Tuesday, February 19, 2008

Mafisadi

Kukamatwa,

Kufilisiwa..


Na Makongoo Oging’

Serikali imetoa tamko kali kuwa mafisadi wote ambao wanamiliki vitu vya thamani watakamatwa na kufilisiwa mali hizo bila kujali vyeo vyao....

MAFISADI KUKAMATWA KUFILISIWATamko hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Godfrey Nzowa alipokuwa na mahojiano maalum na mwandishi wetu ofisi za makao makuu ya idara hiyo jijini Dar es Salaam.

Alisema, kwa kuwa vyombo vya serikali hivi sasa vinashirikiana kwa pamoja na wamefikia hatua ya kuwasaka vigogo mafisadi wanaomiliki mali za thamani zinazotokana na ufisadi wao.Alisema wanaojihusisha na dawa za kulevya ni mafisadi na wale wote ambao majina yao yamo katika orodha ya polisi (majina yao ameyahifadhi kutokana na sababu za kiusalama) na wapo nje ya nchi, watasakwa kwa kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) ambao wameonyesha ushirikiano mkubwa.

“Ukweli ni kwamba kazi imeiva na mafisadi hao tunawafuatilia na tukiwakamata tutawafikisha mahakamani na mali zao walizopata kwa njia zisizo halali tutazitaifisha kwa manufaa ya umma,” alisema Kamanda Nzowa.
Alitaja mali hizo kuwa ni nyumba, magari ya kifahari na akaunti zao za ndani au nje ya nchi.

Kamanda Nzowa aliongeza kuwa, wapelelezi wa polisi wa nchi mbalimbali duniani tayari wamekuwa wakikutana na kujadiliana jinsi ya kugundua mbinu wanazotumia mafisadi ili kudhibiti.

Akizungumzia hali ya udhibiti wa dawa hizo, Kamanda huyo alisema kuwa kwa asilimia kubwa biashara hiyo imepungua kutokana na ushirikiano kati ya raia na polisi.

Alisema watumiaji wakubwa wa dawa hizo sasa wameacha na kujishughulisha na kazi halali za kujipatia mapato.
Aliongeza kuwa watumiaji wa dawa hizo ambao walihukumiwa na mahakama na kumaliza vifungo vyao hivi sasa wapo katika maangalizi ya polisi na wamekuwa wakiripoti kila wiki makao makuu ya kitengo cha kuzuia dawa za kulevya
nchini.

Kamanda Nzowa ameomba ushirikiano zaidi kwa wananchi ili kukomesha kabisa biashara hiyo haramu ambayo inaharibu vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.



No comments: