Wednesday, February 20, 2008

“SISI SI MAGAIDI NA

SIYO WACHOCHEZI!



Kauli ya Wana Jambo Forums kuhusu Madai ya Kuhusishwa na mtandao wa Kighaidi na Kihalifu yaliyotolewa na Jeshi la Polisi February 20, 2008


“Matokeo haya yanaonesha hali halisi iliyopo Tanzania, hali ya uoga na ya kutojiamini inayowakumba Watanzania walio wengi wanapotakiwa kuelezea kwa uwazi maneno yale yale wanayoyanong’ona pembeni kwa hamasa kubwa. Kwa mtindo huu Taifa letu linaweza kuishia kuwa la walalamishi wasio na ujasiri wala dhamira ya dhati ya kukemea maovu pale inapobidi.”

Nukuhu kutoka Ripoti ya Kamati Teule kuhusu Richmond


Utangulizi:

Wanachama wawili wa tovuti ya majadiliano ya Jambo Forums wako mikononi mwa Polisi kwa madai ya kushiriki katika mtandao wa kihalifu, na kichochezi na kighaidi. Madai hayo yaliyotolewa na jeshi la Polisi leo siyo tu yanatukana akili za wanachama wengi wa Jambo Forums lakini pia yanaonesha ni jinsi gani Jeshi Letu la Raia wa Tanzania linaweza kutumika kama mtutu wa kulipua uhuru wa maoni, fikra, mawazo, na habari nchini.

Sisi ni nani?

Mtandao wa Jambo Forums ni mtandao huru ambapo Watanzania na wasio wa Tanzania wanashiriki kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa Taifa letu bila hofu yoyote, kwa uhuru na kwa uwazi kabisa, tukiweka maslahi ya Tanzania mbele kuliko maslahi yetu binafsi. Tafadhali angalia kiambatanisho “Ifahamu Jambo Forums”.

Madai ya Uchochezi:

Kwa mujibu wa Inspekta Jenerali wa Polisi na baadaye Msemaji wa Jeshi hilo aliyezungumza na BBC Jambo Forums inahusishwa na kauli za uchochezi na kuchafua sifa za watu n.k Ni ukweli kwamba baadhi ya mawazo ya watu yanawezekana kuwa ni makali na ambayo yanawaudhi watu wachache. Hata hivyo ni msimamo wa Jambo Forums kuwa “Hoja hujibiwa kwa hoja” na mtu yeyote ambaye anahisi kuwa kilichosemwa juu yake si kweli au cha kizushi anauhuru wa kuja hadharani na kuweka ukweli wazi au kumtumia mtu mwingine kufanya hivyo kwa niaba yake.

Hivyo madai ya uchochezi hayana msingi wowote isipokuwa kujaribu kujenga chuki na woga usio na msingi kwa wananchi wa Tanzania. Ni msimamo wetu kuwa wachochezi nchini ni wale waliokwapua fedha za umma toka Benki Kuu, walioliingiza kwenye Mkataba wa Richmond (hadi kuvunja baraza letu la Mawaziri) na wale ambao walishiriki kununu Rada kwa bei ya juu huku wakigawiana mabilioni ya fedha za Watanzania. Ni wachochezi wale ambao waliwapiga Watanzania kule Kiteto kwa sababu ya tofauti za kisiasa na ambao leo hii bila hata haya wanadiriki kusimama na kuwabebesha mzigo na dhambi zisizokuwapo vijana wawili wasiojua hili wala lile. Hawa ndio wanaochochea fikra za kujiona duni kwa Watanzania.

Madai ya Ughaidi

Kama kuna madai ya kichochezi na kizandiki ni ya kuihusisha forum hii na kitendo au mawazo yoyote ya kighaidi. Hakuna wakati wowote ule ambapo Jambo Forums imewahi kuvumilia kauli au mada yoyote ambayo inazungumzia matumizi ya nguvu kufikia maamuzi ya kisiasa. Hakuna mwanachama yeyote wa Jambo Forums ambaye ameachwa kuandika jambo lolote lile lenye kutishia uvunjaji wa amani, sheria, au kwa namna yoyote ile kutishia maisha ya binadamu mwingine yoyote. Kwa hili Polisi wanajaribu kumpa mbwa jina baya ili waweze kumuua!

Pia kuihusisha Jambo Forums na vitendo vya kighaidi ni kutukana akili za wanachama wake wengi ambao wamo ndani ya serikali, CCM, vyombo vya habari, makanisa, misikiti, vijijini n.k Kwamba watu hawa wote hawajui ughaidi ni kitu gani. Tunaamini kuwa maghaidi wa kweli ni wale wote ambao hadi leo hii wanaendelea kudunda mitaani wakiwa wamekula hela za umma ambazo zingeweza kutumiwa kutokomeza umasikini, magonjwa na ujinga. Hawa ndio ambao leo hii wangetiwa pingu na kina IGP Mwema.

Uhuru wa Maoni

Ni kauli za kejeli na ambazo zinaudhi kusikia kuwa Polisi wanadai wanaheshimu “uhuru wa maoni”. Kwa kadiri inavyoonekana maoni ambayo wanayataka wao ni yale yaliyopitishwa kwenye “litmus test” ya jeshi hilo na kumulikwa na darubini za CCP ili kuona kama ni maoni “safi, yanayopendeza, yanayokubalika, na ambayo yanaendana na mawazo ya serikali”.

Kitendo cha kuingilia kati mtandao huu ni jaribio la kwanza la wazi na dhahiri dhidi ya uhuru wa maoni ili kuhakikisha kuwa maoni ambayo si mazuri na yasiyosababisha watu wapige makofi hayatolewi hadharani.

Tunaamini kuwa haki ya Katiba inayotajwa kwenye Ibara ya 18:1, 2 ambayo inasema

Kuwa

“Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

(2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”

Katika ibara hiyo hakuna mahali popote panaposema kuwa ni maoni ya aina gani au mawazo ya aina gani ambayo mtu anaweza kuwa nayo. Na zaidi ya yote ibara hiyo inahakikisha kila raia anayo “haki ya kupewa taarifa wakati wowote kupitia chombo chochote”. Hivyo mashambulizi dhidi ya Jambo Forums ni mashambulizi dhidi ya haki za kikatiba ya “kila raia”

Kwanini Jambo Forums imelengwa?

Kimsingi tunaamini kuwa Forum yetu imeshambuliwa kwa sababu kubwa kadhaa.

1. Tumekuwa ni forum ya kwanza kuwa na ujasiri wa kuweka mikataba ya kifisadi kwa kila mwananchi kuona. Mikataba ya Buzwagi, Richmond, IPTL n.k iliwekwa hadharani kwenye jambo forums ambapo watu walikuwa huru kuiangalia, kuichambua na kuionesha ni jinsi gani haikuwa na maslahi kwa Taifa letu. Hili limewaudhi wale walioshiriki kwenye mikataba hiyo.

2. Kitendo cha Waziri Mkuu na Mawaziri wengine kujiuzulu na hatimaye kuvunjwa kwa baraza la Mawaziri ingawa kimetokana na jitihada za wazi za wabunge wa CCM kwa namna moja au nyingine kimehusiana na mafanikio ya forum hii kulichambua suala la Richmond katika vipande vyake vidogo vidogo na kulionesha wazi ni jinsi gani lilikuwa limejaa kila aina ya usanii!

3. Jambo Forums ilikuwa ni forum ya kwanza kuelezea na kuweka picha za viongozi wa upinzani waliopigwa kule Kiteto siku chache zilizopita na hivyo kuwaweka wananchi jinsi gani Jeshi la Polisi nchini siyo tu linakiuka haki za binadamu bali pia linajitahidi kuhakikisha watu hawajui vitendo vyake hivyo. Ni wazi kuwa mashambulizi haya ni jaribio la Polisi kulipiza kisasi.

4. Tunaamini kuwa Jambo Forums imekuwa na nguvu ya kuamsha mawazo na mabadiliko ya wananchi na kuwapa ujasiri wa kuhoji na kuhoji zaidi kauli za viongozi wao. Mara kadhaa sasa Jambo Forums imeweza kuzichambua kauli za viongozi kuzikebeki na kuzidhihaki na kuonesha kuwa ni kauli zisizo na msingi. Kwa viongovi ambao wamezoea kuimbiwa sifa na kupigiwa makofi kauli za “kupaa kwa ndege ya Lowassa” na nyingine kama hizo bila ya shaka zimewafanya wajione duni na hivyo wameamua kujitutumua.

Msimamo wetu.

  • Ni msimamo wetu kuendelea kuwa na mawazo huru na fikra huru na hatutosita kuzitoa fikra hizo mahali popote pale tukitumia haki zetu kama binadamu na kama raia.
  • Kitendo cha kukamata wanachama wenzetu wawaili kwa madai ya kupandikiza siyo tu ni kitendo cha kibabe bali pia kinaonesha ni jinsi gani serikali na vyombo vyake wameshindwa kwenye uwanja wa hoja na sasa wanaleta vihoja.
  • Kama kuna mtu yeyote anayedai kukashfiwa anao uhuru wa kuingia kwenye forum hiyo au kumwandikia administrator majibu yake na kuweka msimamo sawasawa. Hivyo Polisi kutumiwa na viongozi wa kisiasa au marafiki zao kunyamazisha mtandao huu ni kuonesha jinsi gani Jeshi hilo linasimama upande wa mafisadi.
  • Vijana waliokamatwa waachiwe mara moja kwani tunaamini wamekamatwa kama wafungwa wa dhamira (prisoners of conscience)
  • Kwa vile taifa letu hivi juzi lilisifiwa kuwa ni “mfano wa kuigwa” na Rais wa Marekani, jitihada zitafanyika ili kuonesha ni jinsi gani mabilioni ya Marekani yanaanza kutumika kuua uhuru wa vyombo vya habari na kuweka kizimbani haki za raia.
  • Tunakana mmoja mmoja na kama jumuiya mara moja na milele kuwa hatuhusiki kwa namna yoyote ile na kitendo/vitendo, neno, maneno, mawazo, jambo, maoni, hoja, n.k vinavyohusiana na uchochezi, uvunjaji wa sheria au vitendo vya aina yoyote ile vya kighadi kama ilivyosemwa na Polisi.
  • Tunataka badala ya Jeshi letu kutumia muda wake mwingi kupepeleza wana Jambo Forums, wahamishe juhudi zao katika kuwakamata kina Vithlani aliyetuuzia rada kwa kurusha, Jeetu Patel aliyekombwa fedha Benki Kuu, Daudi Balali aliyekuwa Gavana wa Benki hiyo, Gray Mgonja na wale wote ambao wametajwa kwenye ripoti ya Dr. Mwakyembe na kwenye orodha ya Mafisadi kuwa wamelisababisha Taifa letu hasara. Hawa ndio maghaidi nambari moja na ambao IGP Said Mwema na wenzake wanatakiwa kuwaambia wananchi kuwa wamewakamata na watawafikisha mahakamani.
  • Kitendo chochote cha kuwafungulia mashtaka vijana hawa kwa madai ya kuzusha tunakichukulia kama ni cha kiimla, chenye lengo la kuleta utawala wa hofu kwa wananchi.

Hoja hujibiwa kwa hoja!

Wana Jambo Forums

Msemaji wa Jambo: - jamboforums@klhnews.com

Simu: 1 248 556 6748


GONGOLA HAPA: CHADEMA WANAUNGA MKONO UHURU WA FIKRA NA KUTOA MAWAZO BILA KUINGILIWA NA NGUVU ZA DOLA



No comments: