Tuesday, February 26, 2008

Rais wa Uturuki ziarani

Tanzania leo.


Rais wa Uturuki, Abdullah Gül


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, amewataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais wa Uturuki, Abdullah Gül, anayewasili nchini leo kwa ziara ya kiserikali.

Taarifa kutoka kwa Mkuu huyo wa Mkoa ilisema Rais huyo na ujumbe wake watawasili nchini saa 11:00 jioni na kupokewa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere. Kandoro alisema baada ya mapokezi hayo, Rais huyo atakagua gwaride na vikundi mbalimbali vya ngoma vilivyoandaliwa uwanjani hapo na kupigiwa mizinga 21.

Hivyo aliwataka wakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumlaki mgeni huyo ili kuonyesha ishara ya upendo kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa. “Napenda kuchukua fursa hii kutoa mwito kwa viongozi na wananchi wote wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumlaki mgeni wetu huyu pale uwanjani ili kuonyesha ishara ya upendo tulio nao kwa viongozi wetu wa Kitaifa na Kimataifa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.


Alisema msafara wa Rais huyo utaelekea katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski kupitia barabara za Nyerere, Mandela, Buguruni, Uhuru, Mnazi Mmoja, Railway na Sokoine.

No comments: