Lowassa alichafuka
zamani kabla ya
Richmond
HATA kama tuhuma za kampuni hewa ya Richmond zingemnusuru, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, asingefika mbali, kwa vile alikwisha kujitengenezea maadui wengi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), bungeni na serikalini, Raia Mwema imefahamishwa.
Hatua ya Lowassa ya kujiuzulu kiasi cha wiki mbili zilizopita, ilikuwa inahitimisha tu mlolongo wa matukio ndani ya CCM, bungeni na serikalini na hata katika nyanja za kibiashara na kijamii, yanayokwenda nyuma katika wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais ndani ya chama hicho, na baadaye katika utendaji wa kila siku akiwa Waziri Mkuu.
Yeye mwenyewe amekuwa hapatikani kueleza ni nini anafikiri kimemsibu, lakini watu wa karibu naye wameifahamisha Raia Mwema kwamba anaamini kwamba tuhuma za rushwa katika mradi wa Richmond haziwezi kuelekezwa kwake moja kwa moja kwa sababu “hakula hata senti moja” ya kampuni hiyo.
“Amekuwa anasikitika sana. Moyo wake ni mweupe kwa suala hili. Anasema hata senti moja ya Richmond haijui, lakini ameamua kukaa kimya kwa vile jinsi umma ulivyopokea suala hilo ni kama vile tayari hukumu imepita na hakuna anakoweza kusikilizwa.
“Lakini inafahamika kwamba mara mbili alijaribu kuonya kuhusu mradi huo wa Richmond, uliokuwa uzalishe umeme wa dharura. Kwanza mwishoni mwa Septemba 2006 aliandika kwa Waziri wa Nishati na Madini, akitaka Richmond ichunguzwe na Serikali ijiridhishe kama kampuni hiyo ina uwezo, na mara ya pili, ni Oktoba mwaka huo huo, alipoitisha kikao cha wakuu wa idara, kama ya Usalama na vyombo vingine, kutaka kujua hali ya mambo ilikuwaje,” anasema mmoja wa waliozungumza na Raia Mwema wiki hii.
Kwa mujibu wa watoa habari hao, huenda Lowassa akatoa mwanga kidogo wa masahibu yake mwishoni mwa wiki hii, jimboni kwake Monduli, ambako atazungumzia suala hilo na ambako inaelezwa kwamba umma uliompigia kura unamsubiri kwa kuwa unahisi mambo mabaya yanaweza kumsibu mbunge wao.
Lakini tathmini ya matukio wakati na baada ya mchakato wa urais ndani ya CCM, na hatimaye baada ya serikali ya awamu ya nne kuanza kazi, inaonyesha kwamba majeraha ya mchakato, malengo ya kisiasa, kujihusisha na biashara na staili yake ya utendaji vinaweza kuwa vimechangia sana katika kumchafua na kutengeneza maadui miongoni mwa wanasiasa wenzake, watendaji serikalini na hata wafanyabiashara.
Habari za ndani ya Serikali na CCM zinaeleza kwamba, kwa kiasi kikubwa Lowassa alijikuta amezungukwa zaidi na maadui kuliko marafiki katika utendaji kazi wa kila siku, ndani ya Bunge na hata katika Baraza la Mawaziri.
Kwa mujibu wa habari hizo, Lowassa amejikuta akiwa katika wakati mgumu, pengine kuliko alivyotarajia na hata mkubwa wake wa kazi, Rais Jakaya Kikwete, hakuwa na msaada wowote kwake, na hasa katika suala la Richmond, kwa vile aliachia mambo yaende kufuata “demokrasia” ndani ya Bunge na yeye mwenyewe alijiamini kupita kiasi na alipozinduka mambo yalikuwa yamekwisha kuharibika.
Viongozi hao wa juu wa serikali (Kikwete na Lowassa) walijulishwa mapema kuhusu wimbi kubwa la kutaka kumng’oa Lowassa kwa “gharama zozote” hata ingebidi Bunge kuongezewa muda wa hadi wiki mbili kutoa nafasi ya kikatiba ya kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Kuondoka kwa Lowassa kunamfanya kuwa ‘muathirika’ wa kwanza mzito wa uhasama wa kisiasa ndani ya CCM na watu walio karibu naye wamekuwa wakimtisha Rais Kikwete, kwamba “bado yeye” kwa madai kwamba amekuwa akikingwa sana na kuwa karibu na watu wa aina ya Lowassa.
Habari zinasema ya kuwa inawezekana wote wawili, Kikwete na Lowassa hawakupima kabla madhara ya hatima ya uchunguzi wa Richmond ama walitofautiana kimkakati na hiyo inaweza kuwa ndiyo imemfanya Mwenyekiti Kikwete kuzungumza na wazee wa CCM wa Dodoma na Dar es Salaam, akihofia kwamba kundoka kwa Lowassa kutakigawa chama hicho.
RAIS Jakaya Kikwete |
Katika mkutano wa Dar es Salaam, Rais Kikwete alikwepa kuzungumzia undani wa kilichomsibu Lowassa, lakini akaelezea jinsi nchi “ilivyotikisika” na akapiga msemo wa baniani na upati: kudhihirisha kwamba alikuwa akiguswa na kuondoka kwa Lowassa, pamoja na kujikanganya katika hitimisho lake.
Alihitimisha akisema kwamba Lowassa atahukumiwa kwa haki na historia na kwamba hatosita kuvunja tena Baraza la Mawaziri likivurunda, akirejea yaliyotokea bungeni Dodoma, kuwa yalitokana na kuvurunda kwa mawaziri.
Tathmini ya haraka haraka ya baraza jipya la mawaziri, inadhihirisha kwamba hata kama yuko nje, bado Lowassa ataendelea kuwa na nguvu katika ngazi hiyo kwa vile baadhi ya mawaziri walioshika nyadhifa nyeti ni ambao wanamuunga mkono na pia kwamba baadhi ya waliokuwa wakimkosoa, ama moja kwa moja au nyuma ya pazia, kama Anthony Diallo, hawakufanikiwa kurudi barazani.
Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ni kati ya waliokuwa watu wa karibu na Lowassa. Mwaka jana wakati wa kutafuta kura za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, walifanya kampeni ya pamoja na wote walipata kura nyingi.
Baada ya hapo Chenge alipanda hadi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu, japo alishindwa kuzuia wimbi lililoibuka ndani ya kamati hiyo kuhusu tuhuma za ufisadi na hasa suala la Richmond. Kama asingekuwa na nguvu nyuma yake, Chenge asingerejea katika Baraza la Mawaziri, kutokana na kuwa umma unamwona kama mhusika katika mikataba uchwara inayoitia hasara nchi, wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha, naye ni mtu wa karibu na Lowassa. Sasa amekuwa Waziri kamili wa Wizara hiyo, ikiwa imeunganishwa na iliyokuwa Wizara ya Usalama wa Raia.
Wakati Richmond inafukuta, Masha alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, chini ya Dk. Ibrahim Msabaha, aliyejiuzulu kutokana na sakata hilo.
Inaelezwa kwamba uwakilishi wa Lowassa utaendelea kujionyesha pia katika sura za mawaziri kama Naibu Waziri wa Fedha, Jeremiah Sumari ambaye wana mahusiano ya kifamilia na Waziri wa Nishati, William Ngeleja, ambaye ni kati ya walio karibu naye.
Habari zaidi zinaeleza kwamba, Lowassa alijitia kitanzini kutokana na wapambe wake kuonyesha dhahiri, mapema kiasi hiki, kuwa alikuwa ndiye mtu pekee mwenye kila sababu na uwezo wa kumrithi Kikwete atakapong’atuka, akijitanua serikalini na ndani ya CCM.
Hiyo ilizua mahusiano mabaya baina yake na wanasiasa wenzake katika makundi mbalimbali ndani ya Serikali na ndani ya CCM. Inafahamika kwamba kwa muda mrefu hakuna mahusiano mazuri kati yake na Spika Samuel Sitta.
Wakati anatangaza kujiuzulu, Lowassa aliashiria kwamba hakuwa anaona sababu nyingine ya suala lake na Richmond kushikiwa bango kiasi hicho, zaidi ya nafasi ya uwaziri mkuu, lakini hakuthubutu kutaja mtu.
Majina yaliyokuwa yakitajwa kuziba nafasi yake, pamoja na mengine, kama la ambaye hatimaye alikuja kupita, Mizengo Pinda, lilikuwamo jina la Sitta na Naibu Spika wake, Anne Makinda.
Lakini pia imekuwa ikielezwa kwamba hakukuwa na uelewano mzuri kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Wote, Sitta na Membe na hata Lowassa mwenyewe, hakuna ambaye alipata kutamka wazi kutaka kuwania nafasi aliyonayo sasa Kikwete, lakini katika CCM mambo hayo huanza mapema sana miongoni mwa makundi mbalimbali.
Ofisa mmoja mwandamizi serikalini ameliambia Raia Mwema kwamba, kuendelea kuwapo kwa kundi la ‘wanamtandao’ japo katika hali ya kugawanyika, kulikuwa kunawakera watendaji wa vyombo vya usalama na wanamkakati wengine ndani na nje ya serikali, wakihofia kuwa kundi hilo mbele ya safari linaweza kuwa hatari kwa vile ni vigumu kulidhibiti.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, Lowassa na baadhi ya wanasiasa wa karibu naye kama Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, walionekana kuwa ndio vinara wa “wanamtandao”, kundi lililoonekana kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi serikalini na kwenye chama, na kwa ajili hiyo, ilikuwa ni “muhimu” kwa vinara hao “kushughulikiwa” ipasavyo mapema, na suala la Richmond lilikuwa linatoa fursa hiyo.
Inaelezwa hata uteuzi wa Pinda, pamoja na kupata baraka za Lowassa, ni mahsusi kuwa na mtu wa ndani ya mfumo katika nafasi za juu, akiwa nyuma ya Rais Kikwete ambaye naye alitokea jeshini katika kundi hilo hilo.
Habari za kwamba yanayomkuta Lowassa yamechochewa pia na makundi ya waliowania urais mwaka 2005 wakati wa mchakato, nazo zinashika kasi, lakini ‘mzimu’ wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwamba aliwahi kumkataa, umeelezwa kuwa na nguvu kubwa katika hisia za Watanzania wengi na hivyo kuwa moja ya sababu kubwa za mwanasiasa huyo kutoka kaskazini kuonekana “muovu” mbele ya Watanzania wengi.
“Pamoja na utendaji wake ambao haukuruhusu majibu rahisi ya matatizo, kuwapatiliza wahusika, wengine maofisa waandamizi, kama wakuu wa mikoa, hadharani, ambao kimsingi hawakuwa wakitimiza wajibu wa nyadhifa zao, kulimfanya kuwa, pengine Waziri Mkuu asiyependwa na watendaji wavivu nchi nzima, kuliko yeyote aliyepata kushika wadhifa huo,” anaeleza mwanasiasa mmoja aliye karibu naye.
Kuonekana kama mu-imra, jambo ambalo hata Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Richmond, Dk Harrison Mwakyembe alilitaja katika ripoti yake, kulimpa maadui wengi kuliko marafiki katika ofisi za umma. Dhahiri kauli yake ya kwamba hapendi mtindo wa business as usual (kufanya kazi kwa mazoea) ilitisha na ikajenga chuki.
Lakini pengine msigano wa kwanza mkubwa kati yake na Bunge na wabunge, ambao walimpitisha kwa kura nyingi kuwa Waziri Mkuu, ulitokana na kauli yake ya kuwatuhumu wana Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, iliyokuwa ikisikiliza malalamiko ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mbunge wa Mkuranga (CCM) Adam Kighoma Malima.
Hiyo ilikuwa Januari mwaka jana, pale baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo waliposema wazi kwamba yeye kama kiongozi serikalini alikuwa akielemea upande mmoja, hasa alipokaririwa akisema kwamba mfanyabiashara Yusuf Manji, ndiye aliyetoa fedha nyingi kuhakikisha Mengi anashindwa katika kesi hiyo ambayo hatima yake, Malima alibainika kusema uongo bungeni. Malima sasa ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Wabunge waliozungumza na Raia Mwema mjini Dodoma, wiki iliyopita, walisema kipindi hicho ndicho ambacho wabunge walipoteza imani na Lowassa, na kumuona kama kiongozi ambaye hawezi kupambana na rushwa kwa dhati na kwamba anaweza hata kuhusishwa nayo kirahisi kwa kujiweka karibu na watu wasio safi.
Baadaye Kamati hiyo ilisambaratika. Mbunge wa Moshi Mjini (CHADEMA), Philemon Ndesamburo, alijitoa akisema Kamati imechafuliwa na hivyo haikuwa na mamlaka ya kujadili kesi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baadaye, Ndesamburo alidai ya kuwa, Kamati hiyo ilikuwa ikiingiliwa kazi zake na Serikali, lakini baadaye alimtaja moja kwa moja Lowassa akiwa Waziri Mkuu, kuwa aliingilia mwenendo wa kamati hiyo.
Hata hivyo, Lowassa hakuitwa katika kamati hiyo na ilielezwa kwamba uamuzi huo ulitokana na “busara za Spika wa Bunge, Samuel Sitta” kuzuia kuitwa kwa kiongozi wa juu wa serikali.
Kauli hiyo ya “busara za Spika wa Bunge, Samuel Sitta” ndiyo aliyotumia pia mjumbe wa Kamati Teule ya Richmond, Mbunge wa Nzega (CCM), Lucas Selelii, kujibu kwa nini Kamati haikumhoji Lowassa.
Selelii alisema, “hii si mara ya kwanza kumhusisha Waziri Mkuu. Mara ya kwanza ilikuwa kwenye suala la Mheshimiwa Malima na Ndugu Mengi ambapo Waziri Mkuu (aliyejiuzulu) alidaiwa kuwatuhumu wabunge kupokea rushwa. Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilipotaka kumuita kwenye kamati hiyo, (Spika) ulitumia busara zako na kuishauri kamati hiyo kutomwita kutokana na nafasi nyeti aliyonayo Waziri Mkuu katika uongozi wa taifa. Waziri Mkuu hakulalamika. Kwa busara zako, kamati teule haikutaka kumuita kwa kuwa ilikuwa na ushahidi uliojitosheleza…”
Baada ya kauli hiyo ya Selelii na majibu ya Lowassa, ambayo hayakubadili kitu, bungeni wiki iliyopita, Spika alitaja orodha ya wachangiaji. Walikuwamo Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango. Kilango ni mke wa mwanasiasa mkongwe na mahiri, John Malecela. Wengine ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Anne Maulidah Komu, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka na Ndesamburo.
Mchango wa Kilango ulifungua pazia na kutoa mwelekeo wa aina ya mjadala utakavyoelekea na aliunga mkono moja kwa moja maoni ya Kamati.
Kama alivyowasilisha Kilango, Komu, Sendeka, Ndesamburo na baadaye wachangiaji wengine kama vile Mbunge wa Kibakwe (CCM), George Simbachawene, wote waliunga mkono mapendekezo ya Kamati Teule na kumpongeza Lowassa kwa kujiuzulu. Mapendekezo hayo yalipitishwa baadaye na Bunge zima kwa kauli moja.
Ofisa mmoja mwandamizi wa Serikali aliliambia Raia Mwema, Dodoma, wiki iliyopita kwamba, mtiririko wa wachangaji ulimkumbusha ripoti mbadala iliyowasilishwa wakati wa kesi ya Malima na Mengi na waliowasilisha walikuwa ni Kilango na Sendeka.
“Unakumbuka Sendeka na Kilango ndio ambao walisimama kidete katika suala la Malima na Mengi na wakaandika ripoti mbadala wakati wenzao walionyesha wazi kupindisha ukweli. Hiyo iliwajengea heshima kubwa lakini pia ilimjengea Lowassa picha mbaya bungeni,” anasema mbunge mmoja.
Alipojitoa katika kamati hiyo, Ndesamburo alidai kwamba wajumbe wenzake wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, walidaiwa kuhongwa na Manji ili wasitende haki. Alisema alitaarifiwa habari hizo na Mengi, aliyedai aliambiwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, katika mazungumzo binafsi.
Baada ya mvutano wa muda mrefu, kamati hiyo iliwasilisha taarifa yake kwa Spika Sitta, ambaye aliandaa taarifa nzito ikiwa na uamuzi ulioonyesha kwamba Malima alisema uongo, lakini alitumia busara kutaka kuwakutanisha na Mengi kwa lengo la kuepusha migongano katika jamii.
Hata hivyo, sakata la Richmond ambalo ndilo limemng’oa Lowassa, linaelezwa kuwagusa wananchi wengi kutokana na usiri na vitisho kutoka serikalini na hata ndani ya CCM kuzuia watu kujadili ama kuhoji undani wa mradi huo wa umeme wa dharura.
Lowassa anatajwa sana katika kuzuia mijadala hiyo ndani na nje ya serikali, ikiwamo katika vikao vya chama na wiki iliyopita ni wabunge wa CCM waliopewa rungu na Kamati Kuu ya chama chao kutekeleza kile kilichoelekea kuwa mwiba wa kisiasa kwa Lowassa na watu walio karibu naye.
Kutoka Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment