Wakenya wanasubiri mshindi.
HATIMAYE safari ndefu ya kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa nchini Kenya iliyoanza kwa kuzinduliwa rasmi kwa kampeni mapema Agosti, inakamilika kesho baada ya Wakenya zaidi ya milioni 14 kupiga kura ya kuchagua madiwani, wabunge na Rais.
Tayari Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) imetangaza kwamba kila kitu kipo tayari kwa ajili ya uchaguzi huo na kuwataka wapiga kura kuwasili katika vituo vya kupigia kura nchini kote kuanzia saa 12.00 asubuhi.
Kuanzia Alhamisi wiki iliyopita, Wakenya wameshuhudia kampeni nzito zikiendeshwa na wagombea urais watatu katika ngwe ya mwisho ya kusaka wapiga kura katika maeneo mbalimbali ambako walikuwa hawajafika kunadi sera zao katika kipindi chote cha karibu miezi minne ya kampeni.
Wagombea hao, Rais Mwai Kibaki wa Party of National Unity (PNU), Raila Odinga wa Orange Democratic Movement (ODM) na Stephen Kalonzo Musyoka (ODM Kenya), ndio wamekuwa wakiendesha kampeni nzito, wakati mwingine hadi usiku katika harakati zao za dakika za mwisho za kuwashawishi watu wawapigie kura.
Bado hali ni tata na wachunguzi wa masuala ya siasa hapa wanasema bado ni vigumu kubashiri ni yupi hasa anaweza kuibuka mshindi wa kiti cha urais, hasa kati ya Rais Kibaki, anayeungwa mkono na watu wengi kutoka kabila lake la Wakikuyu na Raila Odinga anayeungwa mkono na watu wa kabila lake la Waluo pamoja na makabila mengine mengi, makubwa kwa madogo.
Kama ilivyo kawaida kwa siasa za Kenya kuchukua mkondo wa kikabila, Kalonzo Musyoka pia anaungwa mkono na watu kutoka katika kabila lake la Wakamba wanaoishi katika sehemu kubwa ya Mkoa wa Mashariki.
Kwa bahati mbaya, makabila mengine kama Wameru wanaotoka katika Mkoa wa Mashariki, wanajisikia kuwa karibu zaidi na Wakikuyu na hivyo wanamuunga mkono Rais Kibaki.
Lakini sehemu kubwa ya makabila mengine kama Waluhya kutoka Mkoa wa Magharibi, Wamasai na Wakalenjin (Mkoa wa Bonde la Ufa ), Waborana (Mkoa wa Kaskazini Mashariki) na Wamijikenda kutoka Mkoa wa Pwani, wanaonekana kumuunga mkono Raila Odinga kutokana na kuanza kampeni za chini chini kabla ya wenzake wote kuanzia mwaka 2005. Pia anaungwa mkono na wakazi wengi wa Jiji la Nairobi , ikilinganishwa na Rais Kibaki na Kalonzo. Hii ni kwa mijibu wa kura za maoni zilizotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Raila amefanikiwa kuwanasa Waluhya, kabila la pili kwa ukubwa (idadi ya watu) nchini Kenya baada ya kumtangaza Musalia Mudavadi anayetoka katika kabila hilo , kuwa mgombea mwenza. Pia Raila amefanikiwa kuwanasa Wakalenjin wengi kutokana na hisia zao kuwa walinyanyaswa na kuonewa tangu serikali ya Rais Kibaki ilipoingia madarakani Januari 2003.
Lakini pamoja na kuungwa mkono na watu wa makabila mengine mengi, bado ushindani kati yake na Rais Kibaki ni mkubwa kutokana na idadi kubwa ya Wakikuyu ambao wamesambaa karibu katika kila kona ya Kenya na ambao kwa hakika lazima watampigia kura kiongozi kutoka kwao.
Rais Mwai Kibaki mwenye umri wa miaka 76 sasa, naye amekuwa halali usingizi na amekuwa akiendesha kampeni kwa nguvu kiasi cha kuwashangaza Wakenya wengi ambao hawajahi kumwona kiongozi wao akiwa na nguvu kiasi hiki.
Katika wiki ya mwisho, Kibaki amekuwa akihutubia mikutano ya hadhara kati ya minne mpaka sita kwa siku, huku akilazimika kwenda umbali wa mamia ya kilomita kila siku kuyafikia maeneo mbalimbali ya wapiga kura.
Wakati wa utawala wake, Wakenya walimzoea Rais Kibaki kama mtu mvivu asiyependa kujihangaisha kwa kuzungukia maeneo ya nchi (hata yenye matatizo), na badala yake akiacha kazi zote kwa mawaziri wake. Hata hivyo, baadhi waliihusisha hali hiyo na udhaifu wake kutokana na ajali aliyopata mwaka 2002 pamoja na umri wake mkubwa.
Lakini safari hii uvivu wote umemtoka na katika kipindi chote cha kampeni, alikuwa akichanja mbuga katika kila pembe ya nchi kutafuta nafasi nyingine ya kuongoza Kenya kwa kipindi cha miaka mitano.
Ikumbukwe pia kwamba kampeni za Rais Kibaki ndizo zinazoendeshwa kwa gharama kubwa kutokana na michango ya marafiki zake na hivi karibuni, Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya ilitoa taarifa inayosema kampeni za kumrejesha Kibaki madarakani zimetumia zaidi ya Sh milioni 600 za Kenya na kwamba sehemu ya fedha hizo zimechotwa kutoka hazina ya serikali (Sh milioni 139).
Kwa bahati mbaya hakukuwa na muda wa kujadili ripoti hiyo kutokana na kupamba moto kwa kampeni kwani hata wapinzani wake hawakuwa na muda wa kujadili kwa undani ripoti hiyo, wote wakiwa wamejikita zaidi katika ngwe ya mwisho ya kampeni.
Pamoja na kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kampeni, Rais Kibaki pia wiki inayokwisha aligundua njia nyingine ya kuwashawishi wapiga kura wa Kenya ; kugawa wilaya mpya.
Katika mikutano yake ya kampeni, Rais Kibaki amekuwa akigawa wilaya mpya kwa Wakenya kwa wingi kiasi cha kuwashtua hata wapinzani wake ambao wanawatahadharisha wananchi kuwa macho na ugawaji huo ambao wanaulinganisha na rushwa.
Akiwa katika Mkoa wa Nyanza eneo la Kisii, Rais Kibaki aliigawa wilaya hiyo ambayo hadi sasa bado haijapewa jina, baada ya wagombea ubunge kupitia chama chake cha PNU kumweleza kuwa wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakililia wilaya mpya tangu uhuru.
Katika Mkoa wa Bonde la Ufa , Kibaki pia ametangaza wilaya tatu mpya katika wiki ya mwisho ya kampeni. Hata hivyo, wapinzani wake wanasema ugawaji huo wa wilaya hautamsaidia kupata kura kwa kuwa mgawo anaoufanya huendani na fedha za kuanzishia miundombinu inayokwenda pamoja na uanzishwaji wa wilaya mpya.
Hata vyombo vya habari vya Kenya vimeshutumu hatua hiyo vikisema hailingani na mahitaji halisi ya wananchi wa Kenya na kwamba wilaya zinagawanywa kwa minajili ya kisiasa, hasa katika kipindi hiki cha kampeni. Katika kipindi chote cha kampeni, Rais Kibaki amegawa wilaya mpya zaidi ya 20.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wilaya zimeongezeka kutoka 50 zilizoachwa na utawala wa Rais Daniel arap Moi hadi kufikia 137 zilizopo leo wakati Wakenya wakijiandaa kupiga kura kuchagua serikali mpya kuingia madarakani hapo kesho.
Mashabiki wa Rais Kibaki wanaamini kuwa ugawaji huo wa wilaya utawasogeza viongozi wa serikali karibu zaidi na wananchi ili kuwatatulia matatizo yanayowakabili, na hivyo kuwashawishi wananchi waamue kumpigia kura.
Na wiki hii kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa kampeni, Rais Kibaki alihutubia mkutano pamoja na mtangulizi wake, Daniel arap Moi katika mji wa Baringo uliopo Mkoa wa Bonde la Ufa . Alikuwapo pia mgombea ubunge wa Baringo Kaskazini kwa tiketi ya Kanu, Gideon Moi, mtoto wa Mzee Moi.
Katika mkutano huo, Kibaki pia alitangaza kutoa wilaya mpya baada ya kupata maelezo kutoka kwa wagombea na rais mstaafu kuwa Wilaya ya Baringo ni kubwa mno inayotakiwa kugawanywa kwa kuwa inawawia vigumu viongozi waliopo kusimamia utawala. Moi kama kawaida yake, aliwataka wananchi wa Kenya kumchagua Rais Kibaki akisema wagombea wengine wameanzisha vyama vya kikabila.
Alidai pia kwamba rekodi ya maendeleo katika miaka mitano ya utawala wa Rais Kibaki, inatosha kuwafanya Wakenya wampigie kura ili akamilishe mipango mingi ambayo alipanga kuitekeleza lakini haijakamilika.
Katika kuhakikisha kuwa anamaliza nguvu za Raila katika Mkoa wa Bonde la Ufa , Moi amekuwa akitoa hadithi kadhaa za zamani zinazomhusisha na mambo mabaya, zikiwamo vurugu wakati wa sherehe ya kuapishwa kwa Rais Kibaki pamoja na kuhusika kwake katika njama za kutaka kuipindua serikali yake mapema mwaka 1982.
Hata hivyo, kama njia ya kukabiliana na hatua hii ya ugawaji wa wilaya mpya, katika mikutano yake ya kampeni, Raila Odinga amekuwa akiwaahidi wananchi kuwa iwapo atachaguliwa kuiongoza Kenya, atahakikisha kuwa majimbo yote yanageuzwa kuwa wilaya kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wake wa kuanzisha serikali ya majimbo.
Amekuwa akiwahamaisha Wakenya kumkataa Rais Kibaki akisema ni mtu ambaye haaminiki, akionya kuwa ahadi zote anazozitoa, hawezi kuzitekeleza na kwamba amethibitisha hivyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita alipopewa nafasi ya kuongoza nchi.
Haijulikani kama ni bahati mbaya au ni kwa makusudi, lakini vigogo wote wa kampeni ndani ya PNU hawajahi kumgusa Kalonzo Musyoka katika kampeni ama za kashfa au za kubeza sera zake. Pengine ni kutokana na kuamini kuwa si tishio kwa mgombea wao.
Lakini Kalonzo amekuwa akiwakumbusha wapiga kura katika mikutano yake ya kampeni kila siku kwamba muujiza utatokea na katika uchaguzi wa mwaka huu, atapita katikati ya Kibaki na Raila bila kuonekana na kuibuka. Hizo ndiyo tambo za hapa na hakuna ajuaye nani ataibuka mshindi na kama ugawaji wa wilaya mpya unaweza kusaidia kumrejeshea ushindi rais Kibaki. Wakenya na dunia nzima inasubiri matokeo kwa hamu.
Kutoka Raia Mwema, wiki ya 52 ya mwisho, mwaka 2007.
Viungo "links" na htt://watanzaniaoslo.blogspot.com
No comments:
Post a Comment