Kwaherini…
Kwa hisani ya: http://haki-hakingowi.blogspot.com
yamkuna Bush
RAIS George W Bush ameelezea kufurahishwa na mapokezi, ukarimu na upendo alioonyeshwa na Watanzania akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya siku nne nchini.
Rais Bush ambaye aliwasili juzi nchini, aliisifia Tanzania na kutamka wazi kuwa amefurahishwa na mapokezi makubwa aliyoyapata na kwamba katika usiku wa kwanza akiwa nchini ameona jinsi Watanzania walivyo wakarimu kwake na watu alioambatana nao, ambao leo wanaelekea Arusha.
Inafurahisha sana kwa mapokezi na kuona maelfu ya watu wakiwa wamejipanga barabarani kwa ajili ya kutupokea, alisema Rais Bush.
Katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere alipotua juzi jioni, Bush alionyesha dhahiri kufurahishwa na mapokezi hadi akamwita mama mmoja na kumkumbatia kwa furaha, kitu ambacho watu wengi hawakutarajia kuwa angeweza kufanya.
Jana asubuhi alipoingia Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Bush aliwakuta watu wengi wakiwamo wanafunzi na akimama wafanyakazi wa Jiji la Dar es Salaam. Pia alionyesha wazi wazi kufurahishwa na mapokezi na kuamua kutoa mkono kuwasalimia watu wengi waliokuwa wamekusanyika.
Pamoja na kuwa na ulinzi mkali wa makachero wa Marekani, lakini Rais huyo alijitahidi kusalimiana na kila mtu ambaye alikuwa karibu yake, huku akionyesha uso wa furaha wakati wote. Kuna wakati mwananchi mmoja alidondosha kipeperushi chake na Rais Bush akainama na kukiokota na kisha kumpa.
Wakati akiingia Ikulu kutokea lango la nyuma ya Ikulu katika Barabara ya Ocean, Rais Bush alitembea kwa miguu umbali wa zaidi ya mita 100 akiongozana na mwenyeji wake, Rais Kikwete hadi katika Jengo la Ikulu kwa ajili ya mazungumzo.
Magari zaidi ya 40 yaliyokuwa katika msafara wake, yalibaki nje huku yakiwa yanalindwa na makachero wa Kimarekani na Tanzania, huku barabara hiyo ikiwa imefungwa.
Baada ya mazungumzo na Rais Kikwete ambayo yalidumu kwa takribani saa moja, Rais huyo na mwenyeji wake walitoa hotuba kwa watu waliokuwapo akiwamo Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na viongozi wengine.
Kama mtoto wa mjini, Rais Bush alianza hotuba yake kwa kusema:
"Mambo Zenu?"
Salaam hiyo iliwafanya watu watahayari na kuitikia kwa pamoja "poooa" na minong´ono ilianza kwani hakuna aliyetarajia kama Bush angeweza kuongea neno lolote la Kiswahili.
Katika mazungumzo yake, alitumia muda mwingi kuisifu Tanzania kwa heshima na utulivu iliojijengea na kwamba hata serikali yake imeleta fedha nyingi kama walivyotiliana saini na Rais Kikwete jana, kwa sababu hiyo.
Akiwa anatabasamu, Bush alisema kuwa anamchukulia Rais Kikwete kama rafiki kwa jinsi alivyo mchapakazi na heshima aliyojijengea hasa kwa kuwa sasa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.
Akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi, alionyesha wazi kuwa utawala wake umekuwa ukijali Afrika tangu alipoingia madarakani kwa kutoa misaada mbalimbali.
Kutoka gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment