Thursday, February 28, 2008


Tuhuma za ufisadi zinazowakabili baadhi ya vigogo wa serikali nchini, zimemuingiza kwenye ulingo Rais Jakaya Kikwete na kumuweka katika wakati mgumu wa kupambana nao, uchunguzi wetu umebaini...

Habari kutoka vyanzo mbalimbali zimesema kuwa, kuingizwa kwa rais ulingoni kunatokana na ukweli wa kuwepo kwa misuguano ya chini kwa chini baina ya serikali yake na kundi la mafisadi wenye lengo la kuficha uovu walioutenda.

Imeelezwa kuwa, wakati nia ya serikali ni kujisafisha, wahusika wa ufisadi wakiwemo waliojichotea mamilioni ya pesa kutoka Benki Kuu ya Tanzania BoT na wale wa Kampuni hewa ya Umeme ya Richmond wametengeneza mtandao wa kujihami na nguvu za dola.

Vyanzo vyetu vya habari vilisema hivi karibuni kuwa, umoja wa mafisadi umekuwa ukikutana kwa siri kupanga mikakati ya namna ya kuzima soo, huku taarifa zikikariri kuwepo kwa njama za kuwaingiza kwenye tuhuma za ufisadi za BoT na Richmond viongozi wengine wa ngazi za juu serikalini.

Imedaiwa kuwa, lengo la kufanya hivyo ni kuichafua zaidi serikali ili kuondoa ujasiri kwa wakerekewa wa mageuzi wanaoshabikia ‘walioitafuna’ nchi watiwe kitanzini.

“Mbinu zilizopo ni kuwapakazia viongozi wengine (hakufafanua kama na Rais Kikwete atakuwemo) ili ionekane kama watashughulikiwa basi na vigogo wengine waliopo madarakani nao waonekane walishiriki kwa namna moja au nyingine, yote ni kutaka kuonesha kuwa waliokosea si wao peke yao,” kilidai chanzo chetu.

Aidha, habari za kuaminika zilizolifikia Amani zilidai kuwa, mafisadi walifanya mkutano wao wa siri Juma lililopita ndani ya chumba namba 103 katika hoteli moja maarufu iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam ambapo walipanga mikakati mizito ya kujihami na mkono wa serikali.

Ilidokezwa kuwa, moja kati ya mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kumziba mdomo na kumzuia aliyekuwa Gavana wa BoT Daudi Ballali asirejee nchini kwa hofu ya kukamatwa na kuvujisha siri zitakazowasumbua katika kukabili kesi au tuhuma za ufisadi.

Ballali anahusishwa na upotevu wa shilingi bilioni 133 kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje ‘EPA’ kwa kipindi alichokuwa madarakani kabla hajatimuliwa kazi na Rais Kikwete.

Kufuatia mchezo huo mchafu unaochezwa na mafisadi, wachunguzi wa mambo ya kisiasa walisema kuwa, Rais Kikwete anakabiliwa na mambo mazito ya kiuongozi ili kuweza kutimiza azma yake ya kujenga serikali safi isiyokuwa na viongozi wenye mirija ya ki-unyonyaji.

Imeelezwa na wachunguzi hao kwamba, kauli za watuhumiwa zinazotolewa hadharani hazioneshi moyo wa kweli wa kuwajibika kwa makosa yao, jambo ambalo linaashiria kuwepo kwa makundi ya ‘hawa wabaya na hawa wazuri’ ndani ya chama tawala na serikali yake.

Tangu sakata la ufisadi liibuke hapa nchini, mengi yamesemwa kuhusiana na watuhumiwa walioifikisha nchi mahali pabaya ambapo siku za hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikaririwa na vyombo vya habari akisema atakula sahani moja na mafisadi.


No comments: