* Watu 124 wauwawa kwa kupigwa risasi
* Miili yatapakaa mitaani Nairobi, Kisumu
* Wanajeshi wapelekwa kuongeza nguvu
* Wananchi Kisumu wakabiliwa na njaa
Tausi Mbowe na Mashirika ya Habari
Jamaa akipewa mkong´oto na askari wa kuzuia fujo wa Kenya, GSU (General Service Unit)
ZAIDI ya watu 124 wameripotiwa kuuawa na polisi katika vurugu zinazoendelea nchini Kenya kufuatia wananchi kupinga matokeo ya kura za urais yaliompa ushindi Rais Mwai Kibaki kuendelea kutawala nchi hiyo katika kipindi cha pili cha miaka mitano.
Mbali na kuuawa kwa wananchi hao pia familia zaidi ya 100 hazina mahali pa kukaa kufuatia nyumba zao kuchomwa moto muda mfupi baada ya Rais Kibaki kuapishwa kwenye viwanja vya Ikulu, jijini Nairobi juzi.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), zaidi ya watu 124 wamefariki dunia kutokana na vurugu hizo katika maeneo mbalimbli ya Jiji la Nairobi, Kisumu, Eldoret, Korogocho, Bugoma, Busia, Kakamega na Kericho.
Katika kukabilina na vurugu zinazoendelea katika eneo la Kisumu, askari wa Jeshi la Kenya jana walipelekwa kwa helkopta kwenda kuongeza nguvu.
Wakati wa kurejudi Nairobi helkopta hiyo ya jeshi iliwabeba askari waliojeruhiwa kwenye mapigano hayo.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) pia liliripoti jana kuwa jumla ya miili 40 imehifadhiwa katika hospitali ya Nyanza iliyopo mjini Kisumu huku ikiwa na majereha ya risasi.
Jana hali katika Jiji la Nairobi ilikuwa ya hatari hasa katika eneo la Kibera kutokana na wananchi kupambana na askari waliokuwa wakitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya bila mafanikio. Kitendo cha awananchi kukaidi amri ya polisi hao kiliwafanya askari hao kuanza kutumia risasi za moto na hatimaye kuua na kujeruhi wananchi kadhaa.
Katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo na vitongoji vyake askari wa kutuliza ghasia (GSU), walionekana katika magari huku wengine wakiwa kwenye makundi katika juhudi zao za kutuliza ghasia na hata watembea kwa mguu hawakuruhusiwa kuingia mitaa ya jijini ambako Raila Odinga alikuwa afanye mkutano wa hadhara.
Mapema jana asubuhi, polisi ilitoa onyo kwa wakazi wa Nairobi kwamba kama wangehudhuria mkutano wa Raila wangewaua kwa kupigwa risasi.
Kufuatia vurugu hizo shughuli za kibiashara nyingi zilikuwa zimefungwa huku baadhi ya watu walioneka kupora vitu mbalimbali kama vile televisheni, jenereta, baiskeli na radio kutoka kwenye maduka ambayo wenyewe walikuwa wameyafunga kutokana na vurugu hizo.
Katika eneo la Kibera, wananchi walichoma Soko la Toi na magari kadhaa yaliyokuwa yameegeshwa katika jiji la Nairobi, Kisumu na Mombasa pia yalichomwa moto.
"Bila Raila, hakuna amani " walisikika baadhi ya wafuasi wa ODM katika maeneo ya Kibera ambako wanaishi watu wa kipato cha chini. Katika eneo hilo hali ilikuwa mbaya sana wananchi walikuwa wakichoma vituo vya mafuta huku askari wakiwatawanya kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.
Katika mji wa Mombasa vijana walifunga barabara zote za kufika uwanja wa ndege na kusababisha mtafaruku mkubwa wa watalii na abiria ambao walikuwa wakienda katika uwanja huo kwa ajili ya safari zao.
Vijana hao waliokuwa wameteka barabara hizo walikuwa na silaha mbalimbali ambazo walizitumia kuharibu mali mbalimbali pembezoni mwa barabara hizo, huku polisi wakijaribu kuwadhibiti bila mafanikio.
Watu walioshuhudia ghasia hizo walisema kuwa polisi walirusha risasi za moto baada ya wananchi kuanza kuwarushia mawe.
Hata hivyo, wafuasi wa Odinga jana walishindwa kufanya mkutano uliodaiwa kutaka kumtangaza kuwa mshindi wa kiti cha urais badala ya Rais Kibaki baada ya Jeshi la Polisi nchini humo kuupiga marufuku mkutano huo uliopangwa kufanyika katika Uwanja wa Uhuru Park.
Awali wafuasi hao waliandamana kwa lengo la kufanya mkutano huo, lakini jeshi la polisi lilifanikiwa kuwadhibiti kwa kuwarushia mabomu ya machozi na kuwafanya washindwe kufika kwenye eneo ambalo walipanga kufanya mkutano huo.
Vyombo vya habari vya nchi hiyo jana vilishindwa kuonyesha matukio hayo huku vituo vya televisioni vikionyesha picha za katuni na radio kupiga mziki kutwa nzima baada ya Waziri wa Ulinzi, John Mishuki kutangaza amri ya kuzuia televisheni zote kurusha moja kwa moja matukio ya vurugu katika maeneo mbalimbali nchini humo juzi.
Wakati hayo yakitokea, Odinga kesho kutwa ameitisha maandamano ya amani kesho kutwa kulaani kitendo kilichofaanywa na serikali kumpokonya ushindi.
"Tunaitisha maandamano nchi nzima kwa mujibu wa katiba ya Kenya kwa lengo la kupinga Rais Kibaki kutangazwa mshindi," alisema Odinga wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Raila alisema kuwa hayuko tayari kuwa na mazungumzo yoyote na Rais Kibaki kufuatia matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi.
Alisema matokeo ya kura za rais Kibaki hayakuwa sahihi hasa katika mikoa ya Pwani, Nyanda za Juu Mashariki na eneo la Magharibi na kwamba kura alizopata haziwezi kumwezesha kuongoza nchi.
Pia alimlaumuWaziri Michuki kwa kutumia mabavu kupiga marufuku vyombo vya habari kutangaza moja kwa majo matukio ya vurugu zinaendelea nchini humo.
Tayari waangalizi wa Kimataifa kutoka Jumuhiya ya ya Ulaya walisema matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (ECK) yana kasoro nyingi
Mkuu wa Waangalizi hao, Alexander Graf Lambsdorff aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa utangazaji wa matokeo hayo ulikuwa na kasoro kubwa.
Hata hivyo, wakati waangalizi hao wakikosoa matokeo hayo, Marekani imekuwa nchi ya kwanza kutuma salamu za pongezi kwa rais Kibaki kufuatia kutangazwa kuendelea kuiongoza nchi hiyo.
Balozi Marekani nchini humo alimtaka Odinga kuacha kuhamasisha vurugu badala yake afuate taratibu za kisheria kupinga matokeo hayo ili kudumisha amani nchini humo.
katka kuunga mkono hoja hiyo mabalozi wa nchi za nje nchini Kenya walikutana jana na kutoa tamko la kumtaka Odinga kupinga matokeo hayo mahakamani.
hata hivyo Odinga alidai kuwa hakuna tofauti kati ya Rais Kibaki na dikiteta wa kijeshi akimfananisha kiongozi huyo na dikteta anayetumia silaha kujipatia madaraka.
Wakati huo huo viongozi wa dini nchini humo wamewataka viongozi wa wa kisiasa kuzungumza na wananchi ili wawe watulivu ili kurejesha amani na kujenga uchumi wa Kenya.
Naye aliyekuwa mgombea wa urais aliye shika nafasi ya tatu kupitia ODM-K, Stephen Kalonzo Musyoka amewaomba wananchi kuwa watulivu ili kuresha amani nchini humo.
Katika hatua nyinigne, njaa imeripotiwa kuukumba mji wa Kisumu ambapo jana wakazi wake walionekana wakihaha kutafuta chakula baada maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula kufungwa kwa siku mbili mfululizo na katika baadhi ya maeneo ambako kulikuwa na chakula kiliuzwa kwa bei ya juu.
No comments:
Post a Comment