazi kubwa kwa sababu kuna watu wanashirikiana na wawekezaji hawa wa nje ili kujinufaisha wao. Ni kazi ngumu sana kwake.”
Askofu Kilaini anasema kwamba pamoja na kwamba ufisadi wa kimataifa ulianza wakati wa Awamu ya Tatu, bado Mkapa alijitahidi kufungua milango ya uwekezaji kutoka nje.
Kwamba wawekezaji wa nje wanapokuja na vitu vyao pamoja na fedha, hutumia fedha hizo kuwanunua viongozi walioko madarakani, ambao ndio huingia katika duru za kusaini mikataba. Hapo ndipo hukubaliana na wageni hao, na kulisaliti taifa na watu wake.
“Wanakuja na vitu vyao na mapesa mengi sana.
Sasa wanapofika hapa wanayatumia mapesa haya kuwapa viongozi walioko madarakani. Viongozi wa aina hii, ambao ndio walipaswa kumsaidia Rais Kikwete, ndio hao hao wanakuwa wa kwanza kumkwamisha.
“Hao ndio wanaofanya dhamira nzuri ya Rais Kikwete, ya kupambana na rushwa hii kubwa, iwe ngumu kuitekeleza. Inabakia tu kusikia kelele za rushwa kwenye mahakama zetu hizi ndogo, ikiwahusu watu wadogo… Hii haitoshi.
“Tunashukuru kwamba Awamu ya Nne, chini ya Rais Kikwete, imeunda Kamati ya Kuchunguza Mikataba ya Madini. Tunashukuru kwamba kamati hiyo ina watu kutoka upinzani. Unajua kunapokuwa na watu wa upinzani kwenye kamati kama hiyo inakuwa rahisi kwetu sisi kujua kinachofanyika. Wanatuambia kinachofanyika.
“Kwa hiyo, kama ndani ya kamati (ya kuchunguza mikataba ya madini) kuna watu wanaotaka kuchukua fedha kutoka kwa wawekezaji hawa wa nje, ili mambo yafichwe, basi kwa vyovyote vile watashindwa. Walau kuna uwezo sasa kuuliza na kuambiwa kinachoendelea ndani ya kamati.”
Askofu Kilaini anasema kwamba wabunge wana wajibu wa kutetea maslahi ya taifa, na hasa kupiga vita ufisadi huu wa kimataifa. Kwamba wakilindana, mwishowe wajue nchi ikizama na wao watakuwamo.
“Wabunge wajue kuwa tukizama, basi tunazama wote… Wao wakilindana tutatokomea wote… Tunawasifu wale wote wanaokuja juu pale maslahi yetu yanapokuwa hatarini. Wale ambao bado wana ‘usisi’ waache na wawaige wenzao.
“Rais Kikwete ameonyesha moyo wa kukubali kuulizwa maswali magumu na kukubali kutafuta majibu ya maswali haya magumu. Kwa mfano, sisi wengine hatukutegemea kuona (Zitto Zuberi) Kabwe, ambaye alikuwa amepewa adhabu na Bunge, anakuwa kwenye Kamati ya Madini. Hatukutarajia kabisa.”
Zitto Kabwe, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, alisimamishwa ubunge Agosti mwaka huu, baada ya kuwasilisha hoja ya kutaka kupewa ukweli kuhusu mkataba wa uchimbaji madini eneo la Buzwagi, kanda ya Ziwa, ambao ulisainiwa London, Uingereza.
Baada ya hoja yake hiyo, iliibuka hoja nyingine inayopingana na hiyo, ikidai kuwa Zitto alikuwa akilidanganya Bunge, na hivyo kubebeshwa adhabu hiyo hadi Januari, mwakani.
Hata hivyo, Askofu Kilaini anasema kwamba vyama vya upinzani vinao wajibu wa kusema ukweli pale panapostahili, badala ya kutafuta hoja za kupinga tu.
“Vyama vya upinzani visijione kuwa vinatafuta hoja za kupinga tu. Wapinzani wanao wajibu pia wa kutafuta suluhu wakati matatizo yanapojitokeza. Wawe na uzalendo. Waweke mbele uzalendo kila yanapokuja maslahi ya kitaifa.”
Askofu Method Kilaini alizaliwa Machi 30, 1948, katika Parokia ya Katoma iliyopo katika Dayosisi ya Bukoba. Alipata upadirisho Machi 18, 1972.
Aliteuliwa kuwa Asofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam mnamo Januari 8, 2000, kisha kuwekwa wakfu Machi 18, 2000.Kutoka Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment