Barua ya wazi kwa
Balozi wa
Marekani nchini
M. M. Mwanakijiji
Mhe. Balozi,
SAA chache zijazo, Rais wa Marekani, George W. Bush, atafanya ziara yake ya kwanza na pengine ya mwisho kama Rais wa Marekani nchini Tanzania.
Tunaposubiri kwa hamu ujio wa Rais Bush, ninajikuta nikiwa nimegubikwa na hisia ya uharaka na hofu. Hivyo kwa namna moja natumaini kuwa barua yangu hii itafanya sauti za Watanzania wengi walioko nyumbani na nje ya nchi isikike wakati wa ziara hii. Bila ya shaka, sauti za viongozi wetu pia zitasikika.
Matukio ya kisiasa hivi karibuni nchini, matukio ambayo yalisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na hatimaye kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri ni ishara ya wazi kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto ambazo zinatisha mwelekeo wake kitaifa kuelekea mafanikio ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na ambayo kama hayatakabiliwa kwa nguvu zote, basi yanaleta kiza katika mafanikio ya wananchi wa taifa hili.
Mhe. Balozi, Tanzania iko kwenye kizingiti cha mafanikio na watu wake wamepiga kambi kwenye malango ya mafanikio. Hata hivyo, ndoto yao hiyo ya kuweza kupata maisha ya mafanikio ya mali, utulivu wa kisiasa, na neema ya mtu mmoja mmoja, kila siku inatishiwa kiasi kwamba kunaifanya ndoto hiyo kuwa ngumu kutimilika.
Kashfa ya Kampuni ya Richmond Development Company (RDC), ni mfano dhahiri wa changamoto hizo ambazo Tanzania kama taifa inakutana nazo.
RDC, kampuni ya Kimarekani, bila huruma ilitumia matatizo na majanga yetu kama nafasi pevu ya kuweza kujitajirisha kwa kutumia maumivu ya Watanzania wakati ule tulipokuwa na ukosefu mkubwa wa nishati.
Kampuni hii ilijifanya imekuja kutuokoa kwa kutuahidi kutuletea majenereta ya kuzalishia umeme. Leo hii tumekuja kutambua kupitia ripoti ya Bunge kuwa, huu ulikuwa ni ulaghai mkubwa zaidi dhidi ya nchi yetu.
Kwa upande mwingine, viongozi wetu ambao tuliwaamini kuwa wanapofanya kazi zao wanaweka maslahi ya Watanzania na nchi mbele, wao pia imethibitika kuwa wametuangusha na kuisaliti kabisa imani hiyo. Wametuchukulia “sisi wananchi” bila ya kutujali na kwa msaada wa hiyo kampuni ya Kimarekani, kusababisha upotevu wa mabilioni ya shilingi ambayo kwa hakika yangeweza kutumika kwenye miradi mingi ya maendeleo nchini.
Mhe. Balozi, ninafahamu jinsi ambavyo wewe binafsi unaguswa na matatizo ya VVU/ukimwi na matatizo mengine ya kijamii. Bila ya shaka unaweza kujikuta unakatishwa tamaa na matukio ya kifisadi kama yaliyothibitishwa wiki iliyopita.
Inawezekana vipi taifa masikini kama la kwetu kuweza kupoteza mamilioni ya fedha namna hii? Sina uhakika ni kwa kiasi gani serikali yako ilitoa msaada kwa Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe. Kwenye ripoti nimeona mahali ambako wanasema waliwaandikia kuhusu Richmond, lakini sijaona jibu lenu lilikuwa ni nini?
Kama walipewa msaada tunashukuru, kama la, basi tunatumaini kuwa ziara hii ya Rais Bush itakuwa ni kichocheo cha kutoa msaada huo.
Marekani inayo sheria inayokataza makampuni ya Kimarekani kutoa rushwa au kufanya mambo ya kifisadi katika nchi za kigeni, sheria ambayo inajulikana kama Foreign Anti-Bribery and Corruption Practices ya mwaka 1998. Tunaamini kuwa sheria hii inaweza kutumika kuichunguza kampuni hii ya Richmond na mahusiano yake na viongozi wetu wa serikali.
Kabla ya hapo, kampuni hii ilipewa tenda ya kutandaza bomba la mafuta toka Dar hadi Mwanza umbali wa karibu kilometa 1,200 hivi. Tenda hiyo, kampuni hiyo ilipewa kwa upendeleo maalum.
Kabla ya RDC kupewa tenda hiyo, kampuni ya Kitanzania ya Africommerce ilifanya upembuzi yakinifu na ilikuwa tayari imeshatumia kiasi kikubwa cha fedha kujiandaa na mradi huo. Hata hivyo, kwa namna ambayo wachache wanafahamu, mradi huo wa Africommerce ulinyang’anywa na kupewa RDC ambao walishindwa na baadaye kuhamishiwa kwa kampuni toka Uarabuni.
Hata hivyo, cha kushangaza zaidi ni pale ambako mwezi mmoja baadaye kampuni iliyoshindwa hata kutandaza bomba moja au kufyeka nyasi ikajikuta inapewa mradi mwingine wa nishati na watu wa wizara ile ile. Hilo liliwezekana vipi?
Balozi, miezi sita ambayo umekuwepo nchini Tanzania, bila ya shaka umeweza kuona tofauti kubwa ya maisha ya wananchi wetu. Nina uhakika katika pita pita yako ya kuzunguka mitaa ya Dar au nje ya Dar, umeweza kuona tofauti ya hali ya maisha kati ya makundi makubwa ya watu.
Upande mmoja kuna wale ambao kutokana na nafasi zao serikalini au kwenye chama tawala au wenye mahusiano na wakubwa wa chama na serikali wamejikuta wakiishi maisha ya anasa. Watu hawa siyo tu wanaishi maisha ya anasa bali “anasa” ndilo jina la ubini wao.
Upande mwingine bila ya shaka utakuwa umeona ufukara na umasikini uliokithiri kati ya Watanzania. Hauhitaji kwenda mbali na Dar kuweza kuiona tofauti hiyo. Bila ya shaka unashangaa inawezekana vipi kuwa na pande mbili zilizo tofauti kiasi hiki.
Tofauti ambazo zinaonyesha jinsi ilivyo rahisi kwa watu wengine kutajirika na kupata unafuu wa maisha, huku watu wengine wakiwa wamefungiwa milango ya mafanikio hayo. Bila ya shaka kashfa za fedha za hivi karibuni nchini zinaweza kuwa zimekupatia dokezo la nini kinaendelea nchini.
Watumishi wabovu serikalini ndio tatizo kubwa zaidi ambalo Tanzania kama taifa linakabiliana nalo. Nafahamu kuwa hata Marekani tatizo la ufisadi wa viongozi si jambo geni, lakini ninyi wenzetu hamuwaonei haya watendaji wabovu kwani mnathubutu hata kusweka lupango maseneta, wawakilishi au watendaji wengine. Mnazo njia nyingi za kuwashughulikia viongozi mafisadi, iwe kwenye serikali za mitaa, za majimbo au za shirikisho lenu.
Bila ya shaka uliweza kuona au hata kusikia sauti za furaha na shangwe katika mitaa ya Jiji la Dar kufuatia kujiuzulu na hatimaye kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri. Sauti za vigelele, makofi na honi za magari ni ishara ya jinsi gani Watanzania wanasubiri mabadiliko ya viongozi wao.
Hisia hiyo ya mtu kujiona unathaminiwa na serikali yako na kwamba kweli inakusikiliza si mali ya Wamarekani peke yao au tunu wa Waulaya. Wananchi wa Tanzania nao wanaona kuwa wanayo haki ya kusikilizwa na kupatiwa viongozi bora, siyo tu wanaona hivyo bali wanadai hivyo.
Mhe. Balozi, wewe si mgeni katika eneo hili la Afrika ya Mashariki. Umeshaishi hapa na umefanya shughuli mbalimbali, hivyo kwa namna moja unaelewa nini kinachoendelea. Unaweza kuwa umeona mafanikio ambayo tumeyapata hadi hivi sasa na kwa hakika unaweza kuona ni jinsi gani mafanikio hayo ni kidogo na ambayo yana mipaka. Matukio ya umwagaji damu nchini Kenya bila ya shaka yamekuumiza moyo kwani ulishawahi kuishi nchini humo miaka ya sabini.
Kwa upande wa Tanzania, hata hivyo kashfa ya Benki Kuu na hii ya Richmond bila ya shaka inaweza kukushangaza vimewezekana vipi. Hata zile kashfa nyingine kama ya ndege ya rais, rada na machimbo ya Kiwira, zote zinapiga kelele kuwa Tanzania inahitaji viongozi wawajibikaji.
Mhe. Balozi, wasifu wako unaonyesha kuwa ulishiriki kwa karibu katika kubuni na kuanzishwa kwa Akaunti ya Changamoto ya Milenia ambayo “ni jitihada za Marekani kwa nchi zinazoendelea na ambazo zinafanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.”
Pia umeshiriki kwa kiasi kikubwa katika jitihada za Marekani kusaidia nchi masikini kukabiliana na janga la ukimwi. Hapa Tanzania juhudi hizo zinafahamika wazi. Katika jitihada hizo Marekani imekuwa ikimwaga fedha nyingi katika miradi mbalimbali na kwa serikali ambazo zinaonyesha jitihada ya kukabiliana na matatizo hayo.
Hata hivyo, kuendelea kumwaga fedha nyingi bila ya kutengeneza taratibu na njia nzuri ya kuzisimamia ni sawa sawa na kujaribu kujaza maji kwenye “mabirika yaliyovunjika”. Kuendelea kutupatia mabilioni ya fedha bila kuhakikisha zinasimamiwa vizuri hakusaidii matatizo yetu na ufisadi bali kunaongezea. Miaka thelathini iliyopita kiasi cha dola bilioni 2 zimetolewa na wahisani mbalimbali kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hata hivyo, ndani ya miaka kumi tu iliyopita, Tanzania imepoteza dola bilioni moja kutoka taasisi moja tu ya Benki Kuu kwa njia za udanganyifu, wizi, na ubadhirifu.
Katika ziara hii ya Rais Bush, kuna makubaliano na mikataba kadhaa ambayo itatiwa sahihi. Makubaliano hayo yataendeleza utamaduni wa kumwaga fedha nyingi Tanzania bila kuweka njia zinazoeleweka na za wazi za kusimamia fedha hizo. Swali ambalo wengi tunajiuliza ni kuwa ni kwa muda gani jumuiya ya wafadhili wataendelea kutoa fedha nyingi bila kuweka masharti ya jinsi gani fedha hizo zinasimamiwa? Kwanini wasitumie kiasi kidogo cha fedha kutujengea miundombinu ya usimamizi mzuri wa fedha za serikali badala ya kuendelea kumwaga fedha ambazo zinaishia mikononi mwa watu wachache?
Ni ombi langu na bila ya shaka nawakilisha mawazo ya Watanzania wengine kuwa, badala ya kuendelea kutupatia fedha nyingi zisizo na usimamizi mzuri, wakati umefika kwa serikali yako kuanza kudai Tanzania ifanye mabadiliko ya sheria yake ya fedha, ile ya manunuzi ya serikali na pia kutengeneza vyombo ambavyo vitahakikisha kuwa fedha za umma zinalindwa na wale wote wanaozifuja kukabiliana na mkono wenye nguvu wa sheria.
Kabla hamjatoa fedha zile za milenia na nyingine, itakuwa vizuri kama mtaitaka Serikali ya Tanzania kufanya mabadiliko makubwa katika utendaji wake hususan kwenye masuala ya rushwa, mikakati ya kukabiliana na ufisadi, na kuhusika kwa viongozi wa umma na vitendo vya ubadhirifu. Mnao uzoefu mkubwa katika maeneo hayo.
Pia naomba serikali yako kupitia wizara yake ya sheria ianzishe uchunguzi wa Kampuni ya Richmond ya mjini Houston ili kuona kama kampuni hiyo imevunja sheria ile inayokataza rushwa katika nchi za kigeni.
Mhe. Balozi, kile ambacho kampuni hii ilifanya kingeweza kusababisha matatizo makubwa ya kijamii na kisiasa nchini. Hali ya wasiwasi na ya kutojua nini kinafuatia baada ya kujiuzulu Waziri Mkuu kwenye nchi nyingine kunaweza kusababisha machafuko ya kisiasa. Tukiangalia yanayotokea kwa majirani zetu kaskazini, tunaweza kuona kuwa kampuni hii imejaribu kucheza kamari na amani ya Tanzania. Ni lazima ichunguzwe kikamilifu na washirika wake waumbuliwe.
Mhe. Balozi, nchi yako kwa miaka mingi sasa imeweza kutengeneza maisha ya mafanikio kwa wananchi wake. Na ukweli ni kuwa, mafanikio hayo yanafanya watu wengi watamani si tu kutembelea huko, bali pia kuishi huko. Hata hivyo, sote tunajua kuwa Marekani haikuundwa mbinguni na wala haikuteremshwa kama ule “mji wa Yerusalemu” uliokuwa umepambwa kwa vito vya thamani na dhahabu.
Marekani tunayoiona leo hii kwenye luninga na picha ni matokeo ya jasho na damu ya wananchi wenye kufa kama sisi. Kile ambacho watoto wenu wanafurahia leo hii, ni matokeo ya kazi na juhudi za wale walioshi kabla yao.
Ndio maana Marekani hivi sasa inasimama kama wazo na jaribio la maisha ya wanadamu lililofanikiwa. Marekani inasimama kama alama ya kile ambacho wanadamu wakidhamiria wanaweza kukipata. Ndiyo, Marekani ambayo wengine wanaipiga madongo na kuichukia ndiyo hiyo hiyo inayosimama kama ishara ya watu huru wenye kuthamini uhuru wao na kufanya kila jitihada kuulinda. Ni kwa sababu hiyo, hata mataifa madogo (kama hili la kwetu) wanaiangalia Marekani na mapungufu yake yote na wanaihusudu.
Mheshimiwa Balozi, na sisi hapa Tanzania tuna matamanio yetu. Kila tulalapo na tuamkapo; kila tuendapo shamba na maofisini, na kila tufanyapo shughuli zetu za kila siku, ndani ya mioyo yetu tunatamani kuwa na taifa ambalo viongozi wake ni wawajibikaji, lenye kusimamia haki, taifa ambalo utawala wake unatoka na unabakia kwa wananchi wake.
Taifa ambalo lina shule nzuri, barabara nzuri, maji, umeme, chakula cha kutosha na mafanikio bwelele kwetu sisi wenyewe na kwa watoto wetu. Mambo hayo yote ambayo ni mema tunatambua kuwa si zawadi ya Mungu kwa Wamarekani, bali ni haki ya wanadamu wote wa kila mahali, na wa wakati wote. Hivyo juhudi za wananchi kujenga taifa la namna hiyo zinakwamishwa na viongozi kama tuliowashuhudia wiki hizi chache zilizopita.
Taifa lako leo hii limeshapita kile kizingiti cha mafanikio na watu wako tayari wanafurahia matunda ya mafanikio. Na sisi nasi toka mbali tunatamani tupite katika kizingiti hicho na hatimaye tuweze kufurahia kama taifa na kama mtu mmoja mmoja maisha ya mafanikio na kheri.
Hivyo, ziara ya Rais Bush hapa Tanzania iwe kweli ni chachu ya kuanzisha mahusiano mapya, mahusiano ambayo yatatuonyesha njia ya kuiga katika kufikia mafanikio.
Ni matumaini yangu kuwa ziara hii itatupa nafasi ya kujifunza na kuanza mahusiano ambayo yataleta manufaa ya kweli kwa Watanzania wa kawaida na kutupa nafasi ya kuweza kutimiza zile njozi za tangu utoto kuwa Tanzania yenye neema ya kweli inawezekana.
Tunamwombea Rais Bush na ujumbe wake ziara njema katika nchi hii nzuri ya Mlima Kilimanjaro na ambayo inanukia mafuta mazuri toka visiwa vya Zanzibar. Mahali hapa ambako mwanadamu alianza safari yake kuelekea maisha bora na mafanikio. Karibu Rais Bush na ujisikie uko Tanzania.
mwanakijiji@klhnews.com
No comments:
Post a Comment