Sunday, January 06, 2008

Kenya mnakula bila kunawa?

Mzee wa Kujitoa.

UUUWI! Hii aibu itaendelea hadi lini huku Afrika? Nasema msijidai hamjui yanayotokea hapo kwa ndugu zetu wajukuu wa Nyayo. Eti ni utamu wa madaraka au ni mapenzi kwa nchi yao? Watu wanapigania kuingia Ikulu kwa gharama ya damu? Tumefika mbali nawaapia.

Mbona tulidhani tumeshapata somo la kutosha kule Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari? Eti kwa mawazo yenu ukimwi hautoshi kunyofoa roho za watu hadi ifikie mahala pa kutumia marungu, sime na baruti? Imefikia mahali mnakuwa wanyama kuliko wanyama wenyewe? Nasema hii ni aibu kwa Afrika yote. Si mnajua hao wakubwa wa Ulaya siku zote wanadhani akili zetu ni nyeusi kama ngozi zetu? Mbona mnawapa ushahidi wa bure jamani? Huko simo mtoto wa mama.

Waswahii wanasema mwenzio akinyolewa wewe tia maji. Mwadhani yanayotokea hapo kwa majirani zetu hayawezi kutukuta na siye kama tusipokuwa waadilifu?

Kwani kuna aliyewadanganya au ninyi mnampikia Mola chai hadi mdhani hiyo laana haiwezi kutufika? Mwadhani wananchi wakichoka wanakuwaje? Kama mlikuwa hamjui nguvu ya umma sasa muitazame hapo kwa wajukuu wa Kenyatta. Nijitoe katika hili maana huko simo, tena simo kabisa.

Eti Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi anakiri hadharani hana hakika mshindi ni nani? Nakuapia hayo ni ya Firauni maana ya Musa yana afadhali.

Kumbe alikuwa akitangaza matokeo gani? Wazushi washaanza kuzusha eti kuna kura nyingine zilikuwa fotokopi! Mzee Moi yule anayeitwa profesa wa siasa alishindwaje kusaidia mambo wakati maji yalipoonekana dhahiri yanazidi unga?

Lakini mwaweza kutuambia huko Ikulu kunani hadi hata damu ya watu kumwagika kwa ajili ya tamaa zenu za madaraka? Mmesahahu kwamba sauti ya watu ni sauti ya Mungu? Nawaambieni safari hii mmekutana na mkwe mkiwa uchi! Huko miye nishasema wala simo kabisa.

Eti na Tanzania mwadhani 2010 iko mbali? Nawaambia sitaki kuitwa mchochezi, lakini mjifunze gharama ya kudanganya ni kitu gani. Kuna aliyewadanganya watu wanaweza kudanganywa wakati wote? Nawaambia umma ukichoka hakuna cha risasi za moto wala mabomu ya machozi! Kazi kwenu ili wasije wakawachoka maana ile zomea-zomea ya mwaka jana haitoi picha nzuri. Nijitoe katika hilo.

Eti katika mazingira haya ndio mlikuwa mnatushawishi tuharakishe mchakato wa kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki?

Mmesahahu hao Wakenya ndio walikuwa nambari wani wakisema tufanye haraka ili tuwe shirikisho chini ya rais mmoja?

Wameshindwa kuachiana madaraka wenyewe kwa wenyewe, wataweza kuwaachia Watizedi au Wanyankole?

Nasema afadhali wengi walisema tuende taratibu maana kama ndiyo haya mambo ya Wajaluo na Wakikuyu, hilo shirikisho lina safari ndefu nawaapia. Kama kawa huko miye wala simo.

Na hiyo Jumuiya ya Afrika Mashariki inafanya nini kwa huyo patna wetu? Nasikia Museveni tayari keshatoa zake pongezi! Eti katika mazingira ambayo hata Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi hajui mshindi ni nani kuna busara kutuma pongezi?

Pongezi kwa lipi hasa? Kuweza kung’ang’ania madaraka au kwamba hao waliokufa walikuwa wanastahili kifo? Mwanangu Afrika inashangaza. Nisipojitoa katika hilo nitafanyaje miye?

Jumuiya ya Afrika Mashariki si ina taasisi zake? Kama kumbukumbu zangu hazina makengeza, nadhani tuna hadi Bunge la Afrika Mashariki.

Hawajaona umuhimu kutoa tamko lao? Na hiyo sekretarieti ya jumuiya haidhani ina wajibu japo wa kimaadili kuingilia kati? Au hayo mwayaita kuingilia mambo ya watu?

Kumbe jumuiya tunaungana katika yapi hasa kama si pamoja na haya ya kuondoa siasa mwitu? Mwataka tuamini jumuiya ni kwenye mambo ya soko tu siyo?

Mwataka kuleta mambo ya “diplomasia” kwenye ujambazi? Watu watoane roho bado ninyi hamuoni huo ni ujambazi? Mbona mlipaswa kukemea bila kutafuna maneno? Huko mimi wala simo mwanangu.

Eti urais gharama yake ni damu? Kwani ukikubali kushindwa kwani kiama kinafika? Ustaarabu ni upi zaidi ya kukubali demokrasia ya wengi wape?

Kama mnaingia kwenye uchaguzi mkiwa na matokeo ya kura sasa uchaguzi wa kazi gani? Mtaacha lini viini macho wajameni? Nawashauri Wazanzibari waende Kenya wakawafunze namna ya kufikia muafaka wakati kuna matokeo yenye utata.

Mmesahahu hao ndugu zetu wa visiwani ni mabingwa wa matokeo yenye utata? Wanaweza kuwapelekea nakala mojawapo ya “miafaka” waliyoingia. Nijitoe katika hilo kukingali mapema mtu wangu.

Hivi hao wanaopigana lengo lao ni kujenga nchi hiyo hiyo au kuna nchi tofauti? Kwa nini kupigania fito ikiwa wote mwajenga nyumba moja bandugu?

Tukidhani kwamba hapo kuna ishu ya maslahi binafsi mtatuona wabaya wanakwetu? Nani kawaambia mjiapize kwamba lazima mshinde kwenye uchaguzi?

Kwa nini msijifunze kwetu watizedi namna tunavyoachiana Ikulu kwa staha? Si mnakumbuka tangu Nyerere hadi sasa anaingia Braza JK hatujawahi kutoana ngeu kwa ajili ya hiyo ofisi ambayo ni msalaba?

Kwa nini mwataka Kenyatta ageuke huko kaburini mlikomzika? Miye lazima nikimbie mbio katika hilo. Simo, tena simo kabisa.

Mbona mnafikia mahali mnatufanya tutamani Wazungu warudi kututawala? Eti wale babu zenu waliopigana maumau ili kuwaweka huru mnataka kuwapa ujumbe gani?

Mwadhani walipigania uhuru ili ninyi mje mpiganie Ikulu? Acheni za kuleta nawaambia. Eti hata hamna huruma kwa watoto na mama zao?

Si tumesikia hadi nyumba za ibada kwenu haziwatishi ndio maana mkatia kiberiti? Kuna kufuru kuliko hiyo? Nijitoe haraka maana machozi yangu kama kawaida yapo karibu sana. Simo tena simo kabisa!

kevinmakyao@hotmail.com
0784 265072

Kutoka Tanzania Daima.

No comments: