Wednesday, January 09, 2008

Membe afafanua safari za Kikwete..



WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema ataandaa orodha ya safari za marais wa nchi za Afrika na gharama zao ili Watanzania waweze kulinganisha na safari zinazofanywa na Rais Jakaya Kikwete.

Kauli hiyo ya Membe inatokana na wadau mbalimbali kudai Rais Jakaya Kikwete amekuwa akifanya ziara nyingi nje ya nchi pamoja na kuongozana na ujumbe mkubwa unaogharimu taifa fedha nyingi.

Akizungumza juzi Dar es Salaam katika kipindi cha 'Hamza Kassongo Hour', kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten, alisema safari za Rais Kikwete ni chache na zenye tija kiuchumi ikilinganishwa na viongozi wengine wa nchi za Afrika.

Alisema si sahihi kulinganisha safari zinazofanywa na Rais Kikwete na marais waliotangulia kwa sababu dunia hivi sasa imebadilika na Tanzania inapaswa itafute wawekezaji kwa lengo la kukuza uchumi.

"Huwezi kulinganisha safari za marais waliotangulia na rais wa sasa, kwani dunia hivi sasa imeendelea na inahitaji rais mwenye kutafuta wawekezaji kukuza uchumi wa nchi yake," alisema Membe.

Alisema iwapo Rais Kikwete hatofanya safari hizo, maisha ya Watanzania na uchumi wa nchi utakuwa mbaya zaidi kuliko ilivyo hivi sasa na nchi itakuwa tegemezi kwa kila kitu.
"Nchi kama Afrika Kusini na Uganda ambazo uchumi wao unakua vizuri kila kukicha viongozi wao wapo safarini kutafuta wawekezaji, sasa iweje sisi wenye uchumi mdogo Rais wetu asiwe na safari nyingi za kutafuta wawekezaji?" alihoji Membe.

Kuhusu ukubwa wa baraza la mawaziri alisema si hoja bali subira ya Watanzania inahitajika zaidi ili matunda ya kazi zinazofanywa na mawaziri hao zionekane baada ya miaka mitano.

Tangu kuingia madarakani kwa Rais Kikwete miaka miwili iliyopita kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kuwa Rais amekuwa akifanya safari nyingi zisizokuwa na tija kwa taifa sanjari na kusafiri na ujumbe mkubwa.Habari hii na Salehe Mohamed, picha na Chacha. DC


No comments: