Wednesday, February 20, 2008

Heshima ni kitu cha bure,

tena ni bure kabisa,

haina hata thamani



Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.



Mpenzi Frank,

HABARI za huko nyumbani mpenzi wangu? Biashara inaendeleaje? Bado una kibanda chako maana siku hizi huwezi kujua, waweza kubomoa siku yoyote.

Yaani kwanza wanabomoa uchumi wetu huko juu na miskendo yao kisha sisi vijana tukijaribu kujinasua watubomoa na sisi pia. Kweli, sisi vijana hatuna thamani hata kidogo. Wanatupenda tukiwatumikia wao tu. Yaani wao wapate neema sisi tupate noma.

Nilifikiri bosi atapata noma pia katika hii orodha mpya. Tena nilikuwa nimeanza kufunga mizigo tayari maana hata bosi mwenyewe akawa hoi. Kumbe bado kaula, tuone kama kweli atabadilika tabia na yeye.

Kwa hiyo usiwe na wasiwasi mpenzi mimi mzima, ila tu sijui kama utamtambua Hidaya wako baada ya miezi michache. Hapa mshahara masihara kama kawaida lakini hawa jamaa wanapokula, wanaacha chakula kufuru. Najua wewe utanitania kwamba napenda kula tu lakini nakuambia mpenzi, naona hata aibu kuiacha hivihivi wakati najua watu wengi huko kwetu wanakula mara moja kwa siku tu. Basi hapa mtu ananenepa bila hata kutaka. Laiti ningeweza kukufungia ndani ya bahasha unawiri na wewe!!

Tuache hayo. Kwa leo, kuna swali moja linanisumbua sana kichwani. Hivi, utaalam wa kusema uongo kavukavu unatokana na umri wa mtu au aina ya kazi anayoifanya? Maana hawa wazee wetu wa siasa nawashangaa sana. Ukisikia wanavyoongea wao kwa wao kisha uwasikie kwenye luninga au radioni tofauti kabisa. Basi niliona labda uongo ni sehemu ya siasa tu.

Najua si wanasiasa tu. Hata wazazi wetu wamo. Unakumbuka wakati ule baba mdogo alipojaribu kunitongoza. Nilipopiga kelele akajitetea weeee utadhani yeye malaika katoka mbinguni kunipa baraka maalum kwa kunishika matiti (na hata hiyo aliapa ilikuwa bahati mbaya, eti alitaka kutoa uchafu begani mkono ukateleza kwa bahati mbaya na kutua kwenye matiti). Na watu wazima wenye akili zao walimwamini! Au walijifanya wanamwamini ili isiwe kashfa. Lakini hata kujifanya hivyo si uongo vilevile! Eti uongo mtakatifu wakati mimi nadhalilishwa hivyo! Utakatifu uko wapi?

Lakini uongo wa hawa mamini-staa na wapambe wao ni kitu kingine. Sijui watauita uongo heshimiwa!! Ni kama wanakula kiapo cha uongo kila wakiamka asubuhi. Imekuwa hivi kwa bosi wangu kiasi kwamba akisema kwamba leo ni Jumanne, naanza kujiuliza kama ni Jumatano.

Waweza kushangaa mpenzi kwa nini nasema hivi. Si nawaona! Mimi sielewi haya maneno yote ya benki kuu na mikataba feki na Richimondi na nini sijui mpaka mitetemeko ya ardhi imeleta maporomoko.

Lakini nashangaa. Kwanza wanasema kwamba hakuna kashfa kabisakabisa na kuwakashifu watu wote wanaoshikilia bango kashfa. Kisha wanasema basi tutachunguza ingawa hakuna kashfa na wanaoshikilia bango ni wavuta bangi na kadhalika.

Ghafla, wanasema kweli kashfa ipo, tena kubwa kabisa na yote ni kwa sababu ya watu wachache waliokashifika peke yao. Kisha wanaanza kurukaruka kama watu waliopagawa kuwalaani haohao waliokula nao jana na juzi kana kwamba ni hao tu walioleta kashfa zote hizi na wao hawakujua kitu.

Lakini wanapoongea sebuleni hapa wanaongelea vingine kabisa. Bosi kila siku neno lake kuu ni ‘wivu’. Hawa wapinzani uchwara wana wivu. Wananchi wana wivu. Aliyetoa taarifa ana wivu. Si wovu wao bali wivu wa watu wengine. Hivi wanatuona sisi wajinga sana? Hatuna akili? Yaani sielewi mpenzi, sielewi, sielewi.

Na hapo nilipata wazo jingine pia. Hivi, huu utamaduni wa Kiafrika wanaotuimbia kila siku, eti tuwaheshimu wazee, tuwaheshimu wazee una maana gani? Kwanza, wanatuheshimu na sisi? Wanapotoa au kutetea uongo wa kitoto mbele yetu, si wamejivua heshima yao moja kwa moja? Na pili, wakitaka tuwaheshimu, si wawe na vitendo vya heshima? Kwa nini nimheshimu yule baba mdogo baada ya yeye kutaka kunibaka? Kweli heshima ni kitu cha bure. Ni bure kabisa, haina hata thamani. Heshima ya kulazimisha ni ujinga mtupu.

Lakini hapa bosi anapata shida kabisa. Kwa kuwa linatetemeeeka kila ‘wavuta bangi’ wakitishia kutaja majina mengi zaidi, hata baada ya kurudi kwenye meza ya msosi, binti bosi akamvaa juzi.

‘Hivi wewe baba niongeze kiyoyozi? Maana naona unatoa jasho kwelikweli.’

‘Unasema nini wewe mtoto? Niko mzima kabisa.’

‘Lakini baba, hivi haya maneno yanayosikika kila mahali ni kweli? Eti yale mambo ya Benki Kuu si hivihivi tu. Eti mngepata wapi pesa zote zile za kampeni bila kutengeneza mpango?’

‘Nakuambia kila siku wapaswa kupiga mswaki sawasawa kabla ya kuja mezani ili usilete harufu ya meno na maneno yaliyooza.’

‘Kwani kuuliza ni ujinga baba? Pale shuleni ni ishu. Pamoja na umimi wa umeme, kila mtu anaongelea hayo pia. Haya mafulana, na pesa za safari na takrima isiyo takrima na nini sijui yalitoka wapi? Chama chenu kina biashara? Na tunajua wenzenu wa nchi jirani walifanya vilevile. Eti skendo kubwa za mikataba feki si tu watawala wale hadi wapasuke, bali wapate fedha za kuwalisha waliwe ili wachaguliwe kutawala na kuwala watu tena.’

BB alikuwa anaongea kwa kejeli sana huku akicheka na bosi alivyomwangalia nilidhani atampiga papo hapo.

‘Kila siku nakuambia usiongelee usiyoyajua. Hawa wambea wa mitaani watakuambia nini?’

BB akapamba moto.

‘Lakini upotevu wa pesa ndani ya benki uliitwa umbea mwanzoni na sasa mmekubali ni kweli. Mikataba feki ya umeme iliitwa uongo kabisa na sasa waona. Kwa nini huu usiwe kweli pia? Mtakana, mtatukana lakini mtabanwa hadi mwisho mtakubali. Kama hamhusiki, kwa nini msikubali tangu mwanzo?’

Bosi kidogo avunje kikombe alivyokiweka chini kwa nguvu. Ilibidi mama bosi aingilie kati haraka haraka.

‘Mwanangu kwa nini unamsumbua baba namna hii? Umheshimu baba yako.’

Heshima, mpenzi! Neno lilelile tena. Lakini hii yote ilikuwa ya kunyamazisha BB ambaye aliondoka pale kwa ghadhabu bila kusema neno. Kweli nawashangaa pia watoto wa wakubwa wanavyothubutu (ningeweza wapi mbele ya baba yangu, si ningezabwa kibao hadi meno yote yangeruka). Lakini bado bosi hakujibu maswali ya binti yake.

Kafoka tu kana kwamba kufoka kutamaliza maswali yake (na yangu pia!!). Na hapo pia nina swali la mwisho. Ukishaanza kusema uongo kama yule mzee wazimu wa nchi jirani, utawezaje kurudi nyuma? Si itabidi uendelee kutunga uongo mkubwa zaidi na zaidi na kuchekwa zaidi na zaidi na kuchukiwa zaidi na zaidi hadi heshima zooote zinazimika moja kwa moja.

Kwa hiyo nangoja kuona sasa lipi litakanwa na kutukanwa tena. Angalao napata senema ya bure hapo. Kama nisingeona uchungu jinsi wanavyotuchonga, ningecheka.

Akupendaye kwa heshima zote na bila hata chembe ya uongo ndani yake,

Hidaya.

Kutoka Raia Mwema wiki hii.



No comments: