BAADHI ya Watanzania, wakiwamo viongozi mbalimbali wastaafu na wale wa vyama vya upinzani, wamekuwa wakiliambia taifa kwamba limepungukiwa viongozi waadilifu na kwamba umaskini unaolikabili taifa letu ni wa kujitakia.
Kwa sababu, licha ya rasilimali kubwa tulizonazo, hatuna viongozi wenye upeo wa kutuonyesha njia ya kuzitumia vyema ili kutupatia maendeleo.
Badala yake tunaona kuwa tunao viongozi wasio waadilifu, mafisadi, wazandiki na wababaishaji wa kutupwa.
Uongozi wa taifa una mfumo wa kitaasisi ambao wengi wanaita ‘system’. Kwa lugha ya kawaida ‘system’ inamaanisha mfumo wa Idara ya Usalama wa Taifa katika kuchagua na kudhibiti ubora wa viongozi na mwenendo wao.
Moja ya wajibu mkubwa wa idara hiyo ni kulipatia taifa viongozi bora, wazalendo na waliofundwa vya kutosha kutumia madaraka yao kutetea masilahi ya taifa. Lakini wimbi la ufisadi lililojitokeza nchini ni ishara kwamba Idara yetu ya Usalama wa Taifa imeshindwa kazi.
Moja, idara hiyo imegeuka kuwa ni sehemu ya CCM, badala ya kutekeleza wajibu wake tulioutaja kulingana na Katiba na sheria za nchi, ikiangalia vyama vyote, taasisi zote za kijamii nk.
Baadhi yao wamejifanya ni watendaji wa CCM na wanapotenda hivyo kazi yao kubwa inakuwa ni kuhujumu viongozi walio kwenye vyama shindani kana kwamba hawa si Watanzania, ila ni maadui wa nchi.
Pili, kuzuka kwa kundi la wanamtandao ambalo linadaiwa kumuweka madarakani Rais Kikwete kunaashiria ushiriki mkubwa wa idara hiyo kupanga mtandao kuhusisha sekta zote za jamii na kuhusisha watendaji muhimu serikalini ili wote kwa pamoja watekeleze azima ya CCM kubaki madarakani.
Inasemekana kwamba nyuma ya ufisadi unaofichuliwa, yapo makampuni ya kifisadi ambayo hayumkini yalianzishwa na Idara ya Usalama wa Taifa kukusanya mabilioni ya fedha yaliyotumiwa na wanamtandao na CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005.
Hakika yeyote anayependa kusema ukweli atakiri kwamba mabilioni ya fedha yaliyotumika kwenye mchakato ndani ya CCM na mabilioni ya fedha yaliyotumiwa na CCM katika uchaguzi uliopita, hayana maelezo au chanzo kingine kama si makampuni hayo ya kifisadi ya kupora fedha za umma.
Sasa tujiulize, taasisi hii ina uadilifu kiasi gani, na je, aijashiriki katika ufisadi kwa namna yoyote ile?
Ikiwa watetezi wa Usalama wa Taifa watasema inatenda kazi zake kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, je, walilala wapi Benki Kuu ilipohujumiwa?
Je, ilikuwa wapi masilahi ya nchi katika uzalishaji wa umeme yalipohujumiwa katika mradi wa IPTL na Richmond?
Je, walikuwa wapi masilahi ya nchi yalipohujumiwa katika ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara, TTCL na makampuni mengine mbalimbali ya umma?
Tunachokiona sisi, Idara ya Usalama wa Taifa haijui wajibu wake na ambayo ufisadi ni sehemu kuu ya kazi yake.
Pia, tunachokiona sisi ni idara hii kutojua kutetea masilahi ya nchi, ambayo ipo tayari kuona rasilimali za nchi zikihujumuiwa ili mradi wanaofanya hivyo ni marafiki zao.
Kazi kubwa ni kulindana, kupeana vyeo bila kuwa na sifa na pia kuwapiga vita wale wanaojitokeza kupingana na mwenendo wa kifisadi.
Tumefikishana mahala watu sasa wanamwagiwa tindikali, wanahushishwa kwenye ajali za kupangwa, bila shaka siku si nyingi tutashuhudia mauaji ya watu kwa mtindo wa kijambazi, unaotumiwa na kundi la Mafia.
Inapotokea kwamba viongozi wa taifa ama serikali wanapata nyadhifa au kuajiliwa kazini kwa sifa za ubabaishaji au kughushi, na hilo likafumbiwa macho, basi hakuna usalama wa taifa.
Kwa maana kwamba ikiwa uongozi utawekwa mikononi mwa matapeli walioghushi sifa za elimu, basi hatima ya taifa itakuwa hatarini.
Je, viongozi wa aina hii wataelewa nini kinachoendelea kuhusu mikataba ya biashara ya madini au mikataba ya umma? Kwa hiyo tusishangae serikali yetu kuendeshwa kama viongozi wake hawajaenda shule, kwani si kila anayejiita daktari ni daktari wa kweli.
Mfano, ilikuwaje kampuni ya kihuni ya Richmond kupewa mkataba wa mabilioni ya fedha kununua majenereta ya umeme bila Idara ya Usalama wa Taifa kujua?
Je, kukosekana kwa umeme si jambo nyeti na hatari kwa usalama wa taifa? Au labda idara hii inaona Watanzania wamelala usingizi na wako tayari kufanyiwa vitendo viovu na wako tayari kulipishwa kodi na kubebeshwa gharama kubwa za maisha bila kulalamika au hata kufanya maandamano?
Labda Watanzania wamekuwa wapole mno katika kutetea haki zao. Bila shaka Idara ya Usalama wa Taifa itaona ugumu wa maisha wanaopata wananchi pale tutakapokuwa tayari kuandamana na kuwatoa maofisini na kuwafukuza kwa bakora hao mafisadi!
Kwa ujumla, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama tulivyonavyo, chombo ambacho akijatutendea haki ni Idara hii ya Usalama wa Taifa. Hawa wamelala usingizi wa pono wakati nchi inahujumiwa, wananchi tunapata taabu.
JWTZ, Magereza, JKT na Polisi wanafanya kazi nzuri, tunawapongeza, licha ya kwamba wamekuwa wakilalamikia bajeti za wizara zao kuwa ni finyu kuliko bajeti ya Idara ya Usalama wa Taifa.
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), chini ya Davis Mwamunyange, wanafanya kazi nzuri na ndiyo maana hadi sasa nchi yetu haijavamiwa na maadui.
Polisi chini ya IGP - Said Mwema, nao wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la uhalifu.
Magereza chini ya Kamishna Mkuu, Agustino Nanyaro nao wamejitahidi, kwani hadi sasa hatujasikia kuwa wafungwa wamevunja magereza na kutoraka. JKT nao wanajitahidi kwa kuwalea vijana na kuzalisha mali.
Wakati umefika sasa watendaji wa Idara ya Usalama wa Taifa wawajibike kikamilifu bila kumuonea haya kiongozi yeyote, ama sivyo itabidi idara hii ivunjwe, tuunde chombo kipya, na hilo linawezekana, kama tuna uchungu wa kweli na Tanzania yetu.
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.
0755 312859:
katabazihappy@yahoo.com; www.katabazihappy.blogspot.com
No comments:
Post a Comment