Jakaya Kikwete ajitosa Kenya
Mwandishi Wetu
HabariLeo; Tuesday,January 01, 2008 @19:01
Mwandishi Wetu
HabariLeo; Tuesday,January 01, 2008 @19:01
RAIS Jakaya Kikwete amesema Tanzania haiwezi kukaa kimya wakati nchi jirani ya Kenya ikiwa kwenye hali ya wasiwasi.
Wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo, watu kadhaa wanahofiwa kuuawa mjini Eldoret baada ya kushambuliwa na waandamanaji waliovamia kanisa na kulichoma moto, ikiwa ni sehemu ya machafuko yanayoendelea kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu.
Polisi wa Kenya wamethibitisha kuwa idadi ya waliokufa ni kati ya 35 na 40, wanawake na watoto. Watu hao, wengi wakiwa ni wanawake na watoto, walikuwa wameomba hifadhi ndani ya Kanisa la Kenya Assemblies of God, kabla ya kanisa hilo kuchomwa moto.
Wanawake na watoto hao walikuwa wanakimbia makazi yao ambayo yalichomwa moto mapema na washambuliaji hao. Chama cha Msalaba Mwekundu kimeeleza kuwa kimezidiwa na idadi ya majeruhi kutoka Eldoret.
Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ikimkariri Rais Kikwete jana, ilisema Rais alisisitiza haja ya wanasiasa nchini Kenya kuona umuhimu wa kukaa na kujadiliana ili kuiokoa hali mbaya iliyojitokeza nchini humo kutokana na ghasia na fujo zilizozuka baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa Desemba 27, mwaka jana.
Rais Kikwete alisema anajaribu kuwasiliana na viongozi mbalimbali wa kisiasa nchini Kenya na wa Serikali ya Uganda ili kuangalia njia zitakazotumika kupunguza hali ya vurugu iliyopo nchini humo. Hata hivyo, aliwataka Watanzania wanaoishi nchini humo kuchukua tahadhari.
Takribani watu 214 wameripotiwa kuuawa kutokana na mapambano kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga ushindi wa Rais Mwai Kibaki, 76, aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK).
Raila Odinga, 62, mwanasiasa aliyewahi kufungwa jela na pia kuwa katika Baraza la Mawaziri la Kibaki, aliongoza kwa siku za kwanza za matokeo rasmi ya kura kabla ya juzi kutangazwa kushindwa kwa tofauti ya kura 231,728 dhidi ya mkongwe huyo wa siasa za Kenya.
Katika uchaguzi huo uliozua mtafaruku ambao haujawahi kutokea katika historia ya Kenya, Rais Kibaki alitangazwa mshindi kwa kura 4,584,721 wakati mpinzani wake mkubwa, Odinga alipata kura 4,352,993.
Kutokana na vurugu hizo zilizosambaa katika miji na majiji, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani na Uingereza zimeingilia kati na kuelezea wasiwasi juu ya hatma ya nchi hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amevitaka vyama vya siasa kuondoa tofauti zao kwa njia ya mazungumzo na kuzingatia sheria. Pia ameyataka majeshi ya ulinzi kuheshimu haki za raia.
Kwa upande wa Marekani, imeondoa msimamo wa awali wa kumpongeza Kibaki baada ya kuwapo taarifa kuwa baadhi ya kura zilizohesabiwa, zimezidi idadi ya waliopiga.
“Kinachoonekana hapa, kuna matatizo makubwa ambayo yanahitaji utatuzi kulingana na katiba yao na mfumo wa sheria,” alisema Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Tom Casey. Aliongeza kuwa hawezi kutoa pongezi kwa mtu yeyote, kwa sababu kulikuwa na tatizo kubwa katika kuhesabu kura.
Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya, pia walielezea kutokuridhishwa na mchakato wa kura baada ya kusema kuwa katika baadhi ya majimbo, yakiwamo Molo na Kieni, matokeo yaliyotangazwa hayaendani na idadi ya wapiga kura.
Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, amewasiliana kwa simu na Rais Kibaki na mpinzani wake, Odinga, akitaka kufahamu ni namna gani wanashughulikia machafuko yanayoendelea nchini hapa.
Pia Brown amewataka viongozi hao kushirikiana na kuafikiana katika kuleta amani. "Akizungumza na wote, Waziri Mkuu wa Uingereza alielezea namna anavyoguswa na uchaguzi wa Kenya, na zaidi aliwataka wote kushirikiana na kuwa na mashauriano,” ilisema taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Odinga amesema yuko tayari kukutana na Rais Kibaki kwa sharti la rais huyo kukubali kwanza kuwa yeye (Odinga) ndiye aliyeshinda katika uchaguzi huo. Odinga, ambaye ameitisha mkutano utakaofanyika kesho katika viwanja vya Uhuru Park, jijini hapa, anaendelea kusisitiza kutokuutambua ushindi wa Kibaki huku akimlinganisha na mtawala dikteta anayejipatia madaraka kwa mtutu wa bunduki.
Kauli hiyo ya Odinga ya kukutana na Kibaki kwa masharti, inazingatia mwito uliotolewa na watu mbalimbali, zikiwamo taasisi za kimataifa zinazowataka Kibaki na Odinga kuingia majadiliano ya amani ili kunusuru nchi hiyo na machafuko yanayoendelea.
Katika ujumbe wake wa Mwaka Mpya, Kibaki alielezea utayari wake wa kufanya mazungumzo, lakini akatahadharisha kuwa serikali yake itahakikisha kuwa inawadhibiti kikamilifu wale wanaovunja amani.
Licha ya wasiwasi kutanda kwa raia wa nje waishio nchini humo, pia umetanda kwa Wakenya waishio nje wakihofia usalama wa ndugu zao. Baadhi walikaririwa wakielezea ujumbe wa simu unaolinganisha machafuko hayo na yale ya Irak.
Machafuko hayo yametajwa kuathiri uchumi kwa kiwango kikubwa baada ya mashine za kuchukulia fedha (ATM) zote kutokuwa na fedha, hali ambayo imeathiri wageni na watalii waliomo nchini humo.
Wakati takribani wageni 290, 000 huingia nchini humo kila mwaka kati ya Januari na Februari, baadhi ya watalii walikaririwa na vyombo vya habari wakielezea ugumu wa kusafiri kutoka Nairobi kwenda Mombasa kutokana na hofu ya vurugu.
No comments:
Post a Comment