Bunge lapitisha
mapendekezo
ya kamati ya
Richmond
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana lilihitimisha mkutano wake wa 10 mjini Dodoma kwa kupitisha mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge ya Kuchunguza Mkataba wa Kuzalisha Umeme wa Dharura kati ya Kampuni ya Richmond Development Company (RDC) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Hitimisho la mkutano huo wa Bunge lililokwenda sambamba na kumalizika kwa mjadala mkali dhidi ya Kashfa ya Richmond iliyobainishwa na kamati hiyo teule iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe kwa namna ya pekee, ulithibitisha kwamba masuala ya siasa yanazongwa na mambo mengi yasiyotabirika.
Akihitimisha mjadala wa Richmond, Dk. Mwakyembe alieleza namna kamati yake ilivyoyapa uzito mkubwa mawazo yaliyotolewa na wabunge wote waliochangia hoja yake aliyoiwasilisha Jumatano ya wiki iliyopita, na ambayo siku moja baadaye ilisababisha kujiuzulu kwa waliokuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha.
Tofauti na ilivyokuwa wiki iliyopita, wakati akisoma ripoti ya kamati yake kwa mara ya kwanza, jana Dk. Mwakyembe ambaye ni mtaalam wa sheria na hususan masuala ya katiba, alitumia muda mwingi kuweka sawa tafsiri sahihi ya kile kilichoandikwa katika taarifa yake hiyo ya kurasa 165.
Katika eneo la kwanza, Mwakyembe alieleza kusikitishwa kwake na matamshi yaliyotolewa na Lowassa na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz katika michango waliyoitoa walipoijadili ripoti hiyo ya kamati teule ya Bunge.
Akianza na Lowassa, mwenyekiti huyo wa kamati teule alieleza kushangazwa na tuhuma zilizotolewa na waziri mkuu huyo mstaafu kwamba, kamati teule ilimzushia mambo ya uongo na pia akalalamika kwa kutotendewa haki ya kuhojiwa kama ilivyokuwa kwa mashahidi wengine.
Katika hili, Dk. Mwakyembe alijikita kujibu hoja nne zilizotolewa na Lowassa akionyesha kuwa, kamati hiyo haikumlenga yeye (Waziri Mkuu) kama mtu binafsi.
Dk. Mwakyembe kwanza alieleza kushangazwa na uamuzi wa Lowassa kushindwa kueleza kile alichokuwa akikijua kuhusu Richmond wakati alipopewa nafasi ya kuwa mtu wa kwanza kuchangia hoja ya kamati yake.
Hata hivyo, Mwakyembe alisema kama ilivyofafanuliwa ndani ya ripoti yake, wakati wa uchunguzi wake, kamati haikukuta sehemu yoyote ile kuwapo kwa ushahidi uliokuwa ukimhusisha Lowassa moja kwa moja na Richmond, hata baada ya kubaini kuwa alikuwa akifanya mawasiliano ya karibu na Wizara ya Nishati na Madini.
Mwakyembe alisema kwa kuzingatia ukweli huo, ndiyo maana kamati yake haikutaka hata mara moja Lowassa awajibishwe na badala yake ikamtaka yeye mwenyewe kupima uzito wa suala zima na kufikia uamuzi ambao angeona unafaa.
Akifafanua, alisema kuwa kamati hiyo ilikuwa na kazi ya kuchunguza na kubaini ukweli kuhusu Richmond Development Company LLC na katika kuifanya kazi hiyo, hakukuwa na ushahidi uliomhusisha Lowassa moja kwa moja, hivyo hawakuona umuhimu wa kumwita na kumhoji mtu mkubwa kama Waziri Mkuu.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe alisema kuwa kulikuwa na siku 45 ambazo kamati hiyo ilifanya kazi na ilitoa wito kwa mtu yeyote, mwenye ushahidi kuhusu suala hilo kujitokeza kusema mbele ya kamati.
“Kwamba Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni na ambaye serikali yake inachunguzwa katika mazingira ambayo anatajwa sana na vyombo vya habari kuhusika na suala hilo, kukaa bila kujitokeza kutoa maelezo inashangaza,” alisema Mwakyembe akionyesha dhahiri kwamba Lowassa mwenyewe alikuwa anawajibika kujitokeza katika kamati hiyo.
“Tunashukuru kuwa amepima na kuamua kujiuzulu,” alisema Dk. Mwakyembe na kubainisha kuwa, kwa wale ambao kamati ilibaini kuwa wametenda makosa ya kiuwajibikaji au ukiukaji wa maadili, kamati hiyo ilipendekeza wazi wazi wachukuliwe hatua.
Akimzungumzia Rostam ambaye alichangia mjadala huo kwa maandishi, Dk. Mwakyembe alimtaka mbunge huyo ama kufuta au kuthibitisha madai yake kwamba kamati hiyo teule ya Bunge iliendelea na kazi hata baada ya muda wake wa Desemba 30 kuisha.
Kwa kuwa Rostam hakuwepo bungeni jana, Dk. Mwakyembe aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala hilo na baadaye wakati akitoa ufafanuzi, Sitta alisema kuwa mbunge huyo atatakiwa kuthibitisha kauli yake au kuifuta wakati wa mkutano wa 11 wa Bunge utakaoanza Aprili 8, mwaka huu.
Mbali ya hilo, Dk. Mwakyembe alishangazwa na kauli ya Rostam kuwa kamati haikumtendea haki kwa kumpelekea wito siku ya Desemba 24 wakati ikijua kuwa kwa mazingira ya wakati huo, asingeweza kupatikana kwa sababu ya sikukuu.
Lakini Dk. Mwakyembe alikumbusha kuwa siku hiyo, watu wengine wanne, Edward Hosea wa Takukuru, mtu mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ngilima na Mkurugenzi wa Kampuni ya Dowans, nao walipelekewa wito wa kuitwa na walifika kuhojiwa Desemba 27 kama walivyotakiwa.
“Tulimwita Rostam Aziz ili atusaidie kujibu maswali kadhaa… kwanza ni kwa nini Kampuni ya Dowans inatumia anwani ya barua pepe na fax ya kampuni yake ya Caspian... pia tulimtaka atueleza kwa nini aliitafutia Richmond, Media Consultant (mshauri wa mambo ya habari),” alisema Mwakyembe .
Mbali ya hilo, Dk. Mwakyembe alikanusha madai ya mbunge huyo wa Igunga ambaye katika mchango wake aliilaumu kamati hiyo kwa kumtaja yeye kuwa ni mmiliki wa Dowans, iliyorithi mikoba ya Richmond.
Katika hili, Mwakyembe alisema upo uwezekano mkubwa kuwa mbunge huyo hakuisoma ripoti yake, bali alisimuliwa na marafiki kwani kamati yake haikupata kueleza sehemu yoyote ile kwamba, Rostam alikuwa ndiye mmiliki wa Dowans.
Awali kabla ya mjadala huo kuhitimishwa kwa wabunge kuridhia mapendekezo yote ya kamati teule, wajumbe wawili wa kamati hiyo, Stella Manyanya na Lucas Selelii kwa nyakati tofauti walieleza kuhusu kuhofia maisha yao kutokana na kuwapo kwa taarifa za kutishiwa.
Selelii kwa upande wake aliahidi kumuonyesha Spika wa Bunge, Sitta ujumbe wa maneno katika simu ya mkononi uliokuwa ukielekeza vitisho hivyo dhidi yake na muda mfupi baadaye Manyanya akalieleza Bunge kuwa alikuwa yuko tayari kupoteza maisha yake kwa ajili ya kutetea maslahi ya Watanzania.
“Mtuombee. Wenye nia mbaya wanatutishia maisha. Tuna text messages. Tutakupatia bwana Spika pamoja na majina ya watu ambao hatukuwataja katika ripoti yetu… tutakupatia ili chochote kitakachotokea Bunge lichukue hatua,” alisema Selelii.
Akiahirisha mjadala wa Bunge jana hiyo hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipongeza utaratibu mzima uliowezesha kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge na akasema serikali imekubali kuyatekeleza mapendekezo yote ya kamati hiyo.
“Lakini ni dhahiri utaratibu huu unapata mwanya wa kutumika inapobainika kuwa sheria, taratibu na kanuni mbalimbali zimepuuzwa na serikali katika utendaji wake wa kazi. Kwa hiyo, jibu sahihi kwa serikali ni kufanya kazi kwa umakini na uadilifu mkubwa.
“Kwa hiyo, ahadi yangu kwa Bunge hili ni kuhakikisha timu hii mpya ya mawaziri inatimiza wajibu wake ipasavyo. Kwa nini serikali ifikishwe katika hatua ya kuundiwa Kamati Teule wakati serikali inao uwezo mkubwa wenye utaalamu wa kutosha,” alisema na kubainisha kuwa, katika suala la Richmond, serikali haikuwajibika ipasavyo.
Alisema kuwa Rais Kikwete alikuwa ameshaliagiza Baraza la Mawaziri jipya kutoitafuna nchi ama kwa makusudi au kwa uzembe kwani kufanya hivyo ni kuwasaliti Watanzania.
“Kwa hiyo, dawa ya kweli kwa serikali kuepuka kuundwa Kamati Teule za Bunge ni serikali kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kutanguliza mbele uzalendo na maslahi ya taifa letu. Vinginevyo kamati hizi zitaendelea kuundwa. Serikali tujipange upya,” alisisitiza.
Alisema kuwa serikali inayapa mapendekezo ya kamati teule uzito unaostahili kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za nchi.
Pinda alisema kuwa, kutokana na uzito wa suala hilo, serikali imeamua kuunda timu ndogo ya wataalamu, ambayo itayachambua kwa makini mapendekezo kwa kuzingatia yaliyomo kwenye Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge na pia taarifa za majadiliano zilizomo katika kumbukumbu za Bunge (hansard).
Alisema kuwa wajumbe wa timu hiyo atawateua kutoka Ikulu katika Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tume ya Mipango, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bodi ya Wasajili ya Wakandarasi, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi (PPRA), TAMISEMI na Tume ya Maadili.
“Matukio katika mkutano huu yameitambulisha nchi yetu kama nchi yenye kukomaa kwa demokrasia na yenye utawala bora. Mkutano huu umeonyesha jinsi nguvu za mihimili mitatu zinavyofanya kazi.
“Aidha, mkutano huo umeonyesha uwajibikaji na upeo mkubwa wa viongozi wetu katika kukubali demokrasia ifanye kazi kwa amani na utulivu. Tumetimiza yote yaliyomo katika katiba yetu. Huu ndio uthibitisho kwamba katiba yetu inaweza kutuongoza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza,” alisema.
Akizungumzia changamoto zinazolikabili taifa hivi sasa, Pinda alitaja tatizo kubwa la kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kama jambo linalopaswa kushughulikiwa haraka.
Alisema kuwa takwimu za matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2007 zinaonyesha kuwa ni asilimia 54.11 tu ya wanafunzi 419,136 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ndio waliofaulu na kuwa kiwango hicho ni kidogo kwa asilimia 16.4 ukilinganisha na asilimia 70.51 ya wanafunzi 401,011 waliofanya mtihani mwaka 2006.
Kuhusu upungufu wa nafaka nchini, alisema kuwa kumesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo nchini.
Alisema pamoja na matatizo yaliyojitokeza nchini, lakini upungufu wa nafaka umechangiwa pia na kuongezeka kwa matumizi ya nafaka duniani katika uzalishaji wa nishati.
“Hali hii inasababisha uhaba wa mahindi yanayoweza kuagizwa kutoka nje ya nchi. Kutokana na hali hii, haitegemewi kwamba bei za nafaka katika soko la dunia zitashuka katika muda mfupi ujao,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali imeamua kusimamisha kwa muda uuzaji wa mazao ya nafaka, hususan mahindi na mchele, nchi za nje hadi mwezi Mei 2008.
Alisema hatua hiyo inalenga kusaidia chakula kilichopo nchini kuendelea kupatikana na pia kupunguza kasi ya kupanda kwa bei.
Pia serikali imeamua kuondoa ushuru kwa waagizaji wa zao la mahindi kutoka nje ya nchi kwa lengo la kupunguza uhaba wa nafaka kwa kipindi hiki hadi mwezi Mei 2008 ambako mazao mapya yataanza kuingia sokoni.
“Aidha, tani 300,000 za mahindi zimeruhusiwa kuingizwa nchini bila kodi kati ya kipindi cha mwezi Januari hadi Mei 2008,” aliongeza.
Kutoka Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment